Je! Hadi sasa kuna manabii wa Mungu?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: Mbona Biblia inasema..

Mathayo 11:13
[13]Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana.

Maana yake ni kuwa manabii waliishia kwa Yohana mbatizaji, kuanzia hapo hakukuwa na nabii tena. Sasa iweje leo hii mseme kuna manabii?

JIBU:

Shalom.

Sio kweli kabisa, na hakuna mahali katika Biblia iliposema kwamba Yohana ndiye aliyekuwa nabii wa Mwisho, Bwana Yesu wala hajawahi sema Hivyo, na wala katika hivyo vifungu hakumaanisha hivyo. Bali biblia ilisema kuwa Yohana Alikuwa nabii aliyekuja kumtengenezea Yesu Kristo njia.

Tafakari hivi vifungu.

1 Wakorintho 12:28
“Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.”

Unaona hapo.? Biblia inasema kwamba Mungu ameweka Wengine katika kanisa na miongoni mwao ndio hao manabii

Soma na hapa..

Waefeso 4:9-11

9 Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?

10 Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote.

11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

Umeona na hapo pia inasema jambo lile lile, kwamba manabii wapo….Kwahiyo huduma zote unazoziona huko nje yaani Mitume, manaabii, waalimu, wainjilisti, wachungaji, N.K… Hizo Zote zinapaswa ziwepo katika kanisa la Mungu…Lakini Kumbuka kuwa kazi ya shetani ni kuupotosha ukweli ikiwa na maana kwamba kama kuna Manabii wa ukweli basi tambua na wa uongo pia wapo, kama kuna wachungaji wa ukweli basi na wa uongo pia wapo, kama kuna wainjilisti wa ukweli basi na wa uongo pia wapo.. Bwana Yesu alitoa angalizo hili..
👇🏾👇🏾

Mathayo 7:15-20
15 Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.

16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?

17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.

18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.

19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.

20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.

Mathayo 24:4-5,11
4 Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye.

5 Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.

11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.

Kumbuka kuwa huwezi kuwajua manabii wa uongo kama huwajui wa ukweli, kwasababu hata katika hali ya kawaida Utawezaje kuijua Kwanza noti bandia ilihali ile ya ukweli huijui, je utatumia Vigezo vipi kuithibitisha kwamba hii ni feki au orijino.? Na ndivyo ilivyo kwa manabii na watumishi wengine na hata makanisa, kwamba huwezi kuujua uongo kama ukweli bado huujui….Sasa swali je utaujuaje ukweli na ni nani atakyekujuza huo ukweli..?


Jibu lipo hapa

Yohana 16:13-14
13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, ATAWAONGOZA AWATIE KWENYE KWELI YOTE; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.

Umeona hapo kwenye mstari wa 13 unasema kwamba huyo Roho Atatuongoza katika Kweli yote na inasema kwamba huyo Roho hatanena kwa shauri lake bali Yote atakayoyanena yatatoka Kwa Yesu Kristo.

Sasa je huyu Roho Mtakatifu tunampataje.?


Jibu tunalipata hapa..

Matendo 2:38-40
38 Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.

40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.

Hiyo ndio kanuni ya kumpokea Roho mtakatifu; Kwanza ni Kutubu na kuachana na dhambi na kisha Kubatizwa kwa ubatizo sahihi wa maji mengi, ili upate ondoleo la dhambi na baada ya hapo ndio utampokea Roho Mtakatifu ambaye atakutia katika kweli yote ya maandiko na kukusaidia kuishinda dhambi…

Swali je wewe umekidhi hivyo vigezo.? nadhani jibu unalo ndani yako..Lakini kama bado nakushauri mgeukie leo hii Yesu Kristo ili ayaponye maisha yako, maana siku hizi ni za mwisho Hukumu ipo karibu kutokea, ishara zote zimeshatimia na kutuonyesha kwamba Yesu karibu anakuja Kuwachukua wateule wake…Fanyika kuwa miongoni mwa wateule wake ili upokee Roho mtakatifu..Biblia inasema…

Warumi 8:9
Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.

LEAVE A COMMENT