KANISA LA KWELI NI LIPI DUNIANI?

  Kanisa, Uncategorized

Shalom, Bwana Yesu apewe sifa. Kwanza kabisa, inabidi tufahamu kuwa, sehemu yoyote ile ambapo watu wanakusanyika kwa lengo la kumwabudu Mungu wa Mbinguni basi, hao watu tayari wanakua ni kanisa, haijalishi  wamekusanyika mahali gani, chini ya mti, kwenye nyumba ya mtu au kwenye jengo fulani. 

Sasa swali ni je! Kanisa la kweli ni lipi duniani?

Jibu: Kanisa siku zote kichwa chake na msingi wake mkuu ni Kristo Bwana, kwasababu yeye ndiye aliyejitoa nafsi yake kwaajili ya Kanisa kama tunavyosoma katika

Waefeso 5:25  Enyi waume, wapendeni wake zenu, KAMA KRISTO NAYE ALIVYOLIPENDA KANISA, AKAJITOA KWA AJILI  YAKE.

Na pia Kristo Bwana yeye ndiye kichwa cha kanisa kama tunavyothibitisha hilo katika 

Waefeso 5:23  Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, KAMA KRISTO NAYE NI KICHWA CHA KANISA; naye ni mwokozi wa mwili. 

Hivyo, kama Kristo ni kichwa, basi, watu wote tu viungo katika yeye.

Sasa ili kufahamu kanisa sahihi ni lipi, kwanza ni lazima tuwafahamu wale ambao watakaoenda siku ile kwa Bwana Yesu na kusema kuwa walimtumikia, kwani hawa ndio watakao tusaidia kufahamu kanisa sahihi ni lipi. Chukulia mfano wa maisha ya kawaida tu, kwamba mtu ameajiri wafanya kazi wa kujenga nyumba fulani kuanzia asubuhi hadi jioni, sasa itakapofika jioni wale walioajiriwa wataenda kwa yule aliyewaajiri ili wapate malipo yao. Vivyo hivyo sasa, kwa wote walio watumishi wa Mungu, kwa wote wanaohubiri habari za Kristo, hawa ndio watakao mfuata Bwana Yesu siku ile. Sasa kwa kuwafahamu watu hao, ndipo tutaweza kufahamu kanisa la kweli ni lipi. Sasa hebu tusome maandiko kidogo ili tuwatambue watu ambao watakaoenda mbele za Bwana na kujitambulisha kama wao ni watenda kazi wake

Matayo 7:22  Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana,hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? 

Unaona hapo kuwa, watu watakaoenda kwa Bwana watakua na sifa gani? Waliofanya unabii, uinjiristi, miujiza n.k sasa ukichunguza kwa makini utagundua kuwa hizo ni karama za Roho mtakatifu 

Waefeso 4:11  Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 

Na hawa wote kwa ujumla ndio wanaounda kanisa na ndio ambao siku ile wataweza kusimama mbele za Bwana na kusema kuwa walifanya kazi na wanastahili malipo, hivyo basi hadi hapo utakua umeshafahamu kuwa, sifa ya kwanza ya kanisa la kweli ni lazima liwe na karama za Roho mtakatifu, kanisa ambalo halina karama za Roho mtakatifu hilo si kanisa sahihi kabisa, wewe jiulize tu, siku ile hilo kani litakapoenda mbele za Bwana litasema lilifanya kitu gani? Ni wazi hakuna.  Hivyo makanisa yote ambayo hayana karama za Roho mtakatifu hayo si ya Mwana wa Adamu.

Lakini kama ukiendelea kusoma mstari wa 23 utaona kuwa Bwana aliendelea na kuwaambia hao watu wenye hizo karama kuwa

Matayo 7:23   Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. 

Bwana hakuwajibu kuwa “hapana hamkufanya unabii, uinjiristi n.k kwa jina langu” bali kinyume chake aliwaambia tu ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu. Sasa hii ni kuonesha nini? Ni kuonesha kuwa kuna kitu kingine zaidi ya karama za Roho mtakatifu, na kitu hiki si kingine zaidi ya kuyafanya mapenzi yake, sasa tunaweza sema tena kuwa, kanisa sahihi ni lile lenye karama za Roho mtakatifu na lenye kufanya mapenzi ya Bwana. Ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini ni wazinzi toka hapo, ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini waumini wanavaa nguo zisizo sitili miili yao toka hapo, ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini wanawake wanapaka wanja, make up, kucha bandia nywele bandia n.k toka hapo,   Ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini waumini wanavaa milegezo na kunyoa viduku toka hapo, ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini hawayashiki maagizo ya Bwana kama kushiriki meza ya na kutawadhana miguu toka hapo. Ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini wanawake hawafuniki vichwa wakati wa ibada toka hapa, ukiona kanisa linaongozwa na mchungaji mwanamke toka hapo. Ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini hauambiwi kuhusu utakatifu wa ndani na nje ambao pasipo huo huwezi mwona Mungu toka hapo, ukiona kanisa lina karama za Roho mtakatifu lakini kufanyiwa huduma fulani kama maombezi ni lazima utoe fedha, basi toka hapo kwa usalama wa nafsi yako. Hao watu tayari wapo chini ya laana kwani wanahubiri injili nyingine japokuwa wana hizo karama kama ilivyoandikwa katika 

Wagalatia 1:8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. 

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. 

Ndugu, haijarishi kanisa lako ni zuri kiasi gani au ni kubwa kiasi gani, au lina wafuasi wengi kiasi gani, au unalipenda kiasi gani, hilo kanisa lako si zaidi sana kuliko kuyafanya mapenzi ya Bwana Yesu. Hizi ni nyakati za mwisho tunazoishi na Bwana atakuja kuwanyakua watakatifu wake, hivyo jitahidi na wewe utafute kanisa sahihi ili atakapokuja akukute huko.

Bwana akubariki. Shalom 

7 thoughts on - KANISA LA KWELI NI LIPI DUNIANI?

LEAVE A COMMENT