IFAHAMU HUDUMA YA MWANAMKE “MZEE “KATIKA KANISA.

  Mwanamke, Uncategorized

Shalom.


Yapo maagizo mengi sana ya Bwana juu ya namna impasavyo mwanamke wa kiKristo kuenenda. Lakini leo tutaangalia juu ya huduma/wajibu wa mwanamke mzee katika kuukamilisha mwili wa Kristo (kanisa).


Mwanamke mzee tunayezungumzia siyo lazima awe tu yule kikongwe au mwenye mvi kichwani,  hapana bali mwanamke yeyote mwenye umri wa makamo, ambao wengi wao wanajulikana kuwa wenye vyeo vya “umama au mke” katika familia zao, hao pia wanatambulika kama wanawake wazee. Sasa hii pia haimaanishi kwamba kama wewe ni binti basi huna cha kujifunza katika somo hili, hapana. Kama vile tu mama nyumbani anavyomfundisha binti yake majukumu ambayo kwakawaida ni yake na kumuachia siku mojamoja atunze nyumba asipokuwepo, vivyo hivyo na hapa binti wa kiKristo unapaswa kujifunza ili kujijengea msingi mzuri kwa baaadaye.


Tunasoma katika kitabu cha Tito 2:3-5

3 Vivyo hivyo na WAZEE WA KIKE wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;

4 ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;

5 na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao .wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.

Leo hii tunaishi katika jamii yenye mporomoko mkubwa sana wa maadili, hususani tabia chafu kwa watoto wetu, kuibuka kwa wake wavivu, wakaidi, wasengenyaji, wenye madharau n.k. na  utaona kundi lidhihirishalo tabia hizi ni la wanawake vijana kwa asilimia kubwa,

Lakini na ni haohao ndio wenye jukumu la malezi kwa watoto  wao lakini hawalichukulii kwa uzito. Imekuwa kawaida kuwaona watoto sikuhizi wanatukana, wanavaa nusu uchi, wamejaa miziki ya kidunia kichwani na hawana neno la Mungu ndani yao, Na mama zao hawana habari, wanashinda kwenye masaluni, na kwenye mabaraza kuzungumza habari zisizostahili.


Sasa Bwana kwa kulijua hilo alituandikia mapema na kutoa majukumu kwa wanawake wazee, juu ya wanawake vijana , ili jina la Mungu lisitukanwe. Pengine leo hii unapishana na vijana hawa wa kike wasio na maadili na huoni hasara yoyote wanayoileta katika kanisa la Kristo,

Kwamfano utakutana na mabinti wengi ambao mienendo yao kanisani haipendezi hata kidogo, kiasi kwamba hata watu wa nje wakiwaona, wanasema kama ukristo ndio ule ni heri nibaki kama nilivyo. Utakutana na binti anakatiza mitaani na vimini na suruali, mfano wa wale wahudumu wa baa. Na bado huyo huyo ni mwimbaji kwaya kanisani, utajiuliza tatizo ni nini? Je ni mzazi, au mchungaji, au nani?

 Sasa kwa vyovyote vile mwanamke mzee huwezi kukwepa lawama au hukumu juu ya hili ikiwa jina la Mungu linatukia kwa uzembe wa kutokutimiza wajibu wake kanisani.
Au labda unasema kizazi hiki hakisikii hawatanisikia mimi, je! umejaribu kwanza kuangalia mwenendo wako binafsi? Je, Wewe mwenyewe unaishi maisha matakatifu ya kuikataa dhambi? Bwana alilijua hili kwamba ili uweze kuwa na ushawishi kwanza wewe mwenyewe uwe na mwenendo mwema, Tito2:3-4.


Mama, Bwana amekupa huduma kubwa sana katika kanisa, unapotimiza wajibu wako huu wa kuchunga mienendo ya mabinti, unaokoa ndoa zao, unaokoa watoto ambao ndio kizazi cha baadaye, unapunguza wimbi la vijana waasherati, unaliheshimisha kanisa la Kristo, jina la Mungu linabarikiwa kwa sababu yako,  . Huna haja ya kusimama kuhubiri kama mchungaji au askofu, Kristo anautambua mchango wako na anauheshimu kama anavyouheshimu ule wa mchungaji au askofu. Usikae mbali na Baraka za Bwana, timiza wajibu wako.
Bwana akubariki.


Tafadhari washirikishe na wengine

LEAVE A COMMENT