Jina la Bwana Wetu na Mwokozi Wetu Yesu Kristo litukuzwe milele na milele, Yeye ni alfa na omega, mwanzo na mwisho, anayedumu milele na milele, Amina.
Karibu tujifunze neno la Mungu wetu, iliyo hazina na mafundisho pekee tunayopaswa kuyapokea kuliko fedha, dhahabu, na vyote vitamanikavyo katika macho ya wanadamu.
Mithali 8:10 Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi.
11 Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.
Moja ya ishara ambazo Bwana Yesu alizataja kuwa zitaambatana na wale waliomwamini na kubatizwa (katika ubatizo sahihi ambao ni kwa jina la Yesu Kristo na kuzamishwa katika maji tele), ni kuwa WATASEMA KWA LUGHA MPYA, zingine zikiwa ni uponyaji n.k
Marko 16:17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; WATASEMA KWA LUGHA MPYA;
18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Sasa, lugha hizi mpya au Kunena kwa lugha mpya kumegawanyika katika makundi mawili, kunaweza kuwa lugha za wanadamu kama zile za siku ya pentekoste (Matendo 2:8), au zinaweza kuwa lugha za malaika (1 Wakorintho 13:1), lakini leo hatutazungumzia hizo, ila nachotaka tujifunze ni kitu kingine cha ziada ambacho kinaweza kuwa kipya kwako kuhusu lugha mpya inayotoka katika kinywa cha mkristo (achilia mbali lugha za karama ambazo ni za malaika au wanadamu).
Kwanza kabisa, ukisema lugha mpya inamaanisha ni maneno au matamshi ambayo muhusika anakuwa hajawahi kuzungumza tangu hapo hawali kabla ya kumpokea Kristo katika maisha yake, anakuwa anatoa matamshi tofauti kabisa na yale ya mwanzo kabla ya kumpokea Kristo, kama alikuwa anatoa maneno ya uongo anaacha na anaanza kutoa maneno mapya ya ukweli, kama alikuwa mtukanaji kama mtume Paulo (1 Timotheo 1:13), anaacha na kuanza kusema maneno mengine mapya tofauti na yale ya matukano, au Kama alikuwa msengenyaji, msingiziaji, mbea, mwenye kulaani n.k, yote hayo anayaacha na kuanza kutoa maneno mapya ambayo ni tofauti na yele ya mwanzo katika kinywa chake (hiyo ndiyo lugha mpya kutoka katika kinywa cha mkristo ambayo nataka pia tuifahamu), kwani Roho Mtakatifu anamfanya mkristo huyo kuwa kiumbe kipya na kumpa kinywa kipya tofauti na kile cha kwanza alichokuwa nacho kabla ya kumwamini Kristo.
Biblia inasema katika…
2 Wakorinto 5:17 Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa KIUMBE KIPYA; YA KALE YAMEPITA TAZAMA! YAMEKUWA MAPYA.
Ndugu mpendwa, ukijiona bado una kinywa cha uongo, umbea, usengenyaji, matusi, usingiziaji, mizaha na utani usio na maana, story za ngono na uasherati, story za wanawake na ma-boyfriend, basi jichunguze mara mbili mbili ni roho gani uliyoipokea na iliyopo ndani yako, kwani ni wazi kuwa, kama angekua ni Roho wa Mungu, basi angekupa kinywa kipya na ungesema kwa lugha mpya tofauti na hiyo ya maneno machafu inayotoka kinywani mwako, ndivyo alivyotuangiza..
Waefeso 4:29 NENO LO LOTE LILILO OVU LISITOKE VINYWANI MWENU, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.
Bwana atusaidie kulitambua hilo;
Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.
Shalom.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
ITAMBUE NA KUIFANYA HUDUMA YA YOHANA MBATIZAJI KATIKA UKRISTO WAKO.
Je! Ni lazima mgonjwa adongoke chini pale anapoombewa?
Ni Mtume gani aliyekuwa Mkuu na Wa kwanza kuliko wote katika biblia?