KWANINI MNANIITA BWANA, BWANA, WALAKINI HAMYATENDI NISEMAYO?

Biblia kwa kina, Uncategorized No Comments

Shalom ndugu yangu mpendwa katika Bwana, karibu tujifunze maneno ya Uzima ya BWANA wetu na MUNGU wetu Yesu kristo kama Tomaso alivyotuthibitishia katika

Yohana 20:28 Tomaso akajibu, akamwambia, BWANA wangu na MUNGU wangu!

Sasa utagundua kuwa, dunia hii tunayoishi sasa sio ile ambayo BWANA aliikusudia na hiyo ni kutokana na dhambi ambayo iliingia duniani pale Edeni. Sasa MUNGU alikua na mpango mwingine wa kurejesha dunia katika hali ile ile kama iliyokuwepo pale Edeni na hata zaidi na kuondoa dhambi na kumfanya mwanadamu aishi maisha yale ya kwanza walioishi wanadamu wa kwanza pale Edeni kama alivyotabiri katika Isaya 65:19-25

Sasa mpango huu ulimuhitaji Bwana kutoa nafsi yake kwaajili ya dhambi zetu ili tuokoke na dunia hii.

Wagalatia 1:4 ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.

Sasa Bwana alishafahamu ni mambo gani ambayo mwanadamu akiyafanya ataweza okolewa na dunia hii mbovu, na mambo hayo aliyafundisha yeye mwenyewe na mengine aliagiza na kutukumbusha kupitia mitume wake na watu wote waliomwamini aliwaagiza kuyafanya hayo yote aliyoyasema.

Lakini Bwana alisema hivi katika

Luka 6:46 Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?

Hiyo sentesi inamaanisha kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kuyatenda aliyoyasema na sio kumwita Bwana, Bwana tu. Na pia inaonyesha kuwa kuna hasara kubwa sana endapo tusipo yatenda. Hii ni kumaanisha nini? Hii ni kumaanisha kuwa, wapo watu wengi sana siku hizi ambao wanamwita Bwana, Bwana lakini yale asemayo, hawayatendi. Sasa hawa watu wengi miongoni mwao wapo ambao ni watumishi wa Bwana kabisa, wananena kwa lugha, wanatoa mapepo, wengine ni waalimu, wahubiri, wachungaji, manabii, mitume n.k lakini hawayatendi yale Bwana aliyoyasema na ndio hao watakao kuja kutimiza unabii ambao Bwana aliutoa katika

Mathayo 7:21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.

Ukisoma mstari wa 22 Bwana alitabiri na kusema “wengi wataniambia siku ile” sasa aliposema wengi hakumaanisha kuwa ni watu kumi au mia moja, hapana! Ila ni wengi sana.

Wewe mchungaji ambaye hutaki kutenda ambayo Bwana aliyaagiza jitahidi utubu na urekebishe usije ukawa mmoja wapo wa watakao timiza unabii huu, wewe kaka uliyeokoka fanya aliyokuagiza Bwana wako, acha huo uasherati wako na ulevi wako usije ukapatikana na madhara baadaye, wewe mwalimu usiyetaka kuwafundisha watu nini Bwana ameagiza, tubu na ujirekebishe kwamaana unawafungia watu Wengi ufalme wa Mbinguni, na wewe mwenyewe OLE ile ya Mathayo 23:13 itakuhusu.

Wewe nabii unaye wafariji watu kuhusu mambo ya mwilini na huku unaacha kuwaambia hatari itakayowapata baadaye kwa kutokuyafanya Bwana aliyoyasema tubu na uwaonye watu kwa faida ya nafsi zao.

Bwana ametuambia mengi mno ambayo tunapaswa kuyafanya hadi atakapokuja, lakini leo hii watumishi wengi wa Mungu wanakuwa wakwanza kuyapinga kwa kutumia fahamu zao wenyewe kwa kisingizio kuwa huo ni ukristo wa zamani na kutimiza haja za miili yao wenyewe na kukosa unyenyekevu. Wewe unayejiita mtumishi wa Mungu na huku hutaki kutenda mambo ambayo Bwana amekuagiza fahamu kuwa wewe sio wa Mungu kama ilivyoandikwa katika

Yohana 8:47 Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.

Aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu ila yeye asiyeyasikia huyo sio wa Mungu. Sasa utagundua kuwa hayo maneno Bwana hakuwaambia walevi, wala waasherati wala makahaba, ila aliwaambia mafarisayo ambao walikua wakimtumikia Mungu, hivyo hata wewe unayejiita mwalimu, mchungaji, nabii n.k fahamu kuwa huo mstari unakuhusu wewe, usiposikia maneno ya Mungu kuhusu ubatizo sahihi basi jua wewe si wa Mungu ndo mana huwezi kusikia, usiposikia maneno ya Mungu kuhusu utakatifu basi fahamu kuwa wewe si wa Mungu, usiposikia maneno ya Mungu kuhusu mapambo katikati ya Kanisa basi kuwa jua wewe sio wa Mungu

Hivyo ndugu yangu, katika siku hizi ambazo Bwana yupo karibu sana kurudi, jitahidi kuyatenda yote aliyoagiza na mapenzi yake kwa uvumilivu ili tupate ile ahadi ya uzima wa milele

Waebrania 10:36 Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.

Bwana akubariki. Shalom!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *