KAMA YOSHUA ANGALIWAPA RAHA, ASINGALIINENA SIKU NYINGINE BAADAE. 

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Maneno hayo tunayoyasoma katika maandiko matakatifu yanamaanisha kuwa, katika wana wa Israel, hakuna hata mmoja aliyeingia rahani mwa Mungu, hakuna hata mmoja aliyeingia katika pumziko/sabato ya Mungu wakati ule wanatoka Misri na kwenda Kaanani,  kwasababu hata Yoshua na Karebu hawakuingia katika raha ya Mungu (Sabato) kwani, kama wangeingia katika raha ya Mungu basi Yoshua asingenena kwamba kuna raha nyingine baadae.

Waebrania 4:8  Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye. 

Sasa ukisoma toka juu maandiko yanaeleza kwanini hawakuingia, hawakuingia kwasababu lile neno la AHADI ya kuingia katika pumziko la Mungu halikuchanganyika na IMANI (kwa Yesu Kristo)

Sasa kitu hicho kilikua ni kivuli cha mambo yajayo lakini uhalisia wenyewe haukuwepo bado, uhalisia wenyewe ulitimilika baada ya kuja na kupaa kwa Kristo duniani. Sasa kipindi kile hakukuwa na mtu yeyote aliyeingia katika pumziko la Mungu (sabato) ijapokuwa Mungu alitaka watu waingie katika raha yake, basi Mungu ametoa nafasi nyingine tena kwa wanadamu wote duniani kuingia katika sabato yake ili wapate pumziko, ametoa fursa tena kwa watu wote wa ulimwengu huu kuingia katika raha yake.

Waebrania 4:6  Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, 

7 AWEKA TENA SIKU FULANI, akisema KATIKA DAUDI baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, 

Hapo anaposema “AWEKA TENA SIKU FULANI” ndio hiyo nafasi ya pili ya watu wote duniani kuingia katika pumziko lake, ila sasa, wakati huu ni KATIKA DAUDI pekee, sasa anaposema katika Daudi anamaanisha ni katika Yesu Kristo pekee, maana yeye ndiye SHINA na MZAO WA DAUDI kama alivyosema katika

Ufunuo 22:16  Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. MIMI NDIMI NILIYE SHINA NA MZAO WA DAUDI, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi. 

Kumaanisha kuwa, hakuna mtu atakayeweza Kuingia rahani mwa Mungu pasipo Bwana Yesu, hata watakatifu wote walio kufa tangu zamani hawakukamilishwa pasipo Yesu Kristo na ndio maana ile siku walifufuka baada ya Kristo kuwa wa Kwanza kufufuka.

Matayo 27:52  makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;

 53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, BAADA YA KUFUFUKA KWAKE, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. 

Hivyo basi, ili tutumie nafasi hii iliyotolewa na Mungu kuingia katika pumziko lake hatuna budi kupitia kwa Yesu Kristo maana yeye ndiye mlango wa kondoo.

Yohana 10:7  Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi MLANGO wa kondoo. 

Hakuna namna utaweza ingia rahani mwa Mungu bila Yesu Kristo, hakuna. Sasa unaingiaje rahani mwa Mungu? Rahani mwa Mungu unaingia kwa kudhamiria ndani ya moyo wako kuacha uzinzi na uasherati, pombe, vimini na suruali kwa wanawake, make-up, mawigi, kucha bandia, kutukana, kusema uongo, usengenyaji, nk kisha kumkiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni WA MAJI MENGI NA KWA JINA LA YESU sawa sawa na matendo 10:48

Hivyo ndugu yangu, kama bado upo nje ya wokovu, basi, fahamu kuwa wakati sahihi wa kuupokea ni sasa, wakati wa kufanya uamuzi wa kumpa Bwana Yesu maisha yako ni sasa, maana tunaishi wakati ambao yupo mlangoni kurudi kama alivyosema miaka mingi iliyopita.

Ufunuo 22:10 Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana WAKATI HUO UMEKARIBIA. 

11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. 

12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. 

Tafadhari, washirikishe na wengine habari hii njema.

Bwana akubariki, Shalom.


MADA ZINGINEZO:

Kwanini Nabii Eliya alitumwa sarepta kwa mjane katika mji wa sidoni?


Sabato zilizowekwa na wanadamu ni zipi? 

LEAVE A COMMENT