chakula cha watoto kuwapa mbwa Kuna maana gani? (Mathayo 15:21-28)

  Maswali ya Biblia

Ili tuweze kuelewa vizuri Habari hii hatuna budi kusoma kuanzia juu kidogo. Tukisoma hiyo mistari ya hapo juu tutapata kuelewa vizuri.

Mathayo 15: 21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.

22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.

23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.

24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.

26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.

27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.

28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.

Tukirudi nyuma tuna ona Bwana Yesu alipokuja duniani, hakuja kwanza kwa watu wa mataifa, hapana kwasababu wao hawakujua kama kuna mwokozi yeyote, kadhalika watu wa mataifa walikuwa ni watu wasiokuwa na dini, wapagani, wasiomjua Mungu, walikuwa wanaabudu miungu,na ndio maana Bwana akawafananisha na mbwa katika mfano huo

Lakini hao wayahudi ni taifa la Mungu tangu zamani uzao wa Ibrahimu, pamoja na hayo kwa muda mrefu walikuwa wanalitazamia kuja kwa uwokovu wao ambao ungeletwa tu na MASIHI mwenyewe atakaye kuja kutoka mbinguni, Hivyo kwa kuwa wale ni uzao wa Mungu, uzao wa Ibrahimu, sasa ulipofika muda wa Mungu kuwatimizia haja yao waliyokuwa wanaisubiria kwa muda mrefu, ndio akamleta Bwana Yesu duniani aje kuwakomboa

Na ndio maana sasa tunamwona Bwana Yesu alipokuwa duniani, hakuhubiri na kufundisha katika nchi yoyote nnje na israel, kadhalika hakuwatuma hata wanafunzi wake katika mji au kijiji chochote cha mataifa, kwasababu hakutumwa kwao, bali kwa wale waliomtazamia yaani taifa la Israel (wayahudi).

Lakini sasa tunamwona huyu mwanamke ambaye ni mtu wa Tiro, (mwanamke aliyekuwa wa kimataifa), asiyekuwa na dini wala Imani katika Mungu wa kweli, alipomwona Bwana akipita kando kando ya miji yao, akamfuata ili ahudumiwe naye, lakini Bwana hakuonyesha kumjali kwa namna yoyote ile, lakini kwa vile alivyokuwa akimsumbua sumbua, ndipo Bwana akamwambia sikutumwa [kwa watu wa mataifa] ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli (yaani wayahudi)..lakini alipozidi kumsumbua sumbua, aliongezea na kumwambia “si vema kutwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”..yaani akiwa na maana kuwa si vizuri kuiondoa ile neema ya wokovu kwa wale waliostahili kuipokea(yaani wayahudi) na kuwapatia watu ambao hawakustahili kuipokea au kuitazamia(watu wa mataifa).

Lakini pamoja na hayo tunakuja kuona baadaye, ile neema ililetwa kwetu sisi mataifa, baada ya wale ambao waliostahili kuipokea kuikataa, hivyo sisi sasa sio mbwa tena bali tumefanywa kuwa wana wa Mungu kwa kupitia damu ya Yesu Kristo.

Hiyo ndio jambo la siri iliyokuwa imefichwa tangu zamani kwamba sisi watu wa mataifa tumehesabiwa kuwa warithi wa wokovu sawa na wayahudi kwa kupitia njia ya Yesu Kristo. Haleluya. Hivyo ndio maana Mtume Paulo akasema katika.

Waefeso 3: 4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.

5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

6 ya kwamba MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

Tunajifunza nini katika habari hii? Tumwendeapo Mungu, kwa haja ihusuyo wokovu wetu, hata kama ni kweli tutakuwa hatustahili mbele za Mungu, pengine mienendo yetu imekuwa mibaya sana, na tumeomba mara ya kwanza, na ya pili na ya tatu hatujajibiwa

Haifai kukataa tamaa, tuzidi kuomba tuzidi kuomba kama yule mwanamke Kwasababu Bwana Yesu alishatupa mfano unaofanana na huo, juu ya yule kadhi dhalimu, aliyekuwa hamchi Mungu, lakini yule mwanamke mjane alivyomwendea mara ya kwanza hakupewa haki yake, lakini kwa jinsi alivyokuwa akimwendea endea mara kwa mara, alimpatia haki yake.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT