HESHIMA YANGU IKO WAPI? 

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, jina Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele. Karibu katika kujifunza maandiko matakatifu ya Mungu wetu aliye hai. 

Kwa kawaida katika jamii zetu, heshima ni kitu muhimu sana katika kuwaunganisha wanajamii, kukiwa na heshima kati ya wanajamii, hata uhusiano mzuri utaongezeka kati yao, hata katika familia pia, mume anapaswa kuwa na heshima kwa mkewe na mke Vivyo hivyo, watoto wanapaswa wawe na heshima kwa wazazi wao na kati yao wenyewe hata maandiko yanavyosema hivyo pia.

Wakolosai 3:18  Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.

 19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. 

20 Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana. 

21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa. 

Kama wana, wanavyotakiwa kuwa na heshima kwa baba zao, au kuwapa heshima baba zao, ndivyo ilivyo hata kwetu sisi wakristo, tunatakiwa kuwa na heshima kwa Baba yetu au kumpa heshima Baba yetu. Kama wewe umemwamini Bwana Yesu na kubatizwa katika ubatizo sahihi na KUJITENGA na uovu, basi, tambua wewe ni mwana wa Mungu, Mungu anakufahamu wewe kama binti yake, Mungu anakufahamu wewe kama mwanawe wa kiume kama maandiko yanavyosema katika 

2 Wakorinto 6:17  Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

 18 NITAKUWA BABA KWENU, NANYI MTAKUWA KWANGU  WANANGU WA  KIUME NA  WA KIKE, 

Soma tena

Yohana 1:12  Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika WATOTO WA MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; 

Ijapokuwa tunefanyika kuwa wana, lakini hatumpi heshima Baba yetu, wana wengi wa Mungu leo hii hawampi heshima Baba yao inayomstahiri, hivyo kupelekea Baba kuuliza HESHIMA YANGU IKO WAPI?

Malaki 1:6  Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, KAMA MIMI NI BABA YENU, HESHIMA YANGU IKO WAPI? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani? 

Kama unampa heshima baba yako kwa kumwamkia kila uamkapo asubuhi, heshima ya Kwa Mungu wako iko wapi unaposhindwa kumshukuru kila siku asubuhi anapokuamsha ukiwa na afya njema? 

Kama unaheshimu kazi yako kiasi kwamba, hata kama mvua ikinyesha kubwa kiasi gani hawezi chelewa kwenda kazini kwasababu inakupa kipato, heshima kwa Mungu wako iko wapi unaposhindwa kwenda kukusanyika na wenzako kwasababu mvua imenyesha? 

Kama unawahi kila siku kwenye majukumu yako, mikutano na biashara na zako, iko wapi heshima kwa Baba yako unapochelewa fika ibadani. Mungu anakuuliza mwana wa Mungu, heshima yake iko wapi?

Unakuta mwana wa Mungu hawezi chezea simu mbela ya uwepo wa bosi wake awapo kazini, lakini mwana wa Mungu huyo huyo utamkuta anachezea simu Kanisani, tena muda ambao mahubiri ynaendelea na mbele ya uwepo wa Baba yake aliye Mbinguni. Mwana wa Mungu, Baba anakuuliza heshima yake uki wapi?

Unakuta mwana wa Mungu anavaa vimini na suruali aendapo Kanisani lakini aendapo kwa wakwe zake anavaa nguo nzuri za kumsitiri mwiki wake. Ndugu yangu, heshima yako kwa Mungu wako iko wapi? Kweli Kwenye nyumbani mwa Mungu ndo sehemu ya kuonesha utupu wako na maungo yako? 

Kijana anavaa suruali kiunoni akiwapo ukweni au aendapo kufanya udahiri wa kazi, lakini afikapo kanisani anavaa mlegezo, mpendwa, heshima yako iko wapi kwa Mungu wako?

Mtoto wa Mungu, Baba yako anataka heshima yake katika mwili wako, Mungu anataka heshima yake uwapo nyumbani mwake, Mungu anataka heshima yake popote uendapo umwakilishe yeye, kwani wewe ni nuru kwa watu ambao wapo nje ya Kristo, ili kwa matendo yako  ya ndani na ya nje watu wavutewe kwa Mungu kupitia wewe.

Bwana akubariki. Shalom.

Mada zinginezo:

Sabato zilizowekwa na wanadamu ni zipi? 


Mariamu Magdalene alikuwa ni mtume? (Yohana 20:17) 


HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO.

LEAVE A COMMENT