NANYI KWA SUBIRA YENU MTAZIPONYA NAFSI ZENU

Biblia kwa kina, Uncategorized No Comments

Shalom, karibu tuyatafakari maneno ya Bwana wetu na Mungu wetu Yesu Kristo, yeye ambaye ametuita katika neema yake hii ya wokovu kama alivyosema katika 

Yohana 15:16  Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. 

Na ndio maana Bwana alisema katika injili ya Yohana 6:44 kuwa hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipovutwa na Baba yangu aliyenipeleka nami nitamfufua siku ya mwisho. Hivyo basi ni dhahiri kuwa wokovu huu tulionao ni wa thamani sana kwani katika wokovu huu tuna ahadi ya uzima wa milele, ahadi ambayo itatuepusha na ile hukumu ya Mungu iliyowekwa tayari juu ya uovu wa wanadamu wapingao kweli ya Mungu 

Warumi 1:18   Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. 

Ni kweli Bwana ametupa ahadi hii ya uzima wa milele na ahadi zake Mungu wetu huwa ni kweli kama ilivyoandikwa katika 

2 Wakorinto 1:20  Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. 

Lakini urithi wa ahadi hii hauji hivi hivi tu bali Bwana alishaweka wazi kabisa tangu kipindi kile alipokuwepo hapa duniani kuwa, ni kweli tuna ahadi ya uzima wa milele, ahadi itakayotuokoa nafsi zetu na moto wa milele. Lakini hii ahadi tutaipata kwa SUBIRA na uvumilivu mwingi sana. Hebu tusome 

Luka 21:19   Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu. 

Umeona hapo? Bwana alisema “kwa subira tutaziponya nafsi zetu” hii ni kumaanisha kuwa si kitu rahisi rahisi tu kuipata ile ahadi ya kuingia Mbinguni, sasa ni kwanini? Ni kwasababu shetani hapendi wewe uingie huko kwani anaufahamu uzuri uliopo huko hivyo atainua kila kikwazo ilimradi tu wewe uanguke na ushindwe kuendelea mbele. Kama utakumbuka, hata wana wa Israel walipewa ahadi ya kuingia katika nchi ya ahadi na Bwana lakini utagundua kuwa wengi walishindwa kutokana na kukosa SUBIRA na hivyo kumwudhi Mungu. Na sisi pia Bwana anatuambia kuwa kwa subira zetu tutaziponya nafsi zetu, hii ni kumaanisha kuwa, tutakutana na dhiki nyingi sana hapa duniani kama alivyosema katika

Yohana 16:33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.

Kama Bwana alisema kuwa kwa subira yetu tutaokoa nafsi zetu, basi ni wazi pia hata na yeye aliushinda ulimwengu (mateso) kwa uvumilivu na subira. Tutakutana na mateso mengi mno, pengine hata kupoteza kazi kwaajili ya Bwana, pengine hata kufungwa gerezani, pengine hata kupigwa na kudhihakiwa kwaajili ya Bwana, lakini hatupaswi kukata tamaa kwani kwa SUBIRA yetu ndo tutaweza kuponya nafsi zetu. 

Mpendwa katika Bwana, ahadi ya Bwana ni ya kweli lakini pasipo SUBIRA na uvumilivu hatuwezi ipokea, hata maandiko yanatuambia hilo katika

Waebrania 6:12  ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu. 

Umeona hapo? Inasema tukawe wafuasi wazirithio ahadi kwa imani na uvimilivu. Lakini maandiko yanatueleza pia kuhusu Ibrahimu aliyepokea ahadi kutoka kwa Mungu kuwa ni kwa jinsi gani alipokea ile ahadi, biblia inatuambia kuwa kwa uvumilivu akaipata ile ahadi 

Waebrania 6:15  Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. 

Ndugu yangu hadi hapo utagundua kuwa kanuni za Mungu ni zile zile, Ibrahimu alipata ahadi kwa kuvumilia na kitu hicho hicho pia anakirudia kwetu sisi kuwa, kwa SUBIRA tutaipata ile ahadi, kama Ibrahimu  baba wa imani alipata ahadi yake kwa kuvumilia je! wewe ni nani ndugu yangu usiwe na SUBIRA? hayo majaribu unayopitia hapo kazini usife moyo mtazame Bwana, hiyo hali ngumu ya maisha unayopitia baada ya kuacha kuuza mwili wako usikate tamaa jipe moyo mtazame Bwana, hiyo hali ya kutengwa unayopitia kwasababu umeacha makundi ya marafiki zako walevi jipe moyo mtazame Bwana, fahamu kuwa kwa subira yako utajiokoa nafsi yako. Hiyo hali ngumu unayopitia ya kukosa mahitaji yako usife moyo ndugu yangu, mkumbuke Lazaro ambaye alitamani kushiba kwa makombo ya yule tajiri pale mezani hivyo mtazame Bwana kwa subira ukajiokoe nafsi yako.

Mpendwa, Bwana anayajua hayo, lakini wewe utazamie uzuri wa ufalme ule utakaopatikana katika ahadi yake, kwani Bwana alisema hivi

Yohana 14:2  Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. 

Hivyo fahamu kuwa subira yako ndiyo itakayokufanya wewe uwe mrithi wa makao yale ya milele na milele kwani kwa kufanya hivyo utakua unautafuta mji ule udumuo kwasababu hapa duniani hatuna mji udumuo, huo mji wa Dar es salaam si wako, huo mji wa Mtwara si wako, bali wewe utafute ule udumuo kwa subira ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu 

Waebrania 13:14   Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. 

Bwana akubariki. Shalom 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *