Kutabana ni nini katika maandiko? (Mika 5:12)

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: Nini maana ya kutabana katika biblia kama tunavyosoma katika Mika 5:12 

JIBU:  Shalom,  jina la Mwokozi wetu na Mkuu wa uzima Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele.  Neno kutabana tunaweza lisoma katika

Mika 5:12   nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana; 

Kutabana ni kitendo cha mtu kufanya unajimu au uaguzi kwa lugha rahisi tunaweza sema mtu anayetabiri mambo yajayo kwa njia za kiganga na kichawi, kwa kupiga bao n.k   Sasa kufanya vitu hivi ni sahihi? Au Mkristo kwenda kwa watu wanaofanya hivyo vitendo ni sahihi? Jibu ni la! Si sahihi hata kidogo kwa mtu kufanya vitendo hivyo na wala kwa Mkristo kwenda kwa watu hao kwani ni dhambi na machukizo mbele za Mungu.

Kumbukumbu La Torati 18:10   Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, 

11  wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. 

Wakristo wengi leo hii wanasema wamempa Bwana Yesu maisha yao lakini bado wanaenda kwa hawa watu wenye kutabana, bado wanaenda kwa waganga na kibaya zaidi wengine ni wachawi na washirikina, ndugu yangu kama wewe ni Mkristo na bado unajihusisha na mambo hayo ni bora uache mara moja kwani ni machukizo makubwa sana mbele za Bwana. Wewe Mkristo unayeng’an’ania uchawi ni bora uache kwani Bwana alishakupa onyo katika

Malaki 3:5   Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi. 

Acha kwenda kwa waganga kupiga bao, acha kwenda kwa waganga wewe dada kumloga mume wako akupende, acha kwenda kwa waganga na wachawi kuwaloga majirani zako, acha kwenda kwa waganga kupiga ramli ndugu, kwani hayo ni machukizo mbele za Bwana na wachukizao maandiko yanasema sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto na kiberiti.

Ufunuo 21:8  Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili. 

Lakini kama bado hujamwamini Bwana Yesu na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu (matendo 10:48  matendo 8:16  matendo 19:5    1 wakorintho 1:12-13) basi fahamu kuwa wakati ulionao ndio sasa kwani Ufalme wa Mungu umekaribia sana (Marko 1:15).

Hivyo tafuta kanisa sahihi la kiroho lililopo karibu nawe na ukayasalimishe maisha yako kwa Mkuu wa uzima ili upokee kipawa chake cha Roho mtakatifu na kukupa uwezo wa kishinda dhambi na uwelewa wa maandiko.

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

Je! Ni kweli majuma sabini aliyoambiwa Daniel yamekwisha timia?(Daniel 9:23-27)


Maskini wa roho ni watu wa namna gani?(Mathayo 5:3)


“Mke wa ujana wako” anayezungumziwa katika biblia ni yupi?


NIFANYE NINI KAMA MKRISTO ILI MUNGU ANIONGEZEE IMANI KWAKE?


 Je! Ni lazima mgonjwa adongoke chini pale anapoombewa?

LEAVE A COMMENT