1Wakorintho 15:29 “Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?
Ili kuelewa mtume Paulo alimaanisha nini katika habari hiyo, tuanzie mistari ya juu kidogo,
1Wakorintho 15:12 “Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu?
13 Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka;
14 tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure.
15 Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.
16 Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka”.
Kwa mujibu ya maneno haya ya Paulo ni kwamba, katika kanisa lililokuwa Korintho, kulikuwa na baadhi ya watu ambao waliyashika mafundisho ya masadukayo, yasiyoamini kiyama (ufufuo) ya wafu.
Lakini mtume Paulo akawa anawauliza, maswali hayo kama kuwapa changamoto, ikiwa hakuna kiyama ya wafu, kwanini Basi wanamuhubiri Kristo aliyefufuka kutoka katika wafu?, Hakuna maana yoyote kumuhubiri kwasababu hakuna aliyewahi kufufuliwa na kuishi tena, kwa mantiki hiyo.
Ni sawa na leo hii, mtu aseme, siamini kama kuna mbingu, Lakini wakati huo huo ahubiri watu kwenda mbinguni, unaona atakuwa kama anajichanganya.. Ndivyo ilivyokuwa kwa wakorintho hao wakati ule.
Sasa tukishuka mpaka ule mstari wa 29 ambao ni mwendelezo wa habari hiyo hiyo, Paulo anawauliza tena Wakorintho hao, swali hili;
1Wakorintho 15:29 “Au je! WENYE KUBATIZWA kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao”?
Kwamba, kulikuwa na kundi lingine la wakristo hao hao wa huko Korintho, ambao waliamini mfu anaweza kubatizwa, ikiwa mtu atasimama kwa niaba yake,
Hilo limethibitishwa katika maandishi ya zamani ya historia yanaonyesha baadhi ya wakorintho walikuwa na desturi hiyo, kwamba kama mtu amekufa bila kubatizwa, basi walikuwa wanamlaza kitandani, kisha wanamchukua mtu mwingine aliyehai na kumlaza chini ya kitanda chake, kisha kiongozi wa kidini, alikuja na kumuuliza Yule maiti, kama anahitaji kubatizwa, na ikiwa hatojibu chochote, basi Yule mtu aliyelala chini ya kitanda chake, atamjibu, Ndio,.
Kisha atatoka na kwenda kubatizwa kwa niaba yake(Yule maiti). Kisha Yule mtu aliyekufa atasemehewa na kuruhusiwa kuingia mbinguni.
Sasa mtume Paulo ndio anawauliza, wakorintho
“Au je! WENYE KUBATIZWA kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?…
Ikiwa na maana kwanini wafanye hivyo, kama hawaamini kuna ufufuo wa wafu..Hata kazi yao hiyo si itakuwa ni bure tu, kujilaza chini ya maiti. Hivyo aliwauliza ili kuwapa changamoto ya imani yao, Lakini hiyo haimaanishi mitume au kanisa la kwanza, walikuwa na desturi hiyo ya kubatiza kwa ajili ya wafu.
Desturi hiyo ni ya kipagani ambayo inakinzana na Neno la Mungu, mtu akifa ndio basi, anachongojea ni hukumu (Waebrania 9:27), Desturi hiyo inafanana na ile, ya kupelekwa toharani, ambayo inaaminiwa na kanisa Katoliki, kwamba mtu akifa anaweza kupelekwa sehemu ya mateso ya muda, lakini kulingana na maombi ya watakatifu anaweza kutolewa huko. Jambo ambalo ni potofu.
Hivyo ndugu, fahamu kuwa hakuna nafasi ya pili baada ya kifo. Ukifa umekufa, mwisho wako umefika.
Wakati tulio nao ndio sasa, saa ya wokovu ni leo.
Maran atha.