Shalom, jina la Bwana wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele. Karibu katika makala hii fupi na leo tupo katika sehemu ya pili (02) ya makala hii ya ANAYEENDA JEHANAM/KUZIMU KIBIBLIA, basi fuatana nami katika sehemu ya pili ya makala hii.
Kama tulivyotangulia kuona katika makala ya sehemu ya kwanza (01) kwamba, neno kuzimu katika biblia linaweza tumika kuwakilisha Jehanam (Hell), linaweza pia kutumika kuwakilisha shimo lisilokuwa na mwisho (Bottomless pit) na pia linaweza kutumika kuwakilisha kaburi (grave) hivyo tukutanapo na neno kuzimu wakati tunasoma maandiko ni lazima tutambue kuwa neno kuzimu hapo limetumika kuwakilisha nini. Hivyo katika makala hii tutatumia neno kuzimu kuwakilisha Jehanam (Hell) au neno Jehanam lenyewe.
JEHANAM/KUZIMU NI WAPI?
Ili tuelewe Jehanam/Kuzimu ni wapi, tusome kwanza andiko moja kwenye biblia ili tuelewe.
Luka 12:4 Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao WAUUAO MWILI, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi.
5 Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ANA UWEZA WA KUMTUPA KATIKA JEHANAM; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.
Maandiko yanasema kuwa, tusiwaogope wenye uwezo wa kuua mwili tu, bali tumwogope yule ambaye akiisha kuua mwili, anao UWEZA wa kumtupa mtu jehanam. Sasa mtu akiuwa mwenzake, ule mwili ufukiwa chini kisha baada ya hapo anakuwa hana uwezo wa kushughurika na roho. Lakini yupo ambaye mwenye uweza wa kushughurika na roho hiyo na kuitupa jehanam baada ya mwili kuzikwa kaburini, huyo ndo tunapaswa tumwogope. Sasa ni nani huyo mwenye UWEZA wa kumtupa mtu Jehanam/Kuzimu? Ni nani huyo mwenye funguo za kufungua jehanam/kuzimu na kumtupa mtu huko? Tusome.
Ufunuo 1:18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.
Kumbe Bwana Yesu Kristo ndiye mwenye funguo za mauti na kuzimu, ndiye mwenye UWEZA wa kutupa mtu huko na ndiye tunapaswa tumwogope. Hivyo, mtu ambaye hamwogopi Yesu Kristo huyo roho yake hutupwa kuzimu/jehanam. Sasa mtu ambaye hamwogopi Yesu Kristo huyo ni MTENDA DHAMBI.
Hivyo basi, Jehanam/kuzimu ni sehemu gani?
Ni sehemu ambayo, roho zote za watenda maovu (wasiomwogopa Mungu) huifadhiwa baada ya kufa kwao. Ikiwa na maana kuwa, kama roho za watu waliokufa katika dhambi zinahifadhiwa Jehanam/kuzimu, basi hata roho za watakatifu wanapokufa kuna mahali zinahifadhiwa na ndio maana wakati ule Stephano anauawa kwa kupigwa mawe, mwili wake ulikuwa pale lakini roho yake ilipokelewa na Bwana Yesu na kuhifadhiwa sehemu salama ambapo ni tofauti kabisa na kule ambao roho za watenda maovu zinahifadhiwa.
Matendo Ya Mitume 7:58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
59 Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, BWANA YESU, POKEA roho YANGU.
Hivyo basi, Jehanam/kuzimu ni sehamu ambayo roho zote za watu waliokufa pasipo kumtii Mungu huifadhiwa. Hadi hapo utakuwa umeshafahamu kuwa kuzimu ni mahali gani, basi fuata a nami katika sehemu inayofuata ya makala hii.
Bwana akubariki shalom.
MADA ZINGINEZO:
ANAYEENDA JEHANAM/KUZIMU KIBIBLIA (Sehemu ya 01)
JE! MAPAMBO YA VITO NI DHAMBI?
Je biblia inaruhusu kubatizwa kwa ajili ya wafu?(1Wakorintho 15:29)