Moja ya jambo muhimu sana kwa mkristo yoyote yule, ambalo Bwana Yesu alisisitiza ni kuwa WAOMBAJI, na faida ya kuwa waombaji Bwana Yesu aliitaja kuwa, tukiwa waombaji kamwe hatutoingia majaribuni.
Luka 22:40 Alipofika mahali pale aliwaambia, OMBENI kwamba msiingie majaribuni.
Faida nyingine ni kuwa, tunapata mahitaji yetu au vitu ambavyo tunavihitaji hapa duniani tukiomba sawa sawa na mapenzi yake.
Lakini maandiko yanaenda mbali na kutufunza zaidi kuwa, katika swala la kuomba tunapaswa kuomba bila kukoma, ikiwa na maana kwamba, kama mahitaji tunayotaka tutendewe na Mungu hatujapata, basi, tunatakiwa kuendelea kuomba tu, hatutakiwi kukata tamaa na kusema kuwa Mungu hataki kutupa au hajatusikia bali tunatakiwa kuendelea kuomba bila kukoma hadi tutakapopata majibu yetu.
1 Wathesalonike 5:17 OMBENI bila kukoma;
Na swala hili Bwana Yesu alilifahamu, na alipokuwa dunini aliweka wazi jambo hilo kuwa, tunatakiwa kuomba bila kukoma, tunatakiwa kumwomba Mungu daima hadi tupate majibu ya maombi yetu. Alijuwa kabisa kuwa, mwanadamu anaweza kata tamaa pale atakapoona kama hakuna jawabu lolote la maombi yake kutoka kwa Mungu, na ndipo akatufundisha mfano mmoja ambao tunausoma katika.
Luka 18:1 Akawaambia mfano, ya kwamba IMEWALASA KUMWOMBA MUNGU SIKUZOYE, wala wasikate tamaa.
2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.
3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.
4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,
5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.
6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?
Bwana alitoa mfano huo ili kutufundisha na sisi ni jinsi gani tunapaswa kumwomba, Bwana anataka tumwombe daima bila kuchoka, Bwana anataka tumkumbushe mahitaji yetu, asubuhi mkumbushe Bwana hitaji lako, mchana mkumbushe Bwana hitaji lako, na hata usiku pia zidi kumkumbusha Bwana na si siku moja tu bali kila siku, nenda mbele za Bwana ukimkumbusha hitaji lako daima, huko ndiko kuomba bila kukoma.
Na kitu cha kuzingatia ni kuwa, tunayepaswa kumwomba daima ni Bwana na si mtu yoyote, si mtakatifu Paulo, mariamu, Petro, Yosefu au Musa, ni Bwana pekee.
Lakini hakikisha upo katika hali ya usafi, hali ya utakatifu mbele za Mungu, hakikisha unatubu dhambi zako na kuomba rehema daima na kujitakasa, kwani maombi ya wenye dhambi ni machukizo mbele za Mungu bali maombi ya watakatifu ni haruni nzuri ya manukato mbele ya kiti cha enzi cha Mungu.
Ufunuo 5:8 Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu VILIVYOJAA MANUKATO, AMBAYO NI MAOMBI YA WATAKATIFU.
Hivyo zidi kumwomba Bwana Yesu sawa sawa na mapenzi yake daima bila kuchoka.
Bwana akubariki. Shalom.
MADA ZINGINEZO
Je! tunawezaje kufahamu kuwa mtu ana Roho Mtakatifu ndani yake?
Je! Ni dhambi kibiblia kuwaomba wafu (watakatifu)?
JE! NI LAZIMA TUNAPOSALI TUPIGE MAGOTI?
je kuomba hadi mtu awe kanisani au nyumbani?