Je! Ni kweli mtume Paulo alipingana na maandiko ya nabii Yoeli? (Yoeli 2:28)

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

SWALI: Nabii Yoeli alitabiri kwa uweza wa Roho wa Mungu na kusema..

Yoeli 2:28  Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume KWA WAKE, WATATABIRI, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; 

29 tena juu ya WATUMISHI WENU, WANAUME KWA WANAWAKE, katika siku zile, nitamimina roho yangu. 

Harafu baadae anakuja mtume Paulo na kumwandikia Timotheo hivi..

1 Timotheo 2:12 Simpi mwanamke RUHUSA YA KUFUNDISHA, WALA KUMTAWALA MWANAMUME, bali awe katika utulivu.

13 KWA MAANA ADAMU NDIYE ALIYEUMBWA KWANZA, na Hawa baadaye. 

Na pia hata katika waraka wake kwa Wakorintho aliandika hivyo hivyo..

1 Wakorinto 14:34 Wanawake na wanyamaze KATIKA KANISA, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo. 

Je! Hapo si ni wazi kuwa, kwa maneno hayo mtume Paulo alipingana na maandiko ya nabii Yoeli aliyesema Mungu atamwaga Roho wake kwa wanaume na WANAWAKE? Kwa sababu Paulo anakataza wanawake kuwatawala wanaume katika kanisa na huku Nabii Yoeli alisema Mungu atamwaga Roho yake kwa wanawake.


JIBU: Roho aliyekuwa ndani ya nabii Yoeli ndiye Roho huyo huyo aliyekuwa ndani ya mtume Paulo, na kamwe huyo Roho hawezi kujipinga, hivyo, mtume Paulo hakuwahi pingana kwamwe na maandiko ya nabii Yoeli wala manabii wengine na wala torati ya Musa, kwani yote aliyoyahubiri na kuyasema ni yale yale tu ambayo manabii na Musa walikwisha yasema zamani kwamba yatakuja kutokea.

Matendo 26:22  Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, WALA SISEMI NENO ILA YALE AMBAYO MANABII NA MUSA WALIYASEMA, kwamba yatakuwa;

Licha ya  hivyo, mtume Paulo alilifahamu pia andiko linalosema..

Mithali 30:5 KILA NENO LA MUNGU LIMEHAKIKISWA; Yeye ni ngao yao wamwaminio.

6 USIONGEZE NENO KATIKA MANENO YAKE; ASIJE AKAKULAUMU, UKAONEKANA U MWONGO.

Lakini ni Kwanini inaonekana kana kwamba mtume Paulo alipingana na nabii Yoeli au torati ya Musa, wakati Paulo mwenyewe anasema hasemi chochote kilicho  tofauti na hayo? Na kikubwa zaidi Roho ni huyo huyo mmoja? Kwa Mfano; Torati inakataza vyakula fulani visiliwe kwa sababu ni najisi, harafu anakuja Paulo anasema najua sana na tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu kwamba, hakuna kilicho najisi kwa asili yake? 

Warumi 14:14 Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi. 

Jibu ni kwamba, sisi tunakosa ufunuo wa maandiko ambao mitume walikuwa nao na kutaka kutumia fahamu zetu na elimu zetu kutafasiri maandiko kitu ambacho wengi kinatufanya twende kinyume na neno la Mungu, mtume Paulo na mitume wengine hawakuhubiri tofauti na maneno ya manabii, na hata watumishi wote wa Mungu sasa hivi hawapaswi kuhubiri yaliyokinyume na maandiko matakatifu, kwani neno la Mungu limehakikishwa na kuthibitishwa.


Sasa kwanini mtume Paulo anakataza mwanamke kumtawala mwanamume katika kanisa? Sababu zipo nyingi lakini leo tuitazame hii moja ambayo pengine ni ngeni kwako. 

