Omri ni nani kwenye maandiko na sheria zake ni zipi? (Mika 6:16)

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: Omri ni nani kwenye maandiko? Sheria zake zishikwazo na matendo ya nyumba ya Ahabu ni yapi kama tunavyosoma katika maandiko? (Mika 6:16)

Mika 6:16  Kwa maana amri za Omri ndizo zishikwazo, na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, nanyi mnakwenda katika mashauri yao; ili nikufanye kuwa ukiwa, na wenyeji waliomo humo kuwa zomeo; nanyi mtayachukua matukano waliyotukanwa watu wangu. 

JIBU: Shalom, jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele. Omri alikuwa ni miongoni mwa wafalme wa Israel na ndiye baba yake mfalme Ahabu, Omri alitawala miaka kumi na miwili katika Israel, alikuwa ni jemedari ya jeshi la Israel ambaye alitawala baada ya mfalme kuuwawa kwa fitina. Unaweza soma habari yake katika 1 wafalme 16:16-30

Katika utawala wake, alifanya machukizo makubwa sana mbele za Bwana kuliko wafamle wote waliomtangulia

1 Wafalme 16:25  Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia;

 26  kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili. 

Na baada ya kufariki kwake, mwanae Ahabu ndiye aliyetawala kama mfalme katika Israel, lakini na yeye alikuwa muovu mbele za Bwana kwani alioa mwanamke wa mataifa aitwaye Yezebeli

1 Wafalme 16:28  Omri akalala na babaze, akazikwa huko Samaria; na Ahabu mwanawe akatawala mahali pake. 

Sasa wakati ambao Bwana anakaribia kuwapeleka utumwani wana wa Israel (wale wa upande wa Samaria) aliwaonya sana kabla, lakini hawakutaka kugeuka na ndipo Bwana akawaambia kuwa watakua ukiwa.

Mika 6:12  Kwa maana matajiri wake wamejaa jeuri, na wenyeji wake wamesema uongo, na ulimi wao una udanganyifu kichwani mwao.

 13  Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nami nimekupiga kwa pigo liumizalo sana; nimekufanya kuwa ukiwa, kwa sababu ya dhambi zako. 

Sasa moja ya vitu ambavyo viliwafanya wamchukize Bwana ni matendo yao maovu, kwani hadi wakati huo bado wana wa Israel walikua wakifanya mambo yale yale ya utaratibu (sheria) za Omri ambazo zilikuwa ni machukizo kwa Bwana, bado walikua wanashika matendo yote ambayo Ahabu aliyafanya katika utawala wake ambayo yalikuwa ni machukizo makubwa mno kwa Mungu ambayo ni kuabudu mabaali ambayo yaliletwa na Yezebeli.

Sasa ni nini tunachojifunza kwa watu hawa? Ni kuwa, Mungu ni wa upendo sana, kila muda anatulilia tuache dhambi na tumgeukie yeye, lakini sisi hatutaki kusikia, tunafanya shingo zetu kuwa ngumu, tunawaiga watu waovu wa kale wa Sodoma na Gomora, tunawaiga watu wazinzi na waasherati wa kale, tunawaiga waabudu sanamu wa kale, tunawaiga wapaka wanja wa kale wakina Yezebeli, tunawaiga watu waliowadhihaki manabii na watumishi wa Mungu wa kale, tuendelea na uganga tuliorisishwa na bibi zetu wa kale, tunaendelea na matambiko ya mizimu tuliyoachiwa na mama zetu zamani, tunaendelea na uchawi tulioachiwa na mababu zetu wa zamani na kibaya zaidi  ni kuwa, tunawazidi hata wao, lakini Mungu bado anataka tuyaache hayo leo na tumgeukie yeye, kwani tusipofanya hivyo atatuacha ukiwa kama na hao alivyowaacha.

Mithali 1:24  Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu; 

25 Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu; 

26 Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo; 

27 Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.

28 Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione. 29 Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana. 

Hivyo ndugu yangu, amua leo ndani yako kuacha hizo sheria za mababu zako ambazo ni machukizo kwa Bwana kisha tubu na kumpa Bwana maisha yako ili upate msamaha wa dhambi.

Bwana akubariki . Shalom

One Reply to “Omri ni nani kwenye maandiko na sheria zake ni zipi? (Mika 6:16)”

  • Kwa maoni yangu matumizi ya mimea asili kama dawa sio,dhambi tangu mwanzo (m wa.1;29-30) Mungu aliagiza matumizi ya mimea itoayo mbegu na matunda miche itoayo majani kuwa chakula na kazi ya chakula mwilini ni Afya(Tiba lishe)

LEAVE A COMMENT