Itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa Mbinguni.

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

Swali: Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema itakuwa shida kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mbinguni? Je! matajiri hawatoenda Mbinguni? Ni vibaya mtu kuwa na mali nyingi (tajiri)

Matayo 19:23  Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. 

Jibu: Shalom, jina la Bwana lipewe sifa. Bwana Yesu katika mstari huo hakukataza watu wawe matajiri kwani ata yeye mwenyewe alikua na wanafunzi ambao ni matajiri mfano Yusufu aliyeuondoa mwili wake pale msalabi na kuupeleka kaburini

Matayo 27:57   Hata ilipokuwa jioni akafika mtu TAJIRI wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu; 

Kama Bwana angekataza wanafunzi wake wasiwe matajiri basi ni wazi kuwa, huyu mwanafunzi angemwambia aache huo utajiri wake.

Lakini Bwana alichomaanisha ni nini sasa katika mstari huo? Alichomaanisha Bwana ni kuwa mtu ambaye anategemea mali, mtu ambaye moyo wake wote upo kwenye mali alizonazo, mtu kama huyo ni kazi sana kuingia katika ufalme wa Mbinguni. 

Marko 10:24   Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! 

Mtu ambaye anaona mali zake ni kila kitu kuliko kufanya mapenzi ya Mungu, mtu ambaye tegemeo lake na la maisha yake ni katika mali alizonazo na wala si katika Mungu wake, mtu kama huyo ndiye ambaye Bwana anamzungumzia, watu ambao wanapenda fedha na mali wanafarakana na Mungu na ndio maana maandiko yanasema katika 

1 Timotheo 6:10   Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. 

Ukimsoma mtu kama Ayubu kwenye maandiko, alikuwa ni mtu tajiri lakini kamwe moyo wake haukuwa kwenye  mali zake alizokuwa nazo bali ulikuwa kwa Mungu tu. Ukimsoma Ibrahimu kwenye maandiko ailkuwa mtu tajiri lakini moyo wake ulikuwa kwa Mungu tu, wala hakuzitumainia mali alizokuwa nazo na maandiko yanasema kuwa aliishi kama mpitaji tu hapa duniani akiutazamia ufalme na utajiri unaodumu

Sasa wewe kama mwanafunzi wa Bwana Yesu, mtu uliyeokoka na kubatizwa katika ubatizo sahihi na kupokea kipawa cha Roho mtakatifu lakini ni tajiri, si dhambi wewe kuwa na hizo mali nyingi isipokuwa usijivune na wala usizituainie mali ambazo hazidumu kwani utaziacha tu bali mtumainie Bwana ambaye aliyekupa vyote.

1 Timotheo 6:17  Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. 

18  Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; 

19   huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli. 

Hivyo basi, hata wewe ambaye huna mali nyingi sana lakini moyo wako upo kwenye hizo mali na si kwa Mungu wako basi acha kuvitegemea hivyo na kuweka moyo wako kwenye hivyo bali uweke kwa Bwana Mungu atupaye vyote kadiri ya uwezo wetu.

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

Kivipi tunafarakana na imani kwa kutamani fedha?


Koga ni nini katika biblia?


UMEPATA FAIDA GANI?


Nini maana ya wanawake saba watamshika mume mmoja?( Isaya 4:1)


WEWE HU MBALI NA UFALME WA MUNGU.

LEAVE A COMMENT