Ni maovu yapi yanayotoka kinywani mwa Bwana kulingana na (Maombolezo 3:38) 

  Maswali ya Biblia, Uncategorized


SWALI: Tukisoma kitabu cha (Maombolezo 3:38), nabii Yeremia anasema kwamba, katika kinywa cha Bwana kunatoka MAOVU na mema, sasa je! Ni maovu yapi hayo yanayotoka kinywani mwa Bwana? Ni matukano? Uongo, Umbea au usengenyaji?

Maombolezo 3:38 Je! Katika kinywa chake Aliye juu HAYATOKI MAOVU na mema? 

JIBU: Andiko hilo halimaanishi kuwa Mungu anatoa matukano, usengenyaji, umbea, uongo n.k, hapana! Halina maana hiyo kwa sababu, Mungu Yeye ni Mtakatifu na Mkamilifu, asiyekosea katika njia zake zote, na tena, kama angekuwa anatoa maneno hayo ya matukano ni wazi kuwa, angeturuhusu na sisi kuyatoa maneno hayo katika vinywa vyetu, lakini ametukataza. Sasa ni uovu upi huo unaovungumziwa hapo Ikiwa sio masengenyo, uongo n.k? 

Jibu ni kwamba, sio kila sehemu palipoandikwa neno UOVU kwenye biblia kuna maanisha dhambi, hapana! Sehemu nyingine neno hilo linamaanisha mapigo au adhabu kutoka kwa Mungu, ambayo anaiachilia juu ya watu kutokana na sababu fulani fulani, ama kujilipizia kisasi (Nahuumu 1:2), au kutaka kuwafanya wanadamu watubu na kumgeukia yeye. Kwa mfano, Mungu aliwapiga wana wa Israeli kutokana kuziacha njia zake kwa kufanya machukizo mbele zake katika nchi aliyowapa, alikusudia kuwaadhibu na kuwapeleka utumwani kutokana na kumwacha Mungu, sasa hayo mapigo na adhabu ya aina hiyo ndiyo inayofahamika kama UOVU UTOKAO KWA BWANA

Isaya 30:12 Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo; 

13 BASI, UOVU HUU UTAKUWA KWENU kama mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja. 

Soma tena

Kutoka 32:11 Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, KWA NINI HASIRA ZAKO KUWAKA JUU YA WATU WAKO uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?

 12 Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, AMEWATOA KWA KUWATENDA UOVU, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, UGHAIRI UOVU HUU ULIO NAO JUU YA WATU WAKO.


Lakini pia utajiuliza, ni kwa nini iwe kinywani mwa Bwana? Jibu ni kwamba, Mungu hana haja ya kutumia nguvu katika utendaji kazi wake kama sisi wanadamu tufanyavyo, yeye anatamka tu na inatokea, kama alivyotamka iwe nuru, iwe anga na vikatokea wakati anaumba, ndivyo anavyotakamka uovu huo na mema pia kutoka kinywani mwake.


NINI TUNACHOWEZA KUJIFUNZA JUU YA UOVU UTOKAO KWA BWANA?


Tunachoweza jifunza ni kwamba, Mungu anaachilia uovu kutokana na dhambi zetu sisi wanadamu, anaachilia kwa lengo la kutufanya sisi wanadamu tumkumbuke yeye, anaachilia magonjwa, vita, ukame njaa n.k ili wanadamu tugeuke katika njia zetu mbaya na kumfuata yeye, lakini kinachoshangaza ni kuwa, watu bado hatujatambua hilo, bado tunaendelea kutokutenda haki na kuwaomea wanyonge, bado tunaendelea na zuruma na kula rushwa, bado tunaendelea na utoaji mimba na umwagaji damu zisizo na hatia, bado tunaendelea na ushoga na usagaji, bado tunaendelea na kuabudu sanamu na kuwaomba wafu, uchawi, uganga, fitina na kila aina ya machukizo ijapokuwa tunapigwa na majanga hayo na dhiki lakini hatubadiliki na kumgeukia Mungu kama maandiko yanavyosema..

Hagai 2:17 NALIWAPIGA KWA UKAVU, NA UKUNGU, NA MVUA YA MAWE, KATIKA KAZI ZA MIKONO YENU; LAKINI HAMKUNIELEKEA MIMI, ASEMA BWANA.

Tumrudie Mungu sasa. Shalom 

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

USITUMAINIE HEKALU LA BWANA


JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO.


Je! Kuna Mungu wawili? (Kulingana na Yohana 1:1)


Je! Bwana Yesu alikuwa ni mdhambi kulingana na Mathayo 3:6? 

Bwana wa mavuno ni nani? (Mathayo 9:38)

LEAVE A COMMENT