FAHAMU NINI MAANA YA MUNGU NI ROHO (Yohana 4:24)

  Biblia kwa kina, Mungu, Uncategorized

Jina la Bwana litukuzwe, karibu tuongeza maarifa na kujifunza neno la Mungu Wetu Yesu Kristo, kama maandiko yanavyosema katika

Wakolosai 3:16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. 

Leo kwa kibari cha Mungu tutatazama andiko linalosema Mungu ni Roho, na ninaamini kwa neema zake nyingi utapata kujifunza kitu kipya

Tusome…

Yohana 4:24 MUNGU NI ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. 

Kwanza kabisa jiulize, kama MUNGU NI ROHO basi NI ROHO WA NAMNA GANI? Kwa sababu hata malaika nao ni roho, hata ibilisi na mapepo nao ni roho. Ukishajiuliza swali hili ndipo utakapokuja kugundua kuwa, kumbe vipo viumbe vingine tofauti na Mungu ambavyo ASILI YAKE PIA NI ROHO, hivyo basi, ni wazi kuwa, MUNGU AMBAYE NI ROHO atakuwa anayo sifa nyingine ya kipekee inayomtofautisha Yeye na hizo roho zingine zote kwa sababu Mungu Yeye hawezi linganishwa na kitu kingine chochote kile, si malaika na wala si mwanadamu.

Isaya 40:18 BASI, MTAMLINGANISHA MUNGU NA NANI? AU MTAMFANANISHA NA MFANO WA NAMNA GANI?

Umeona hapo?…Sasa sifa inayomtofautisha MUNGU NA ROHO zingine ni ipi? Hapo ndipo tutakapomtambua Mungu ni Roho lakini ni Roho wa namna gani. 

Sifa hiyo si nyingine zaidi ya UTAKATIFU

Walawi 20:26 Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa MIMI BWANA NI MTAKATIFU nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu. 

Ambapo anataka kila kiumbe chake kiwe kitakatifu kama Yeye alivyo mtakatifu, na ndio maana hata malaika zake aliwaumba katika asili hiyo ya utakatifu, na pia anataka kila mwanadamu chini ya jua awe hivyo, na endapo kiumbe chochote kile kisipokuwa na sifa hiyo kitatupwa katika ziwa la moto milele na milele baada ya siku ya hukumu, wanadamu na malaika (Mathayo 25:41)

Hivyo basi, Mungu ni Roho ndio, lakini ni ROHO TAKATIFU, na wote wanaomwabudu halisi ni lazima wamwabudu katika ROHO WAKE NA KWELI, vinginevyo ni kinyume chake (wasio mwaabudu halisi).

Lakini sifa hiyo ya yeye kuwa ni Roho, haimzuii Mungu kufanya anachotaka katika ulimwengu aliouumba Yeye Mwenyewe, hapana! Kwani Yeye hana mipaka, anaweza fanya chochote kile, anaweza jidhihirisha katika mwili (ijapokuwa Yeye ni Roho), na AKALA CHAKULA NA KUNYWA KAMA MWANADAMU, ni kama vile tu alivyofanya alipomtembelea rafiki yake Ibrahimu katika hema yake.

Mwanzo 18:1 BWANA AKAMTOKEA IBRAHIMU KARIBU NA MIALONI YA MAMRE, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.

 2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, 

3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.

4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.

 5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.

 6 Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate.

 7 Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa.

 8 Akatwaa SIAGI NA MAZIWA, NA NDAMA aliyoiandaa, AKAWAANDIKIA MBELE YAO, akasimama karibu nao chini ya mti, NAO WAKALA

Umeona hapo?..Mungu ambaye ni Roho (Bwana) alijidhihirisha katika mwili na kula na kunywa kama Mwanadamu? Lakini si hivyo tu, pia Mungu Huyu Huyu aliye Roho anaweza amua kuonekana na mtu yoyote yule katika roho kama anavyotaka yeye, ni kama vile tu alivyoonekana na Danieli au Ezekieli katika roho, au kama vile alivyoonekana na mtume Yohana au nabii mikaya katika kiti chake cha enzi, au kama vile anavyoonekana katika roho na manabii wote wakike na wakiume duniani leo hii (lakini Kama apendavyo Yeye), kwa sababu biblia inasema hakuna mtu aliyemwona Mungu ISIPOKUWA YULE ALIYEJALIWA. 

Hivyo basi, Mungu ni Roho lakini ni ROHO TAKATIFU, na wala hana mipaka katika utendaji kazi wake, yeye ni Baba peke Yake, Mmoja na wa milele (Malaki 2:10, Isaya 9:6), Yeye ni Bwana (Isaya 42:8) Yeye ni Roho (2 Wakorintho 3:17), Yeye ni Yehova (Kutoka 6:2) na pia Yeye ni Mwokozi (Isaya 43:11), Yesu Kristo, Mungu aliyejuu ya mambo yote.

Warumi 9:4 ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; 

5 ambao mababu ni wao, na katika hao ALITOKA KRISTO kwa jinsi ya mwili. NDIYE ALIYE JUU YA MAMBO YOTE, MUNGU, MWENYE KUHUMIDIWA MILELE. AMINA.

Je! Unapenda kumwelewa Mungu (Bwana), katika ukuu wake na siri zake wakati ukiwapo hapa duniani?.. basi Mche Yeye kwa maana maandiko yanasema

Zaburi 25:14 SIRI YA BWANA IKO KWAO WAMCHAO, Naye atawajulisha agano lake. 

Je! Unatamani kumwona Bwana kama alivyo katika furaha tele na shangwe kwenye mbingu mpya na nchi mpya?..Basi ishi maisha ya utakatifu

Waebrania 12:14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; 

Na unafanya hivyo kwa kumwamini Kristo na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, na kisha dumu katika fundisho la mitume na manabii watakatifu wa Bwana na sio dhehebu lako wala taasisi ya dini yako.

Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.

Bwana akubariki, Shalom.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

Kwanini Bwana Yesu alijeruhiwa ubavuni pale msalabani?


Nini maana ya mstari huu “unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya wanadamu” (2 Petro 2:21) 


Je! Ni kweli mtume Paulo alipingana na maandiko ya nabii Yoeli? (Yoeli 2:28)


USITUMAINIE HEKALU LA BWANA


Bwana wa mavuno ni nani? (Mathayo 9:38)


UKUMBUKE HUSIA WA BWANA.  

LEAVE A COMMENT