NA HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO YONA.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Bwana wetu Yesu kristo. Bwana Yesu alisema katika

Matayo 12:41 Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwasababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.

Ukisoma maandiko utagundua kuwa Yona alimezwa na samaki kwa muda wa siku tatu na kutapikwa pwani na yule samaki, baada ya hapo alikwenda kuhubiri katika mji mkubwa wa Ninawi kuwa waache uovu wao kwani ulikua ni mwingi mno na ulipanda juu mbele za Bwana na Bwana alisema kuwa, endapo hawatouacha uovu wao na kugeuka basi baada ya siku arobaini mji ule ungeangamizwa. Na tunaona watu wa ninawi waliposikia yaliyo mpata Yona huko baharini na mahubiri yake kuwa waache uovu kwani ghadhabu ya Mungu itawajia wasipoacha matendo yao maovu ndipo wakamsadiki Mungu na mahubiri ya Yona na kufunga. Na habari zilipomfikia mfalme, naye akaamuru watu wote na wanyama wasile kitu bali waomboleze kwa kuvaa magunia na kwa kufunga ili kutubiaa uovu wao huo. Hebu tusome kidogo;

Yona 3:3 Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu.

4 Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.

5 Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.

6 Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.

7 Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;

8 bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake.

Watu wa Ninawi walitubu kwa mahubiri ya Yona na Mungu aliwasamehe uovu wao. Lakini Bwana Yesu alisema kuwa kizazi hiki kibaya kinatafuta ishara, hakitapewa ishara ila ishara ya Yona.

Luka 11:29 Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona.

Sasa ishara ya Yona ni ipi? Ishara na Yona ni pale alipokua tumboni mwa yule samaki kwa siku tatu na sisi watu wa kizazi hiki kibaya na cha zinaa tumepewa ishara hii ya Bwana kufa na kushuka kuzimu na siku ya tatu kufufuka.

Sasa utagundua kuwa baada ya Yona kutemwa na yule samaki na kwenda kuhubiri, watu wa Ninawi walitubu na kuacha dhambi zao, na sisi pia watu wa kizazi hiki, ni tangu lini Bwana afufuke? Ni takribani miaka elfu mbili sasa imepita na injili inahubiriwa kila siku lakini hatutaki kuacha dhambi. Kama watu wa Ninawi walitubu kwa mahubiri ya Yona, sasa imetupasaje sisi kwa mahubiri ya Bwana Yesu? Maana alisema “na hupa yupo mkuu kuliko Yona” hivyo basi kama ni kuomboleza inatakiwa iwe ni zaidi ya watu wa Ninawi kwani anayetuhubiria ni mkuu kuliko Yona.

Dada/kaka unayesoma ujumbe huu, ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa uache huo uzinzi na uasherati wako unao ufanya na hutaki kuacha? Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa acha huo ulevi na hutaki kuacha? Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa amini injili na kubatizwa katika ubatizo sahihi na hutaki? Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa acha hivyo vitendo vya rushwa unavyovifanya kazini kwako na hutaki?

Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa uache hivyo vimini, masuruali, make up, nywele bandia, kucha bandia na hutaki kuviacha? Ni mara ngapi umesikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa uache hayo matusi na hutaki? Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa uache huo usengenyaji na hutaki?

Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa uache kuzisujudia hizo sanamu na hutaki? Ni mara ngapi umeyasikia mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona kuwa uache kuwaomba hao wafu unaowaita watakatifu na hutaki? Basi leo fahamu kuwa ile siku ya hukumu watu wa Ninawi watakuhukumu kwasababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona ila wewe ulikataa kutubu kwa mahubiri ya aliye mkuu kuliko Yona.

Hivyo basi, ndugu yangu. Tubu leo na kuacha hayo maisha na kumgeukia yeye aliye mkuu kuliko Yona kuyakubali mahubiri yake kwani nafasi bado unayo sasa.

Aliye MKUU kuliko Yona akubariki.

Shalom.


Mada zinginezo:

Je! Hadi sasa kuna manabii wa Mungu?


Naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.


Maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ni yapi, kibiblia?(1Petro 2:2)


Neno Daawa linamaana gani kibiblia?

LEAVE A COMMENT