Nakusalimu kwa jina kuu la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Nuru ya neema yake ikupe nguvu ya kuijua kweli ya Mungu na kuifuata. Amina.
Ili Bwana Yesu azaliwe zamani zile alipokuja katika mwili duniani na kuishi pamoja nasi ili kutuonesha njia na kutukomboa kwa kazi ya msalaba, kuna watu ilibidi waingie gharama kubwa sana; wengine walipoteza watoto wao kwa kuchinjwa (Mathayo 2:16), wengine iliwalazimu kutembea umbali mrefu sana kwenda kumuona mtoto Yesu na kutangaza kuzaliwa kwake Mwokozi wa ulimwengu, wale Mamajusi toka nchi za mbali (Mathayo 2:1-2) na wengine wengi.
Ila leo tujifunze kwa mtu mmoja aliyeitwa Yusufu (Baba mlezi wa Bwana Yesu).
Naomba tuweke sawa jambo moja hapa; Yusufu ndiye mbeba ahadi ya kuzaliwa Bwana Yesu na siyo Mariamu kama watu wengi wanavyomtukuza Mariamu leo. Ahadi ya Mungu ilikuwa Mwokozi atazaliwa katika ukoo wa Daudi (Yohana 7:42) na Yusufu ndiye aliyekuwa ukoo wa Daudi (Luka 2:4) hivyo yeye ndiye aliyebeba ahadi ya uzao wa Bwana Yesu, Mariamu alipata neema ya kumzaa Bwana Yesu kwa sababu alikuwa ameposwa na Yusufu (kwa lugha rahisi kwa sababu alikuwa mke wa Yusufu) sasa kama ingetokea Mariamu asingeolewa na Yusufu basi hiyo bahati ya kufanyika Mama wa Kristo asingeipata.
Tukirudi kwenye mada kuu, ni jinsi gani Yusufu alikubali apoteze vingi ili kuilea mimba ya mtoto Yesu aliyekuwa tumboni. Hebu fikiri katika hali ya kibinadamu amemchumbia mwanamke ambaye amekuambia hajawahi guswa na mwanaume na wewe mwenyewe hujakaribiana naye ukisubiri hadi ndoa ifungwe, halafu ghafla kwenye maandalizi ya kufunga ndoa unapata taarifa huyo mwanamke ana ujauzito na unathibitisha hilo mwenyewe, ni wazi kitakuwa kipindi kigumu sana kwako hasa kama ulimpenda sana na ndivyo ilivyomtokea Yusufu kwa Mariamu.
Yusufu alipotaka kumwacha Mariamu, Malaika wa Bwana alisema naye kwenye ndoto kuwa Mariamu hakufanya uzinzi bali ile mimba ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu ndipo Yusufu akakubali kuingia gharama ya kumlea mtoto Yesu kwa yeye mwenyewe kupoteza heshima yake na uaminifu katika jamii hasa miongoni mwa wacha Mungu wenzie.
Kama Yusufu angemwacha Mariamu basi ingempasa Mariamu auwawe kwa kupigwa mawe kwa dhambi ya unzinzi kwa kuwa ndivyo sheria ilivyokuwa inataka (Walawi 20:10) lakini kwa kuamua kumchukua mkewe basi alikubali yeye mwenyewe ndiyo aonekane mzinzi kwa kumuingilia mwanamke kabla ya kumuoa maana hakuna jinsi angeweza kuwashawishi watu kuwa ile mimba ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu hivyo Yusufu alikubali kudharilika jamii imuone kuwa alikuwa anajifanya mtakatifu kumbe ni mnafiki tu.
