KUFANYA MATENDO MEMA HAIMAANISHI KUWA UMESHAUPATA WOKOVU

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Nakusalimu Katika jina Kuu la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, Karibu tuyatafakari maneno ya uzima maadamu tupo duniani.

Kumekuwa na jambo moja ambalo tulio wengi hatulifahamu pale tunapodhani kuwa Kwa Wema wetu au kwa Matendo yetu mema tunayowatendea watu kwamba kwa hayo basi inatosha sisi kuhitimisha kwamba tayari tunao wokovu ndani yetu, Lakini hilo si kweli, ingawa Kweli Biblia inasema Tusisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.” (waebrania 13:16) lakini hapo haijahitimisha kwamba kwa matendo yetu hayo ndio tayari tumeshapata wokovu…

Sasa tutakwenda kuona mifano kadhaa katika Biblia ambayo kwa hiyo itatusaidia na sisi pia kujua mahali tulipo….. Mtu wa kwanza Tunamsoma ni yule Akida ambaye aliuguliwa sana na mtumwa wake kiasi cha kufa..Tunasoma..

Luka 7:2 Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana.

3 Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake.

4 Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, AMESTAHILI HUYU UMTENDEE NENO HILI;

5 maana, analipenda taifa letu, NAYE ALITUJENGEA SINAGOGI.

Sasa kama tulivyosoma hapo, kwamba huyu akida mtumwa wake alikuwa mgonjwa kiasi cha kufa, lakini aliposikia kwamba Yesu yupo katika mji huo, ndipo akawatuma wale wazee wakamuombe aje amponye mtumwa wake..Lakini hao wazee walipofika kwa Yesu wakaanza kumshawishi na kumnadi huyo akida, kwa kuuelezea wema wake mbele za Bwana, anaowatendea hao wayahudi na kusema “Bwana amestahili mtu huyu umponye mtumwa wake, kwa maana mtu huyu ni mwema sana, na tena analipenda sana taifa hili, na isitoshe, ametujengea na sinagogi tafadhali Bwana tunaomba sana kamponye mtumwa wake.” unaona hapo aidha walimbembeleza sana Bwana Kwa kuuelezea wema wake mwingi..na ndipo Bwana akakubali…Tuchukulie tu katika hali ya kawaida kwa mfano wewe kuna mtu amekufanyia wema mwingi sana… Ambao hutakuja kuusahau, halafu badae mtu huyo aliyekuwa akikutendea wema mwingi, akaja kupata tatizo fulani ambalo lipo juu ya uwezo wake, halafu wewe ukaja kujua hilo, na isitoshe mtu mwenye uwezo wa kumsaidia unamfahamu na tena aidha upo naye karibu sana,…Hebu fikiria ni namna gani utakavyouelezea wema wake mbele ya huyo mtu..

Bila shaka utamuelezea mambo mengi sana ilimladi tu kumshawishi ili autoe msaada wake Kwa huyo mtu mwema…Sasa ndivyo ilivyokuwa kwa hawa wazee wa kiyahudi walivyokuwa wanauelezea wema wa huyu akida kwa Bwana Yesu,…Sasa kumbuka Mtu huyu alikuwa mwema sana, alikuwa anawapenda sana wayahudi, kiasi cha kuwajengea sinagogi, tambua sinagogi ni nyumba iliyokuwa inajihusisha na maswala ya ki-Mungu, Hebu fikiria ni wema mkubwa kiasi gani huu, Bila shaka wayahudi wengi sana walimpenda mtu huyu…Lakini licha ya hayo mtu huyu hakuwa ameokolewa bado,..

Labda utauliza ni wapi biblia imesema hivyo.? Jibu ni kwamba huyu akida kumbuka yeye alikuwa sio myahudi bali alikuwa mmataifa anayeishi israeli na alikuwa ni kiongozi wa hicho kikosi cha askari wa kirumi, chini ya utawala wa kaisari… ikumbukwe kuwa Bwana Yesu Hapo kabla alikuwa akishughulika na watu wa taifa la israeli tu, na ndio maana mahali fulani tunaona yule mama mkananayo aliambiwa nilitumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya israeli (Mathayo 15:24) .. Na vile vile mahali pengine Bwana aliwakataza wale wanafunzi wasiende Kuhubiri kwa watu wasio wa israeli (Mathayo 10:6)

Kwahiyo hapo bila shaka tunajua kwamba kweli huyu akida alikuwa bado hajapata wokovu… Sasa jambo hili lipo kwa watu wengi sana, utakuta mtu ni kweli mwema sana tena anakubalika sana na watu wengi, kwa kujitoa kwake…Lakini sasa isihitimishwe kwamba tayari anao wokovu ndani yake,.. ndugu yangu yawezekana hata wewe unajitolea sana kwa watu kwa ajili ya matatizo yao, umesaidia sana yatima, umesaidia sana wajane, umesaidia sana, wasiojiweza, umesaidia sana wazee..Lakini hayo yote haimaanishi kwamba unao wokovu ndani yako hapana, bali wokovu ni kumkiri Bwana Yesu kwamba ni Bwana na mwokozi Wa ulimwengu.


Sasa hebu tukamuangalie mtu mwingine, ambaye yeye Pia alikuwa akifanya jambo jema sana la kimungu, kiasi kwamba mpaka Bwana Yesu alimpenda kwa jambo hilo.

Tusome…

Marko 10: 17 Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?

18 Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.

19 Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.

20 Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.

21 Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

22 Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

23 Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

24 Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

Umeona hapo? Huyu mtu aliye tajiri, baada ya kuona kuna kitu amepungukiwa katika nafsi yake na kitu hicho si kingine bali kukosa uzima wa milele ndani yake..akamfuata Bwana na kumuuliza nifanye nini ili niurithi uzima wa milele…Ndipo Bwana akamjibu wazijua amri.? Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, Mpende jilani yako kama nafsi yako N.K…Yeye akamjibu Bwana mbona hayo nimeyashika tangia utotoni mwangu,… umeona hapo..? Akiwa na maana, Kuwa tokea utotoni mpaka alipo hapo, kwamba yeye Wala hajawahi kuzini, hajawahi kuiba, kuuwa, kudanganya, kushuhudia uongo, wala hajawahi kuwakosea heshima baba yake na mama yake, Wala hajawahi kosa kuwapenda majirani zake..N.K…Hebu fikiria kama wewe ndio unaye mtoto wa namna hii utajisikiaje? si utajivunia sana hata majirani zako watakuwa wakikupa hata pongezi na kusema mtoto wako umemlea vizuri sana, yaani hatujawahi mkuta akisema uongo, wala hatujawahi muona na mwanamke, wala hatujawahi muona akiiba… wala hatujawahi muona akigombana na watu, aise mtoto wako ni mtulivu sana, na wengine Watakuambia hongera sana Mwenzetu Mungu amekujalia sana.. Maana kwa kizazi hiki kumuona kijana kama wako ni wachache sana.. Umeona lazima watasema tu hivyo, kwa maana mambo kama hayo ya wizi, kusema uongo, kuzini N.K…Hayakubaliki hata mbele za watu.. Sasa ndivyo ilivyokuwa kwa huyu mtu (Kijana) alikuwa mwaminifu sana kwa mambo hayo lakini, bado hajapata wokovu na ndio maana akamuuliza Bwana Yesu nifanye nni ili niurithi uzima wa milele.?…Sasa Bwana baada ya kuona ni mtu mwaminifu kwa kushika amri za Mungu, ndipo akagundua lipo jambo moja linalomkwamisha na kumpelekea kujihisi hana uzima ndani yake, ndipo sasa akaambiwa kauze vitu vyote kisha kawasaidie masikini na wasiojiweza halafu ndio unifuate… Lakini mtu huyu nadhani alifikiri na akaona huyu Yesu anataka kunifirisi sasa, na anataka kunifanya niwe fukara kabisa… Lakini kwa Bwana hakuwa na mpango huo bali alitaka kuona utiifu wa Neno la Mungu, kwa maana alijua mali ndizo zinazomzonga, kwahiyo angeitii ile sauti, basi wokovu angeupata.

Sasa jambo hili ndivyo lilivyo kwa watu wengi leo, utakuta kweli mtu sio mzinzi, sio mwizi, sio mtukanaji, havuti sigara, hanywi pombe, sio muongo, ni mkarimu sana, anavaa vizuri, hajichubuhi, sio msengechaji n.K..umeona tabia hizo ni njema sana na zinakubalika mbele za Mungu na kwa wanadamu pia,…Lakini sasa mtu huyu huyu ukimpelekea habari za wokovu wa Bwana Yesu, utakuta anapinga, na atakujibu mbona mimi nashika amri za Mungu, mbona mimi sio muuaji, mbona sio mzinzi, wala sio mwizi, huwa sisemi uongo N.K.. Na moyoni mwake anashuhudiwa kabisa nje ya Yesu Kristo uzima wa milele hakuna mtu atakaye kuwa nao. (Yohana 10: 28, 14:6)…Ndugu yangu inawezeka na wewe upo katika kundi hili, usijiridhishe, kwa kutokuzini kwako, wala usijiridhishe kwa kutokuwa mwizi, muuaji, msengenyaji, mtukanaji, N.K.. Na ukadhani kuwa hayo ndio yanatosha kukufikisha mbinguni, mkumbuke huyo tajiri yawezekana yeye alikuwa mwaminifu kwa mambo kama hayo kushinda hata wewe, lakini alijitambua kuwa hana uzima wa milele ndani yake…Mpokee Yesu ndugu yangu akufanye kuwa Mrithi wa ahadi zile ambazo Mungu ametuahidia kwa kumuamini Yesu Kristo, kwamba ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako

Mkumbuke pia mtu mmoja ambaye anaitwa kornelio, huyu yeye alikuwa tofauti kidogo na hao wengine, ambao tumekwishaziangalia habari zao…Sasa huyu kornelio hakuwa mpagani, bali alikuwa mcha Mungu sana, na tena alikuwa anasaidia sana watu,..embu tusome habari zake na kisha tutajifunza kitu..

Matendo 10:1 Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,

2 MTU MTAUWA, MCHAJI WA MUNGU, YEYE NA NYUMBA YAKE YOTE, NAYE ALIKUWA AKIWAPA WATU SADAKA NYINGI, NA KUMWOMBA MUNGU DAIMA

3 Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!

4 Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.

5 Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.6 Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.

Kama tulivyosoma habari zake Hapo juu, kwamba huyu kornelio alikuwa mkuu wa kikosi cha askari wa kirumi kilichoitwa kiitalia,…Mtu huyu alikuwa mwema sana, na mwenye kusaidia sana watu,..Licha tu ya kuwa mwema tunasoma, alikuwa akimcha Mungu sana, na kumuomba siku zote…ndipo Mungu akamtuma malaika kwake na kumpasha habari kwamba Sala zako, na sadaka zako ambazo ulizokuwa ukiwapa masikini na wasiojiweza, zimepata kibali mbele za Mungu, ndipo kornelio akashikwa na mshangao kwa jambo hilo..Baadae akaambiwa Tuma watu yafa wakamwite Petro, naye atakwambia yakupasayo kutenda…Na kumbuka pia ukisoma habari hiyo mbele kidogo utaona, petro naye alikuwa akionyeshwa na Mungu maono juu ya Mtu huyo, kwamba hana budi kwenda nyumbani kwake ili kumueleza njia za wokovu,..Swali je! Petro alipofika alimwambia nini kornelio na wenzake.? Tunasoma..

Matendo 10:34 Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;

35 bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.

36 Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote)…….………………………

….44 Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.

45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,

47 Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

48 AKAAMURU WABATIZWE KWA JINA LAKE YESU KRISTO. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

Umeona hapo.? licha ya kornelio Kuwa mwema kiasi kile, kuwa muombaji, na mwenye kumcha Mungu sana kiasi kile, lakini tunasoma bado alikuwa hajaupata wokovu wa Yesu Kristo, na ndio maana Mungu akamtuma Malaika kumwambia, Kwamba mambo yako yote, unayojishughulisha nayo, kwa kuwasaidia sana watu, na kumcha kwako Mungu na kusali kwako sana muda wote….Mungu amependezwa sana na jambo hilo, lakini tuma watu yafa, wakamwite Petro ili aje akwambie Yakupasayo kutenda….

Ndugu yangu inawezekana na wewe pia ukawa kama huyu kornelio, kwamba ni Mwombaji sana, ni mcha Mungu kweli kweli, muhudhuriaji sana wa kanisani, ni mwimba kwaya maarufu sana, ni msaidiaji sana wa watu.N.K..Lakini hayo yote haina maana, kuwa umeshaupata Wokovu, hebu jifunze kwa huyu kornelio licha ya kuwa na tabia zote hizo nzuri, lakini alipoletewa habari wala hakupinga na kusema hapana, mbona mimi namcha sana Mungu, nasaidia sana watu, huwa nafunga na kuomba kila siku, kwahiyo wala hayo sihitaji, imani yangu itaniokoa,..wala hakusema hicho kitu, bali Yeye alitii tu na mwisho wa siku akahubiriwa na kina petro na baadaye akampokea Roho Mtakatifu yeye pamoja na nyumba yake na kisha wakabatizwa kwa jina lake Yesu Kristo….Kwahiyo Usiridhike na matendo yako mema ukidhani kuwa ndio umeshaokoka, usiridhike na kuomba kwako na kufunga, ukidhani kuwa ndio tayari wewe umeshapata kibali cha kuingia mbinguni…Usiridhike kwa kuona kwako maono ukidhani kuwa ndio tayari unakibali mbele za Mungu..Mpokee Yesu kweli kweli, ili hayo mambo mengine ndio yafuate.. Na si kuridhika

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema.


Mada zinginezo:

JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA KORNELIO


Je! neno “Mego” linamaana gani katika biblia?


HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO.


Biblia ni nini? Je Neno hilo lipo katika biblia yenyewe?.


Neno konzi lina maana gani?


Neno konzi lina maana gani?

LEAVE A COMMENT