Ndugu mpenzi, ikiwa na wewe ni miongoni mwa watu walioamua kujitwika misalaba yao binafsi na kumfuata Bwana sawasawa na neno lake katika (Marko 8:34), basi tambua kwamba, huna budi kukumbuka maneno yake ya husia kila siku unapojikana nafsi yako na kijitwika msalaba wako. Kama vile wengi wetu tunapopata nguvu ya kujibidiisha na mambo ya dunia hii mfano elimu, kipindi tu! tunapoyakumbuka maneno ya husia ya wazazi na walezi wetu, pale walipotuambia tusome kwa bidii, ndivyo na sisi pia inavyotupasa kuyakumbuka maneno ya husia ya Bwana Wetu Yesu Kristo ili yatutie nguvu wakati tutembeapo katika njia nyembamba na iliyosonga hapa duniani. Bwana alituhusia kwa kusema…
Matayo 10:25 Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake?
Ndugu, ikiwa umefanyika kuwa mwanafunzi na mtumwa wa Yesu Kristo kweli kweli, hakuna namna utaweza kwepa aliyopitia mwalimu wako na Bwana wako, kama Bwana wako na Mwalimu wako aliambiwa ana pepo unategemea vipi wewe mwanafunzi wake kuambiwa kuwa una Roho Mtakatifu pale utakapoamua kuacha mapambo, kuvaa nusu uchi, vimini na suruali? (Udunia), Ni kitu ambacho hakiwezekani, hivyo huna budi kutokunung’unika kwa ajili ya hivyo bali ukumbuke huo husia wa Bwana.
Unapopitia shida na dhiki, matusi na kejeli, masengenyo na kuchekwa, na pengine hata kutengwa na marafiki na ndugu kwa sababu tu umeamua kumfuata Kristo Mwokozi Wako na injili yake kwa kujikana nafsi yako na kujitwika msalaba wako, basi songa mbele na usikate tamaa katika safari yako, simama imara na uukumbuke husia wa Bwana unaosema..
Yohana 15:20 LIKUMBUKENI LILE NENO NILILOWAAMBIA, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.
Tambua kwamba, wewe sio wa kwanza, wapo wanafunzi na watumwa wengine wengi wa Bwana waliopitia hayo unayoyapitia wewe sasa, na pengine yanaweza kuwa makubwa kushinda yako, waliitwa wapindua ulimwengu (Matendo 17:6), watu wenye wazimu, wasio na elimu, wasaliti, waliuawa kwa upanga (matendo 12:2), walipigwa mawe hadi kufa kama Stefano n.k, lakini hawakuvunjika mioyo wala kukata tamaa kwa sababu ya tumaini la thamani walilokuwa wakilitazama mbele yao, kwani walifahamu hawapaswi kuamini tu, bali na kuteswa kwa ajili ya Kristo.
Wafilipi 1:29 Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, SI KUAMINI TU, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;
Walizingatia husia wa Bwana, kwamba ulimwenguni wanayo dhiki na yeye mwenyewe alifanyika kielelezo kwa dhiki na mateso kama hayo ambayo hatuna budi na sisi kuyapitia..
1 Petro 2:21 Kwa sababu ndio mlioitiwa; MAANA KRISTO NAYE ALITESWA KWA AJILI YENU, AKAWAACHIA KIELELEZO, MFUATE NYAYO ZAKE.
Hivyo, Maneno hayo ya husia ya Bwana yakupe nguvu kila saa na kila dakika unapoyakumbuka wakati unapomfuata yeye kila siku na msalaba wako, kwani kwa kufanya hivyo na kushinda tutamiliki nae, lakini tukishindwa na kumkana, naye atakukana.
2 Timotheo 2:12 KAMA TUKISTAHIMILI, TUTAMILIKI TUTAMILIKI PAMOJA NAYE; KAMA TUKIMKANA YEYE, YEYE NAYE ATATUKANA SISI;
Ukumbuke husia wa Bwana
Bwana atusaidie sana, Shalom.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
JIFUNZE TABIA HII KUTOKA KWA MITUME ANDREA NA FILIPO.
INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI