SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake”
JIBU: Ili tuelewe vizuri tusome, Habari yote, katika Mathayo 11:16-19
Mathayo 11:16 “Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Kimefanana na watoto wanaokaa sokoni, wanaowaita wenzao, wakisema,
17 Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.
18 Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo.
19 Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake”.
Hapo ni Bwana Yesu alikuwa anaonyesha jinsi gani, Hekima inavyopimwa kwa kazi zake ndani ya watumishi wake, na sio kwa mwonekano wake wa nje. Na ndio maana akaanza kwa kueleza Maisha ya Yohana mbatizaji na ya kwake, akasema, Yohana alikuja hali wala hanywi, anaishi majangwani, hajichanganyi na watu, muda wote ni Mungu tu, Yaani tukitafsiri kwa lugha ya sasa, ni mtumishi ambaye, muda wake wote ni kushinda milimani tu, akiomba na kutafakari, akishinda kanisani tu, kufanya ibada, hafanyi kazi yoyote, hana nguo nzuri, hana elimu yoyote, hachangamani na watu.
Kwa kutazama Ni rahisi kusema, Mungu gani huyo anayemtumikia, Mungu hawafanyi watu kuwa hivyo, kushinda tu na njaa muda wote, huyu lazima atakuwa amefungwa akili, kama sio ameathirikia kisaikolojia.
ndivyo walivyomuona Yohana mbatizaji wakasema ana pepo, mtu wa Mungu hawezi kuishi majangwani tu, watu wenye pepo ndio wapo hivyo.
Lakini Bwana Yesu anasema hicho sio kipimo sahihi.
Halikadhalika, mtumishi mwingine anaweza kuwa ni wa kujichanganya sana wa watu, kama vile Bwana Yesu, alivyokuwa anakula na kunywa na watu matajiri na wenye dhambi, marafiki zake wengi ni viongozi au watu wakubwa, anatembelea gari zuri, anakaa kwenye makasri sikuzote.. Hapo pia ni rahisi watu wasiomjua Mungu kusema, huyu ni nabii wa uongo, tapeli, anakula sadaka za maskini. Kisa tu yupo kwa mwonekano huo.
Lakini kipimo hicho cha kimwonekano, sio kizuri kwasababu hakitoi majibu sahihi.
Lakini Bwana Yesu akasema, mwishoni, “hekima imejulikana kuwa na haki kwa kazi yake”.. yaani, haijalishi ni njia ipi mtu ataitumia, ni hekima ipi mtu atakayoichagua kuishi au kukaa kwayo, kinachojalisha ni matokeo ya kazi yake.. ndio itaeleza kuwa hekima hiyo ni sahihi au sio sahihi.
Kwamfano Yohana aliishi majangwani, lakini huduma yake ilikuwa na mafanikio makubwa sana, alifanikiwa kuwavuta watu kwa Kristo, na kuwabatiza watu wengi sana, hivyo hekima yake aliyoichagua ni sahihi kwasababu imeleta matunda.
Halikadhalika, Bwana Yesu naye, alikuwa anaketi na wenye dhambi, alikuwa anakula na kunywa, lakini matunda aliyoyaleta kwa Yehova hayahesabiki.
Hata sasa, tusiwapime watumishi kwa njia walizozichagua, bali tuwapime kwa kazi zake, ikiwa mtu anaishi milimani, lakini hakuna chochote anachokivuna kwa Kristo, hekima hiyo ni ya uongo, vilevile ikiwa anakaa katika Maisha ya kifahari lakini kazi yake ni kuwatabiria watu, hakuna wokovu wowote huyo pia kazi yake ni uongo. Lakini kinyume chake ni kweli.
Kama kuishi kwake milimani kunaujenga ufalme wa mbinguni watu. Wanaokolewa hekima hiyo ni sahihi..Vilevile kama kuishi kwake kifahari hakuathiri utumishi wake zaidi sana matunda ya kweli ndio yanazidi kuonekana pia hapaswi kulaumiwa.
Ukisoma Luka 7:35 inasema vizuri Zaidi… Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.
Watoto wa hekima huwa wanaonyesha kazi zao nzuri kwa hekima waliyochagua.
Bwana atupe jicho la kuliona hilo.