Nini maana ya “Msitweze unabii”? (1 Wathesalonike 5:20)

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

1 Wathesalonike 5:18 shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.  19 Msimzimishe Roho;  20 msitweze unabii;

Neno kutweza maana yake ni ‘kupuuzia au kudharau’ jambo fulani.

Hivyo hapo inaposema Msitweze unabii inamaanisha kuwa tusipuuzie unabii. Kumbuka Biblia ni kitabu cha kinabii, ambacho sio tu kinaeleza habari ya mambo yaliyokwisha kutukia au yanayoendelea sasa hivi..Bali pia  kinaeleza juu ya mambo mazuri na mabaya yanayokuja huko mbeleni.

Hivyo hatupaswi kupuuzia unabii wowote biblia unaotuonya juu ya siku zijazo, Iwe ni za mbinguni, au za kuzimu. kwamfano katika habari hiyo Mtume Paulo alilenga sana sana katika unabii wa siku za mwisho, ambao aliuzungumzia katika mstari wa kwanza kabisa wa sura hiyo ya 5, alisema..

1 Wathesalonike 5:1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Na ndio sasa baadaye kidogo katika mstari wa 20 akasema, “msitweze unabii”..Yaani msipuuzie, juu ya unabii huo.

Lakini leo hii inasikitisha kuona kundi kubwa la watu ambao ukiwahubiria juu ya kurudi kwa pili kwa Yesu Kristo na mapigo ya mwisho, na Jehanamu ya moto, badala waogope na kutetemeka, utaona ndio wanadhihaki na kupuuzia. Wengine watakuambia umerukwa na akili, wengine watasema hizo ni habari za uongo, mbona miaka nenda rudi, tumekuwa tukisubiria mambo hayo na halijawahi kutokea hata moja, iweje lije kutokea wakati huu.

Lakini ndugu yangu, kama Biblia isemavyo wakati watu wasemapo kuna amani na shwari ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, ndivyo itakavyokuwa juu ya siku za mwisho. Ghafla tu, watashangaa watakatifu hawapo duniani, wameshakwenda kwenye unyakuo. Halafu mpinga-Kristo ananyanyuka duniani, Hapo ndipo watalia na kujuta kwanini walipuuzia Neno la Mungu lilipokuwa likiwaonya tangu zamani, kwamba watubu mwisho wa dunia umekaribia.

Hivyo na sisi tunaoishi sasa, tusipuuzie Unabii wowote wa kibiblia. Kwasababu kama Bwana alivyosema mbingu na nchi zitapita lakini maneno yake, hayatapita kamwe. Ni kweli vyote vilivyoandikwa ni lazima vitimie.

Maran atha.

LEAVE A COMMENT