HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, jina la Bwana libarikiwe milele. Nakukaribisha tena katika wasaa huu wa kujifunza neno la Mungu. 

Moja ya tabia ya Mungu ambayo tunaisoma kwenye maandiko ni kuwa, kabla ya kufanya jambo lolote ni lazima kwanza awajulishe watumishi wake, tunathibitisha hilo katika.

Amosi 3:7  Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. 

Lakini licha ya kuwafunulia watumishi wake tu, Mungu pia huwa anatoa na mlango wa kutokea ikiwa amekusudia jambo baya, na anachofanya kwanza ni KULITUMA NENO LAKE.

Zaburi 107:20  Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. 

 Na endapo watu watakubali na kulitii neno lake basi watakuwa salama kutokana na ubaya alioukusudia, lakini endapo watu hawatotii neno la Mungu basi, wataangamia. Mfano, wakati ule Mungu alipokusudia kuwapeleka wana wa Israeli utumwani, alichokifanya kwanza ni kulituma neno lake kwa kupitia manabii kama Yeremia. Lakini pia hata wakati ule alipotaka kuiteketeza miji ya Sodoma na Gomora na ile iliyopo kandokando, alituma kwanza neno lake kwa Lutu na neno lenyewe lilikuwa hili.

Mwanzo 19:15  Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, ONDOKA, MTWAE MKEO NA BINTI ZAKO WAWILI WALIOPO HAPA, usipotee katika maovu ya mji huu. 

Unaona? Mungu alipokusudia kushusha moto na kiberiti kwenye hiyo miji, alituma neno lake kwanza ili watu waepukane na ghadhabu hiyo, na wale waliotii tu lile neno ndio waliopona lakini wale ambao hawakutii waliangamia wote.

Lakini pia, hata wakati ule wa Nuhu, kabla Mungu hajaigharikisha dunia ile, alituma kwanza neno lake kwa Nuhu na neno lenyewe lilikua ni hili.

Mwanzo 6:3  Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia. 

Soma tena

Mwanzo 7:1  Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. 

Unaona? Ni kanuni ile ile tu! ya kutuma kwanza neno kwanza ambayo Mungu anaitumia kabla ya kuleta uangamivu fulani. Vivyo hivyo basi, kuna uangamivu fulani ambao Mungu ameshauweka na kuutamka juu ya dunia hii ya sasa, labda tusome.

2 Petro 3:7  Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. 

Na tena katika 

Warumi 1:18  Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. 

Kama Mungu alimwambia Lutu kwamba naangamiza sodoma na Gomora au kama alivyomwambia Nuhu kuwa anaenda kugharikisha dunia ile ya wakati ule, ndivyo Mungu anavyowaambia na watu wote waishio sasa kuwa, HUKUMU YA MUNGU imeshadhihirishwa juu ya wanadamu, Mungu anawaambia wanadamu kuwa, mbingu na nchi za sasa zimewekewa akiba ya moto.  Lakini kama tulivyojifunza kuwa, kabla ya uangamivu huo, Mungu hutuma kwanza neno lake ili kuwaokoa watu, vivyo hivyo basi, katika hukumu hii, Mungu ametuma neno lake duniani ili watu waepukane na huo uangamivu kama mwanadamu atalikubari hilo neno la Mungu. Sasa maandiko yanasema kuwa, neno la Mungu ni Yesu Kristo.

Ufunuo 19:13  Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu. 

Hivyo basi, ili mwanadamu aepukane na ghadhabu ya Mungu ijayo, hana budi kulitii neno la Mungu, ili tuepukane na hukumu ya Mungu hatuna budi kumkubali Yesu Kristo kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu, na neno hili unalipokea kwa kuacha dhambi zako zote na kumwamini Bwana Yesu na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu sawasawa na matendo 19:5 matendo 10:48 1 Wakorintho 1:13 kisha kupokea kipawa cha Roho mtakatifu wake mtakatifu ambaye atakufanya kuwa mtakatifu na kukuongoza katika kuyajua maandiko matakatifu na kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari, washirikishe na wengine habari hii njema.


MADA ZINGINEZO

Pazia la Hekalu ni nini katika biblia?


NA HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO YONA.


Bado Bwana Yesu anasema nawe kwa mifano?

2 thoughts on - HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO.

LEAVE A COMMENT