USIJENGE WALA KUIMALISHA  UHUSIANO WAKO NA SHETANI.

  Biblia kwa kina

Shalom mwana wa Mungu nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu kristo karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Tofauti na watu wengi tunavyomfikiria shetani kwamba huenda huwa anakurupuka tu anapotaka kumuangusha mwamini katika dhambi na kumrudisha nyumba huwa tunadhani kuwa ni kitendo cha ghafula tu hafanyi maandalizi yoyote anakurupuka tu na kufanya anachotaka lakini ndugu si hivyo.

Leo tutakwenda kutazama  kwa kina ni kwa namna gani shetani anafanya kazi zake tena katika ustadi na umakini mkubwa sana. Tusome kisa kimoja hapa halafu tukitafakri na katika hiki tutajifunza jambo kubwa sana litakalotusaidia katika maisha yetu ya wokovu.

Mwanzo 3:1-3”
[1] Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 

[2]Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;

  [3] lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.

Wengi wetu tunaposoma mstari huu huwa tunaona nyoka alitokea tu akasema hivyo na hawa akaanza kutoa siri mwisho akala matunda la! Sivyo hivyo.

lakini jambo la kwanza aliloanza nalo hapa shetani ilikuwa kuanza kutengeneza urafiki na Hawa taratibu halikuwa jambo la siku moja au wiki au mwezi mmoja bali kilikuwa ni kipind kirefu. Hakuishia tu kutengeneza tu urafiki lakini katika urafiki huo ukawa ni uhusiano(yaani urafiki ule wa karibu sana) na akazidi kuuimarisha siku baada ya siku ili azidi kuaminika na Hawa. Ni mazungumzo mengi yaliyokuwa yakifanyika pale siku baada ya siku. Na baada ya kuona uhusiano au urafiki wao umekuwa ule wa ndani sana ndio akaanza sasa kuingiza mazungumzo yake ya msingi ili kuweza kufanikisha jambo lake.

Na hapo huenda alianza kumwambia habari ama kumuuliza Hawa“je! Unaonaje ungekuwa na uwezo kama Mungu(yaani unapenda kuwa kama yeye) anaekuja kuwatembelea kila siku wewe na Mume wako? Ambae ameviumba vitu vyote hata mimi unaeniona hapa vipi kama ukiwa na uwezo kama huo?”

Na katika mazungumzo kama hayo Hawa huenda alisema “ natamani ndio kuwa kama yeye ila sasa haiwezekani wala hakuna njia yoyote naweza kuwa kama yeye”

Si kwamba shetani alikurupuka kusema hapo hapo fanya jambo Fulani utakuwa kama yeye la! Alikaa tena kwa kitambo kidogo na baaadae ndio anakuja kuuliza swali ambalo alikuwa analijua kabisa. (maana wangelikuwa wanakula nini sasa kama hawaruhusiwi kula kila kitu?)

Taarifa anazozitoa hawa juu ya jambo aliloulizwa hazikuwa za kawaida kabisa lakini zilikuwa ni taarifa za ndani ama siri ambayo yeye na Mume wake ndio waliokuwa wanajua sasa turudi hapo juu kidogo..

Mwanzo 3:2-3 [2 ]Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 

[3] lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa”

Unaona hapo! Hawa asingeweza kusema haya mambo kwa kitu alichokutana nacho siku moja tu. Ni sawa na wewe leo mtu unakutana nae mara ya kwanza unaanza kumwambia siri za ndani za familia yako ni jambo lisilowezekana. Mtu unaeweza kumwambia ni mtu wa karibu na unaemfahamu vyema na kumuamini pia huwezi ukamwambia hata kila rafiki maana katikati ya marafiki zako wapo usiowaamini.

Sasa kwa sababu shetani alikuwa ameshaimarisha urafiki wake vizuri na Hawa na kuna mambo ambayo alikuwa ameshamuuliza ukisoma hupo juu utaona kuwa “vipi angelikuwa na uwezo wa kuwa kama Mungu…..”  ikawa ni njia rahisi sasa ya kutimiza kile alichokuwa amekikusudia. Na ndio maana akapata ujasiri wa kusema hivi…..

Mwanzo 3:4-6” Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 

5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.

6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.”

Unaona hapo anasema “…….., nanyi mtakuwa kama Mungu…..”  Hawa asingeweza kufanya maamuzi kama haya kama asingelikuwa amwemuamini kwanza nyoka. Hivyo aliamini kile alichoambiwa kuwa ni hakika kabisa . kama unavyopewa taarifa na rafiki yako unaemuamini wakati mwingine unaweza hata usitafute kuhakiki maana unamuamini kwa kipindi kirefu.

SASA JE TUNAIMARISHAJE UHUSIANO/URAFIKI NA SHETANI PASIPO HATA KUJUA?.

KUPITIA FIKRA ZETU.
Shetani anauzoefu na mwanadamu anamjua vyema maana  kakaa na kuwasoma watu kwa zaidi ya miaka 6000(wewe pengine hata miaka 90 huna). Hivyo ni mwana saikologia mzuri sana muonekano wako na ulivyokaa anaweza akafahamu ni kipi kwa muda huo unachokiwaza(hawezi kuingia kwenye fahamu zako na kujua kila kitu la!) ila anaweza hisi unawaza nini na ikawa sahihi. Na katika hilo akaanza kukuletea mawazo yake juu ya hicho.

Kama ulikuwa unawaza kula rushwa ataanza kukwambia mshahara ni kidogo kazini mnatumikishwa sana una majukumu mengi. Mshahara hautatosha wewe chukua tu hiyo rushwa au ibia serikali,boss wako ama kampuni yako hawatajua tena fanya mara moja tu nk. Mawazo haya hayataishia siku moja yataendelea kukutafuna ndio hapo anapoanza kutengeneza na kuimarisha urafiki ili mwisho wa siku umuamini kama Hawa.

Na utakuwa unaanza kuona mambo yanazidi kuwa magumu na atazidi sana kukwambia na wewe pasipo kufikiri “mshahara huwa hautoshi siku zote”. Vivyo hivyo katika uzinzi,nk.

TUNAWEZAJE KUMPIGA/KUKATAA.
Unapoona wazo linafuliza sana akilini mwako na linapingana na mapenzi ya Mungu  likatae mara moja  pinga kabisa wala usikubaliane nalo kama maandiko yanavysema.

Yakobo 4:7” Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia”

Na hutaweza kumpinga kama si mtu wa kusoma Neno,kuomba,kufunga hutaweza ndugu haijalishi unaenda kanisani kila siku. Kama hufanyi haya atakuangusha tu katika jambo lolote. Kuwa muombaji unavyozidi kumkaribia Mungu ndivyo unavyozidi kumuweka mbali Shetani.
Ubarikiwe sana.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT