Maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ni yapi, kibiblia?(1Petro 2:2)

Maswali ya Biblia No Comments

Neno hilo utalisoma katika mstari huu;

1Petro 2:1 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.

2 Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”;

Kughoshi ni kubadilisha umbile, au kutia dosari, aidha kwa kuongeza au kupunguza kitu Fulani ili kionekane kama kile cha mwanzo, lakini kiuhalisia ni vitu viwili tofauti.

Leo watu wanaghoshi vyeti, wanaghoshi fedha, hata vyakula navyo vinaghoshiwa, ili vionekane kama vile vya asili. Kwamfano, unaweza kulishwa yai la kuku wa kisasa, pengine ukasikia ladha kama ya la kuku wa kienyeji, lakini mwilini mwako lisiwe na virutubisho vilevile ambavyo ungevipata katika yai la kuku wa kienyeji, Vilevile unaweza ukanyweshwa soda yenye ladha ya machungwa, ukadhani ni kweli yapo machungwa ndani yake, kumbe ni kemikali tu zimechanganywa.

Sasa tukirudi katika huo mstari mtume Petro anasema.. “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa”,

Ikiwa na maana kwamba maziwa Watoto wachanga wanayokunywa, yametoka moja kwa moja katika matiti ya mama zao, hayajachanganywa na sukari wala viwatilifu, wala virutubisho vingine..Bali ni moja kwa moja kutoka kwa mama bila kughoshiwa.

Ndicho ambacho Mungu anaachotaka kwetu, tunywe maziwa ya namna hiyo rohoni, ambayo ni NENO LAKE. (BIBLIA TAKATIFU), Tusilichanganye na mafundisho mengine ya wanadamu, tushike kile tu biblia inasema, kama inasema tuutafute utakatifu kwa bidii, ambao hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao (Waebrania 12:14), Basi tuzingatie hilo kweli kweli. Haijalishi mtu atakuambia utakatifu Mungu hautazami.

Inasikitisha kuona sikuhizi za mwisho, Neno la Kristo limeghoshiwa katika kila eneo, badala mafundisho yetu yalenge toba, ufalme wa mbinguni na utakatifu, yanalenga utajiri na mafanikio tu, uimbaji wetu badala uwe ni wa kumtukuza Mungu na kuhubiri injili, umegeuka kuwa wa singeli, na sebene..

Na sisi tusipokuwa makini, tutaishia kughoshiwa, na mwisho wa siku hatutakuwa kama ipasavyo, tutaishia kuwa wakristo vuguvugu na kwenda Jehanamu.

Katika zama hizi za manabii wengi wa uongo Penda kusoma biblia, na kuiishi biblia. Usiishi kwa maneno ya mwanadamu yeyote.

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *