Mariamu Magdalene alikuwa ni mtume? (Yohana 20:17) 

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: Je! Mariamu magdalene alikuwa ni mtume kwa kutokewa na Bwana Yesu pale alipoambiwa apeleke habari za kufufuka kwa Bwana kwa akina petro? Kwasababu mtume maana yake ni mtu aliyetumwa.  kama ni hivyo kwanini watu wengi wanapinga leo hii wanawake kuwa na makanisa? 

Yohana 20:17  Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.

18 Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo. 

JIBU: Ni kweli kabisa Mariamu Magdalene alitokewa na Bwana Yesu na kuambiwa aende kuwapasha habari watu juu ya kufufuka kwake, lakini kitendo hicho hakikumfanya yeye kuwa mtume, kwani Bwana Yesu kumwambia mtu apeleke taarifa fulani mahali fulani hakumfanyi mtu huyo kuwa mtume, kama ni hivyo hata yule mtu aliyeponywa na kuambiwa akajioneshe kwa makuhani angeitwa mtume, lakini biblia haijarekodi hivyo. Bwana aliwachagua mitume wake kumi na wawili miongoni mwa wanafunzi wake ambao wote walikuwa ni wanaume.

Luka 6:13  Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita mitume.

Mariamu magdalene alipotokewa na Bwana Yesu hakuambiwa kuwa, sasa nenda na wewe ukawe mtume, nenda na wewe ukasimame hekaluni na kufundisha, au nenda na wewe ukafungue kanisa, la! Bali aliambiwa aende akawapashe watu habari njema kumuhusu Bwana Yesu, kwani hata maandiko yanathibitisha kuwa, wanawake watangazao habari njema ni jeshi kubwa.

Zaburi 68:11  Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa; 

Lakini hii haimaanishi kuwa wakafungue makanisa huko na kuwa wachungaji, kwani kutangaza habari njema sio kwenda kufungua kanisa na kuwa askofu au mtume, wanawake wanaweza tangaza habari njema kama Magdalene alivyotangaza habari njema kwa wengine, wanaweza peleka habari njema kwa watu mbali mbali lakini si kufungua kanisa. Mamlaka ya kusimamia kanisa amepewa mwanaume tu.

Waefeso 4:11 Naye alitoa wengine kuwa MITUME, na wengine kuwa MANABII; na wengine kuwa WAINJILISTI na wengine kuwa WACHUNGAJI na WAALIMU;

 12 kwa kusudi la KUWAKAMILISHA WATAKATIFU, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 

Anaposema kuwakamilisha watakatifu maana yake ni kulikamilisha kanisa la Bwana Yesu, yaani wateule wa Bwana ambao wanakuwa chini ya usimamizi wa Maaskofu, wachungaji, Mitume, waalimu na Manabii. Na hata ukisoma biblia utagundua hicho kitu kwa makanisa mbali mbali ya kipindi hicho

Matendo Ya Mitume 13:1  Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli (Paulo) 

Utagundua kitu hicho pia kwa makanisa ya Uyahudini na Efeso n.k waliokuwa wakisimamia makanisa kwaajili ya kuwakamilisha watakatifu walikuwa ni wanaume na ndio waliopewa hayo mamlaka, lakini haimaanishi kuwa, hawakuwepo wanawake manabii, au wanawake wainjilisti n.k jibu ni la! Walikuwepo kwani hizo ni karama za Roho mtakatifu kwa kila atakayeamini, awe mwanamke awe mwanamume (Marko 16:17-18) lakini chini ya usimamizi wa hao watu tuliowasoma kwenye Waefeso 4:11-12  Maandiko yanathibitisha kuwa wanawake hawajapewa mamlaka ya kusimamia kanisa.

1 Timotheo 2:12  Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, WALA KUMTAWALA MWANAMUME, bali awe katika utulivu. 

Na sababu kubwa ya mwanamke kutopewa malaka ya usimamizi wa kanisa biblia imeisema sababu hiyo kwa uwazi kabisa kuwa, Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza na Hawa baadaye na Adamu hakudanganywa bali Hawa

1 Timotheo 2:13  Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.

14 Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa. 

Lakini hii haimzuhii mwanamke kufanyia kazi karama aliyopewa na Mungu kwani hata wakati wa kanisa la mitume, walikuwepo wanawake wakiwafundisha watu njia ya Bwana Yesu n.k lakini haikuwafanya wao wafungue makanisa na kuwa Maaskofu huko, hicho kitu biblia haijaruhusu.

Wengi wanatumia andiko la Warumi 3:22 kuhararisha wanawake kuwa na makanisa na kusimama MADHABAHUNI kufundisha na kuhubiri

Warumi 3:22 ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; 

Tofauti inayozungumziwa hapo ni ya sisi kuhesabiwa haki kwa Mungu kwa njia ya Imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwa watu walio wa sheria yaani wayahudi na sisi tusio na sheria yaani watu wa mataifa, hatuna utofauti wowote katika kuhesabiwa haki mbele za Mungu lakini si kwamba Mungu hana utaratibu katika kanisa lake.

Mama/dada unapopowe ujumbe na Bwana Yesu na kukwambia ufikishe katika kanisa, haimaanishi kwamba uende ukafungue kanisa, unapopewa ushuhuda fulani na kuambiwa fikisha kwa watu waishio duniani haina maana kwamba uende kufungua kanisa, fikisha ujumbe kama ulivyopewa na Bwana Yesu kama Magdalene alivyofikisha ujumbe. Kwa kulitambua hilo, Kuwa watu wengi watabisha na kupingana na kweli, Bwana mwenyewe aliagiza lakini hakutaka kumshurutisha mtu, alisema kuwa, kama ukitaka kuwa mjinga endelea kuwa mjinga.

1 Wakorinto 14:34  Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo.

 35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa.

 36 Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu? 

37 MTU AKIJIONA KUWA NI NABII AU MTU WA ROHONI, NA AYATAMBUE HAYO NINAYOWAANDIKIA, YA KWAMBA NI MAAGIZO YA BWANA.

38  LAKINI MTU AKIWA MJINGA, NA AWE MJINGA. 

Bwana akubariki. Shalom 

Mada zinginezo:

Kulingana na 1 Wakorintho 11:5 Mwanamke anaruhusiwa kusimama madhabahuni na kuhubiri (kufundisha)?


BASI WAKIWAAMBIA, YUKO JANGWANI, MSITOKE; YUMO NYUMBANI, MSISADIKI. 


Je! Kuna Mungu wawili? (Kulingana na Yohana 1:1)


 Je! Waraka wa mtume Paulo kwa Wakorintho, ulikuwa ni kwaajiri ya Wakorintho pekee?

LEAVE A COMMENT