Kwanza kabisa, tunafahamu kuwa, kanisa (kama mke) linapaswa kumtii Kristo (mume), na KUTAWALIWA NAE, na wala si Kristo kulitii kanisa au Kristo KUTAWALIWA NA KANISA kwa sababu Kristo ndiye kichwa cha kanisa. Vivyo hivyo pia, kichwa cha kila mwanamke ni mwanamume (1 Wakorintho 11:3) na mwanamke anapaswa kumtii mume kama vile kanisa (mke) linavyomtii Kristo.

Hivyo basi, endapo ikitokea mwanamke anamtawala mwanamume katika kanisa ni sawa na Kristo KUTAWALIWA NA KANISA  na KULITII KANISA, kitu ambacho hakiwezekani.  Kristo hawezi tawaliwa na kulitii kanisa kwani yeye ni kichwa, na mwanamume hawezi kutawaliwa na mwanamke katika kanisa kwani kichwa cha kila mwanamke ni mwanamume (1 Wakorintho 11:3)


Mwanamke hajapewa mamlaka ya kufungua kanisa, kuwa na kanisa, au kuwa mwangalizi wa kanisa, hiyo ni roho ya yerebeli, mwanamke unayesoma ujumbe huu fahamu kuwa, huna ruhusa ya kuwa mchungaji au askofu katika kanisa kwani utakuwa unawatawala wanaume katika hilo kanisa kitu ambacho ni kinyume na mafundisho ya mitume.

Watu wengi wanatumia andiko hilo la Yoeli kuhararisha wanawake wachungaji na maaskofu kitu ambacho sio sawa, biblia haijasema kuwa wakimwagiwa Roho wa Mungu watakuwa maaskofu au wachungaji, hapana! Biblia ilisema watatabiri, na kutabiri sio kuwa mchungaji au askofu.

Mwanamke anaweza kunena kwa lugha kanisani, anaweza ona maono, anaweza tumiwa na Mungu kufanya uponyaji na kuwaombea watu, anaweza kutabiri kama wale mabinti wa Filipo, anaweza shuhudia na kufikisha ujumbe aliopewa na Bwana popote pale, iwe kanisani au mtandaoni, lakini hana ruhusa ya kuwa mchungaji au askofu na kufundisha katika kanisa, umepewa ujumbe kufikisha katika kanisa, basi fikisha kama Mariamu Magdalene alivyofikisha, mengine tofauti na hayo huna mamlaka nayo, Mariamu Magdalene hakwenda kufungua kanisa na kuanza kujiita mchungaji au askofu au mtume, na wala hakwenda kusimama hekaluni.


Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa, mtume Paulo hakupingana na maneno ya nabii Yoeli, na nabii Yoeli hakuhararisha wanawake kuwa maaskofu, wachungaji na wala kumtawala mwanamume katika kanisa, na mtume Paulo alichosema ndicho Mungu alichokisema Edeni kuwa mwanamke atatawaliwa na mwanamume, tena Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, ukitaka kuwa mjinga endelea kuwa mjinga 

1 Wakorinto 1436 AU JE! NENO LA MNGU LILITOKA KWENU? AU KUWAFIKIA NINYI PEKE YENU?

37 MTU AKIJIONA KUWA NI NABII AU MTU WA ROHONI, NA AYATAMBUE HAYO NINAYOWAANDIKIA, YA KWAMBA NI MAAGIZO YA BWANA.

38 LAKINI MTU AKIWA MJINGA, NA AWE  MJINGA. 

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Bwana akubariki, Shalom.

 +255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI


Je! Umeiamini Injili Ipi?


Je! Ni dhambi kwa mwanamke wa Kikristo kuvaa suruali?


Kuuza cheni na hereni ni sawa kwa Mkristo?


ONDOENI MIUNGU MIGENI ILIYO KWENU.


IJAPOKUWA NALIWAUZUNISHA KWA WARAKA ULE, SIJUTI

LEAVE A COMMENT