SWALI: Naomba kuuliza, je! Maandiko matakatifu yanajichanganya katika Wakolosai 3:1 na Matendo 7:56? Kwa sababu tunaona Paulo anasema Kristo AMEKETI MKONO WA KUUME WA MUNGU, lakini Luka anasema Stefano alimwona Kristo AMESIMAMA MKONO WA KUUME WA MUNGU. Sasa hapo tumwelewe nani na kumwacha nani? Kwa sababu Huyu anasema Kristo AMEKAA na huyu Anasema Kristo AMESIMAMA.
Wakolosai 3:1 Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, AMEKETI MKONO WA KUUME WA MUNGU.
Na Luka naye anasema
Matendo 7:56 Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu AMESIMAMA MKONO WA KUUME WA MUNGU.
JIBU: Kwanza kabisa kabla ya kujibu swali hili inapaswa tufahamu kitu kimoja, watu wengi hatupendi kujifunza biblia kwa kumpa nafasi Roho Mtakatifu ambaye ni mwalimu Bora kabisa, hivyo kupelekea watu kutafsiri maandiko katika hekima zetu binafsi na elimu zetu binafsi na kutengezena picha fulani fulani kwamba Roho Mtakatifu ni njiwa, au mbinguni kuna viti vitatu vya enzi cha Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu n.k, kitu ambacho sio sahihi hata kidogo, ni lazima Roho Mwenyewe atufundishe vinginevyo tutaishi kusoma biblia na kuona maandiko yanajichanganya tu, tutaishia kuona mitume wanampinga Bwana wao, au Ezekieli anapingana na Yakobo, au Paulo anapinga na nabii Samweli kitu ambacho si sawa.
Kwa Mfano; tuchukue andiko la mtume Petro linalosema Yesu Kristo yupo mkono wa Kuume wa Mungu…
1 Petro 3:22 NAYE YUPO MKONO WA KUUME WA MUNGU, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.
Lakini nabii Daudi naye kwa uweza wa Roho anasema kuwa Mungu Yupo mkono wa kuume wa Yesu Kristo.
Zaburi 110:4 Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.
5 BWANA YU MKONO WAKO WA KUUME; Ataseta wafalme, Siku ya ghadhabu yake.
Sasa kwa maandiko hayo aliye mkono wa Kuume wa Mwenzake ni nani? Daudi anasema Mungu yupo mkono wa Kuume wa Yesu Kristo, lakini Petro anasema Yesu Kristo yupo mkono wa kuume wa Mungu, umeona hapo? Kama ukitaka kutumia hekima zako za kibinadamu utaishia kuona Daudi anapingana na mtume Petro.
TURUDI KWENYE SWALI LETU
Biblia haijajichanganya kwenye wakolosai 3:1 na matendo Matendo 7:56, ila akili zetu na mawazo yetu ya kibinadamu ndio yanayojichanganya kwani Roho aliyekuwepo ndani Stefano au Luka ndiye aliyekuwepo pia ndani ya Paulo. Tunachopaswa kuelewa hapo ni kuwa, biblia inamaanisha nini inaposema Mkono wa kuume? Kwa sababu sehemu ambayo Kristo alipo mtume Yohana alishatueleza, kwamba, Yesu Kristo hajasimama wala hajakaa pembeni upande wa kulia wa kiti cha enzi, na wala hayupo kulia wala kushoto kama watu wengi wanavyodhani leo hii, bali mtume Yohana alisema…
Ufunuo 4:2 Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, KITI CHA ENZI KIMEWEKWA MBINGUNI na MMOJA AMEKETI JUU YA YA KILE KITI;
Hapo tunaona mtume Yohana hakuona kiti kingine cha pili cha enzi ambacho taasisi ya uongo ya Mashahidi wa Yehova inasema Yesu Kristo Mungu mdogo amekaa, na wala hakuona sehemu yoyote ile pembeni ya hicho kiti ambayo Yesu Kristo kasimama, bali aliona kiti kiomoja tu cha enzi na Mmoja ameketi pale, Mungu Mkuu, Yesu Kristo, ambaye kila Mwanadamu atadhihirishwa mbele zake
2 Wakorinto 5:10 Kwa maana IMETUPASA SISI SOTE KUDHIHIRISHWA MBELE YA KITI CHA HUKUMU CHA KRISTO, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.
Na tena mtume Yohana anaendelea na kusema..
Ufunuo 5:6 Nikaona KATIKATI YA KILE KITI CHA ENZI na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, MWANA-KONDOO AMESIMAMA, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.
Kufunua kuwa, Mungu huyo huyo Yesu Kristo, aliyeketi katika kiti chake cha enzi, pia ni ndiye Mwokozi
Tito 2:13 tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya UTUKUFU WA KRISTO YESU, MUNGU MKUU NA MWOKOZI WETU;
Na ndio maana Paulo pia alisema…
Matendo 20:28 Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha KANISA LAKE MUNGU, ALILOLINUNUA KWA DAMU YAKE MWENYEWE.
Hivyo basi, Paulo na Luka hawakupingana kwa sababu Kristo hajakaa wala hajasimama, na mkono wa Kuume katika biblia haumaanishi kitu kingine kilichopo upande wa mkono wa kulia kama unavyokaa na jirani yako hapo kanisani, Kazini au sehemu yoyote ile, mkono wa Kuume wa Mungu unawakilisha NGUVU NYINGI MNO, UWEZA (kutoka 15:6), AU UTUKUFU MWINGI MNO WA MUNGU MWENYEWE, ambao atakuja nao siku ile na dunia yote kutetemeka mbele zake
Matayo 26:64 Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi MKONO WA KUUME WA NGUVU, AKIJA JUU YA MAWINGU YA MBINGUNI.
Hitimisho: Tukimwamini Yesu Kristo Kama Mwana wa Mungu, au Mwana wa Adamu, au Mwana Kondoo aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu na kubatizwa katika Ubatizo sahihi haina shida tutaokoka, lakini hiyo ni hatua changa katika Ukristo, ni kama mtoto anayetumia maziwa au uji, itafika wakati tunapaswa tuwe watu wazima kiroho na kutambua vyakula vingine, hivyo, tusikubali kukaa katika hali hiyo hiyo ya kunywa maziwa na uji tu kiroho kama watoto wachanga (Waebrania 5:13), bali tukue kila siku katika vyakula vingine vya kiroho kwa kumjua sana Yesu Kristo Kama biblia inavyosema.
Waefeso 4:13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.
Bwana akubariki, Shalom.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
Makuhani wa Mungu ni watu gani katika biblia?
UMEMWAMINI YESU KRISTO KWA NAMNA GANI?
Bado Bwana Yesu anasema nawe kwa mifano?