Gharama nyingine ni kumnyima mwanae wa kweli (yaani damu yake halisi) aliyezaliwa baada ya Bwana Yesu ambaye kiuhalisia huyo ndiye mtoto wa kwanza wa Yusufu haki ya mzaliwa wa kwanza (mtoto wa kwanza wa kiume wa Yusufu alikuwa ni Yakobo, soma Marko 6:3) lakini haki hiyo ya mzaliwa wa kwanza alipewa Bwana Yesu (Luka 2:22-24) yote hayo aliyafanya ili kumlinda mtoto Yesu. Lakini pia siyo kwamba matendo yote ya Bwana Yesu yalikuwa yanampendeza Yusufu, hapana, kuna mengine alikuwa anayavumilia tu, kwa mfano; lile tukio la Bwana Yesu alipokuwa mtoto kuwatoroka na kurudi hekaluni na kuwasababishia kuhangaika kumtafuta siku tatu alafu wanamkuta pale hekaluni wanamuuliza kwanini umetufanya hivi Yeye (Yesu) anawajibu “imenipasa kuwamo kwenye nyumba ya BABA YANGU” (Luka 2:42-50)
Mimi na wewe tumepata neema ya kuelewa ni nini Bwana Yesu alimaanisha kwa jibu lake hilo ila wakati ule Yusufu hakuelewa maana yake. Alikubali pia kuto kutumia haki yake ya kumkaribia mkewe hadi mtoto atakapozaliwa (Mathayo 1:24-25) pengine hadi alipoacha kunyonya kabisa. Yote hayo hayakumzuia Yusufu kumpenda mtoto Yesu na kumlinda kwa gharama yoyote ile asije kuonekana ni mtoto haramu lakini mwisho wa safari faida yake ilikuwa ni kubwa mno kwani familia yake ilikuja kuwa na utukufu na heshima nyingi kupita familia zote ulimwenguni kwa sababu ndiyo familia iliyomlea Bwana na Mwokozi wa ulimwengu.
Huo ndio mfano wa jinsi tunavyopaswa kuwa, pale unapompokea Bwana Yesu ni sawa na kuruhusu azaliwe ndani yako hivyo huna budi kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha anakuwa hadi kufikia utukufu wake kuwa dhahiri kwa wengine wote wajue kuwa kipindi wanakuona umepitwa na wakati kwa kuacha kuvaa nusu uchi na kuvaa nguo zako za kujisitiri mwili wako, wakati wanakudharau na kukusengenya kisa umeacha ulevi, hutukani tena kama wao, hujipambi tena kama wao, huambatani nao tena katika makusanyiko yao yasiyompa Mungu utukufu bali unakwenda ibadani kukusanyika na waliookoka wenzio ili kuzidisha maarifa ya kumjua Mungu.
Hayo yote umeyafanya kwa gharama ya maisha yako, kwa kujinyima na kujikana kusudi umruhusu Kristo akue ndani yako na jua tu Yesu hatabaki mchanga milele lazima atakua na akikua lazima adhihirishe kuwa Yeye ni Mungu muweza yote hivyo atarudisha heshima yako maradufu na vyote ulivypoteza kwa ajili yake hivyo utukufu wako wa mwisho utakuwa mkubwa kuliko wa mwanzo.
Ndugu Bwana Yesu akizaliwa ndani yako atabaki kuwa mtoto kwa muda akuone je utakuwa tayari kumlea kwa gharama ya maisha yako? Je, utakuwa radhi kutengwa hata na wazazi, ndugu na marafiki zako ili tu usimpoteze Yeye? Utakuwa radhi kupoteza kazi ili usimpoteze Yeye? Kipindi hiki huwa ni kigumu kwa kuwa mara nyingi hafanyi kama unavyotaka wewe, hakusaidii sana bali anataka wewe ndio umsaidie Yeye abaki ndani yako yupo kama mtoto mchanga ndani yako anataka umlinde asiuawe na wazazi wako, au ndugu zako au marafiki zako, au kazi yako, au tabia zako mbaya. Ukiweza kumlinda hadi akakua basi jua atakuwa na uwezo wa kukupa vyote hata usivyoomba.
Mathayo 19:29
Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.
Bwana akubariki.