Matayo 3:5 Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani;
6 NAYE AKAWABATIZA KATIKA MTO WA YORDANI, HUKU WAKIZIUNGAMA DHAMBI ZAO.
SWALI: Maandiko yanasema kuwa, watu kutoka Yerusalemu, na uhayudi wote, na nchi za kandokando ya Yordani walimwendea Yohana mbatizaji na Yohana mbatizaji ALIWABATIZA HUKU WAKIZIUNGAMA DHAMBI ZAO. Sasa Bwana Yesu na yeye alikuwa ni miongoni mwa watu ambao walibatizwa na Yohana mbatizaji, hivyo ni wazi kuwa na yeye aliziungama dhambi zake wakati anabatizwa kama ilivyokuwa kwa wengine. Swali ni je! Bwana Yesu na yeye alikuwa ni mwenye dhambi? Kwani ni wazi na yeye aliziungama zake? kwasababu na yeye alikuwa ni miongoni mwa waliobatizwa kama tunavyosoma maandiko katika.
Matayo 3:16 NAYE YESU ALIPOKWISHA KUBATIZWA mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake;
JIBU: Ni kweli kabisa kuwa, Bwana Yesu alibatizwa na Yohana mbatizaji mto Yordani, lakini maandiko yanasema kuwa, ndani ya Bwana Yesu hakukuwa na hila na wala dhambi haimo ndani yake ( 1 Yohana 3:5 ) na mpaka kuna wakati aliuliza swali kwa uwazi kwa watu kuwa, kama kuna mtu anamshuhudia kuwa yeye ana dhambi na aseme.
Yohana 8:46 NI NANI MIONGONI MWENU ANISHUHUDIAYE YA KUWA NINA DHAMBI? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?
Akiwa na maana kuwa, tokea angali ni mdogo anakua, mpaka anaenda kwa Yohana mbatizaji ili abatizwe, hadi alipofikia ni nani anayemshuhudia katika maisha yake kuwa alishawahi fanya dhambi au ana dhambi? Jibu ni hakukuwa na hata mmoja.
Sasa kama Bwana Yesu hakuwa na dhambi, kwanini alienda kubatizwa? Ubatizo ukikuwa na umuhimu gani kwake? Au ni nini alitaka kutufunza? Tukisoma mistari ya juu kidogo tutapata majibu ya kwanini Bwana Yesu alienda kubatizwa ili hali hakuwa na dhambi.
Matayo 3:13 Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe.
14 Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?
15 Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; KWA KUWA NDIVYO ITUPASAVYO KUITIMIZA HAKI YOYE. Basi akamkubali.
Alichotaka kutufunza ni kuwa, yeye ni kielelezo kwetu na njia yetu katika safari yetu kuelekea ufalme wa Mbinguni, alitaka kutufunza kuwa, ni lazima tukabatizwe ili tutimize haki yote, hata kama tukijiona ni watakatifu kiasi gani, hata kama tukijiona tuna shika amri zote kumi za Mungu bila kuacha hata moja, hata kama tukijiona ni wema kiasi gani ni lazima tukabatizwe na ubatizo sahihi ni wa MAJI MENGI NA KWA JINA LA YESU sawa sawa Na matendo 10:48, matendo 19:5 na 1 Wakorintho 1:13
Bwana akubariki. Shalom.
MADA ZINGINEZO
Biblia imeruhusu ubatizo wa vichanga (kulingana na matendo 16:33?)