Juya ni kitu gani katika biblia?(Mathayo 13:47)

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

Juya ni wavu wa kuvulia samaki, kwa jina lingine unaitwa Jarife.


Neno hilo ni maarufu katika habari hii ambayo aliizungumza Bwana Yesu, Tusome;


Mathayo 13:47 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;
48 hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa.
49 Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki,”


Utalisoma pia katika mstari huu Habakuki 1:15-17.
Habari hiyo inatisha, kwasababu, Bwana Yesu anaeleza mwisho wa dunia utakavyokuja kuwa kwa kufananisha na mvuvi ambaye anavua samaki, bila kuchagua, ni samaki yupi ataingia katika juya (wavu) yake, atakuja kujua wakati ambapo tayari ameshawatoa nje. Ikiwa kuna vyura, konokono, minyoo, samaki, atajua watakapovunwa.


Kuonyesha jinsi mavuno ya mwisho yasivyo chagua, watu wote tutavunwa..haijalishi wewe ni mwema au mwovu, hutanusurika wala kusahaulika.. Sasa ikiwa wewe ni mwema, utakwenda mbinguni, siku ile ya ufufuo itakapofika, kwa tukio linaloitwa unyakuo. Ikiwa utakutwa hai, lakini ikiwa ulikufa kabla ya huo wakati utafufuliwa, na kuungana na walio hai, na moja kwa moja mtakwenda mbinguni kwa Bwana.


Lakini ikiwa wewe ni mwenye dhambi, utabaki, hapa hapa duniani katika dhiki kuu ya mapigo ya Bwana (Ufunuo 16) na kama utakuwa umekufa, utakuja kufufuliwa na kuhukumiwa na kutupwa katika lile ziwa la moto.


Kwahiyo tulifakaripo Neno hilo, tukumbuke kuwa wakati wa mavuno sote tutavunwa, kama vile juya livualo samaki wote baharini bila kuchagua, Kikubwa tujue ni upande upi tutaangukia.


Ufunuo 14:15 “Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa.

16 Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa”.


Swali ni je umeokoka? Je umemaanisha kumfuata Yesu kwa moyo wako wote? Una habari kuwa hizi ni nyakati za mwisho, na kanisa tunaloishi ndio la mwisho lijulikanalo kama Laodikia? Ikiwa bado hujamkiri Kristo, basi geuka tubu dhambi zako, na yeye atakupokea.

Shalom.


Mada zinginezo:

Neno Daawa linamaana gani kibiblia?


Biblia inamaanisha nini kusema “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa,”


Kumkufuru Roho Mtakatifu kukoje?


IFAHAMU HUDUMA YA MWANAMKE “MZEE “KATIKA KANISA.

LEAVE A COMMENT