NINYI MMEKUWA RAFIKI ZANGU MKITENDA NIWAAMURUYO.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo apewe sifa milele na milele. Karibu tujifunze maneno ya uzima kwaajili ya wokovu wa roho zetu siku ile tutakapokufa na kuacha kila kitu hapa duniani (kama Bwana atakua bado hajarudi maana hatujui siku wala saa atakayorudi Bwana wetu).     Maandiko yanasema katika

Yohana 15:14   Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. 

Bwana Yesu alisema kuwa tukiyatenda aliyotuamuru, basi tumekuwa rafiki zake, sasa wote tunafahamu kuwa kinyume cha rafiki siku zote ni adui, lakini endapo ikitokea ukaangukia katika mikono ya adui yako, ambaye unafahamu kuwa anao uwezo kukuzidi wewe basi unaweza tengeneza picha ni kitu gani ambacho kitakukuta, kwa hali ya kawaida si kitu kizuri, ni kitu kibaya sana. 

Hivyo basi kama wewe huyatendi yale ambayo Bwana ameamuru, basi jua wewe ni adui wa Bwana kama ambavyo alivyosema kuwa tutakua marafiki zake kama tukiyatenda aliyotuamuru. Hadi hapo utagundua kuwa, ili tuwe marafiki wa Bwana sharti sio kumwamini na kubatizwa tu bali kuyafanya na yale aliyotuagiza. Swali ni je! Wewe mkristo uliyeokoka unayafanya yale ambayo Bwana aliyokuagiza? Kama jibu ni la! Basi fahamu kuwa wewe ni adui wa Bwana. Biblia inasema katika

1 Wakorinto 7:10  Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe; 

11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe. 

Bwana ameamuru kuwa mke asimwache mumewe na mume asimwache mkewe kwa sababu yoyote ile isipokua ya uzinzi, lakini wewe unayejiita mchungaji, mwalimu, nabii, shemasi, umeachana na  mkeo kwasababu tu mmechokana, basi fahamuni kuwa ninyi ni maadui wa Bwana na kitakachowapata mnakifahamu, wewe mama uliyeokoka na huku umemuacha mumeo kwasababu tu amefilisika tambua kuwa wewe ni adui wa Bwana hivyo tubu na kurudiana na huyo mumeo.

Bwana pia aliamuru tupendane katika

Yohana 15:12  Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. 

 Lakini wewe mkristo uliyeokoka una mwaka wa tano sasa husemezani na ndugu yako hapo Kanisani, una wiki mbili husalimiani na jirani yako pale nyumbani, basi fahamu kuwa wewe ni adui wa Bwana hivyo nenda ukapatane na hao usioelewana nao 

Biblia inasema tena katika 

1 Wakorinto 14:34  Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo. 

35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa. 

36 Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu? 

37 Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana. 

Maagizo ya Bwana yamekukataza wewe dada/mama kusimama mbele za madhabahu katika kanisa (penye mkusanyiko wa wanawake na wanaume) na kuanza kufundisha, na biblia imesisitiza kama ukijiona ni nabii sana au ni mtu wa rohoni fahamu kuwa hayo ni maagizo ya Bwana lakini wewe htaki kusikia, hivyo fahamu kuwa wewe ni adui wa Bwana, tubu leo na uache hiyo tabia.

Tena Bwana alisema katika 

Matayo 5:28  lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 

Alisema kuwa ukimtazama mwanamke na kumtamani basi jua umekwisha zina naye moyoni mwako hivyo hupaswi kufanya hivyo, lakini wewe kijana uliyeokoka, usiku mzima unakesha kutazama pornography na picha za uchi hivyo kukupelekea kufanya uzinzi moyoni mwako, basi fahamu kuwa wewe ni adui wa Bwana hivyo tubu leo na uache hivyo vitendo haraka maana maandiko yanasema

Nahumu 1:2  Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; Bwana hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira. 

Isaya 66:14  Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake, naye atawaonea adui zake ghadhabu. 

Hivyo mpendwa, kama ulikua ni adui wa Bwana kwa namna moja au nyingine kwa kutokuyafanya aliyokuamuru kutokana na sababu ya uelewa wako ni mdogo, basi geuka leo ukayafanye aliyokuamuru na kuwa rafiki wa Bwana. 

Bwana akubariki. Shalom 

LEAVE A COMMENT