NENDENI MKAJIFUNZE MAANA YAKE MANENO HAYA ‘NATAKA REHEMA WALA SI SADAKA’

  Biblia kwa kina, Maswali ya Biblia, Uncategorized

Neno la Mungu ni uzima, tena ni taa na mwanga wetu. Karibu tujifunze ili tupate kuona.

[Mathayo 9:10-13]

10 Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake.

11 Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?

12 Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.

13 LAKINI NENDENI, MKAJIFUNZE MAANA YAKE NANENO HAYA, NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.9

Kitendo cha kula na wenye dhambi kilitafsirika vibaya kwa watu wa dini, na kumwona Yesu kuwa hakutoka kwa Mungu kwa maana hashiki torati na manabii. Hapa walipomwona anakula na wenye dhambi wakakumbuka zaburi ya Daudi

[Zab 50:16-18]

16 BALI MTU ASIYE HAKI, MUNGU AMWAMBIA, UNA NINI WEWE KUITANGAZA SHERIA YANGU, NA KULIWEKA AGANO LANGU KINYWANI MWAKO?

17 Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

18 Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, UKASHIRIKIANA NA WAZINZI.

Mafarisayo walipata mashaka makubwa kwamba hawezi mtu ametoka kwa Mungu akavunja Neno la Mungu. Ndio maana walipomwendea walitaka kujua kwa nini anashirikiana(kula) na wenye dhambi? Lakini swali hilo Bwana Yesu aliwajibu kwa kuwaambia warudi wakajifunze maana ya maneno haya “NATAKA REHEMA WALA SI SADAKA”

Tujifunze kwa ufupi maneno Rehema, Fadhili na sadaka ili tuweze kuielewa vizuri hiyo sentensi aliyoisema Bwana Yesu.

 1. Rehema ni nini?
  Rehema ni neno pana sana, lakini maana hii fupi itakusaidia kupata msingi wa rehema.
  Rehema ni uwezo kuhisi huruma na kusaidia mtu au watu wakiwa katika matatizo/shida. Na mara nyingi ni pale ambapo haukupaswa kufanya hivyo.

Kwa mfano, Upo nyumbani kwako ghafla unasikia mwizi, mwizi.., Unafungua mlango uone nini kinaendelea mara unapishana na mtu anaingia ndani kwako kwa nguvu huku amelowa damu. Ukimwangalia unamfahamu tena alishawahi kukuibia hata wewe. Halafu huyo mtu anakuomba usiwaambie hao wanaomfukuza watamuua. Hapo unakuwa umebeba hatima yake, kisha kwa kumhurumia unawadanganya wanaomuulizia kuwa hayupo hapa amepitiliza. Na kweli unamponya na mauti.

Hivyo, ni nini kilichokufanya umstiri? NI HURUMA TU; Hamna sababu ya msingi angeweza kuitoa huyo mwizi na ukamwelewa kama isingekuwa ni huruma zako. Hivyo hapo umemrehemu! Na Mungu ndivyo alivyokuwa anataka; KUWAHURUMIA WENYE DHAMBI NA SIO KUISHIA KUWALAUMU!

 1. Fadhili ni nini?
  Fadhili ni moyo wa kumtendea mtu mema.
  Mfano kuwasaidia wenye uhitaji kama masikini na wasiojiweza n.k.
 2. Sadaka ni nini?
  Sadaka zilikuwa ni kafara za wanyama zilizokuwa zinatolewa kwa ajili ya mtu kusamehewa makosa/dhambi yake. Na mtu anapokuwa amekosa mbela za Mungu anakuwa hana haki mbele za Mungu lakini akisamehewa dhambi zake kwa njia ya zile kafara, anakuwa mwenye haki. Hivyo wana wa Israeli waliagizwa(lakini sio amri) kutoa sadaka ili wapate upatanisho. Lakini baada ya mda mrefu wakalifanya agizo hilo kana kwamba ni amri wakalikuza kuliko kujifunza kutenda fadhili na rehema, na Bwana akawaona kuwa wamepotea.

[Yeremia 7:22-23]

22 Maana sikusema na baba zenu, WALA SIKUWAAMURU KWA HABARI ZA SADAKA ZA KUTEKETEZWA NA DHABIHU, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri;

23 LAKINI NALIWAAMURU NENO HILI, NIKISEMA, SIKILIZENI SAUTI YANGU, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.

Bwana anasema hakuwahi kutoa amri ya kutoa sadaka bali aliruhusu na akawapa utaratibu wa kutoa sadaka, ilihitajika kutoa sadaka kwa sababu ya makosa, SI KANA KWAMBA MUNGU ALIFURAHIA KUTENDA KWAO MAKOSA ILI WAJE KUTOA SADAKA, au kwamba Mungu alifurahia wanyama kila siku wafe kwa ajili ya hatia zao, bali alitaka WAISHIKE SHERIA YAKE ILI WAWE WAKAMILIFU (mambo ya walawi 11:44-45), maana sadaka ilikuja kwa wasio wakamilifu ili Mungu asije akawagharikisha kwa hasira katika kukosa kwao kabla hawajawa wakamilifu. Lakini Israeli akatukuza sadaka/dhabihu kuliko kutenda wema, rehema na fadhili; kwa lugha nyingine Israeli hakukoma kutenda dhambi, wala kutia bidii kuacha dhambi maana dhabihu ipo ya kuwaondolea dhambi wakati wote. Kwa mda wako unaweza kusoma, Isaya 1:10-17. Hapa nitanukuu mistari michache,

[Isaya 1:11-17]

11 Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana……………..

17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.

Unaona sadaka zilimchukiza Bwana kwa sababu watu hawakuitafta Kweli bali walienda katika njia zao, na wakija mbele za Mungu walijaa wingi wa wanyama kwa ajili ya sadaka, MUNGU ALIWAONA NI WANAFIKI MBELE ZAKE.

Hadi hapo tumepata picha halisi ya kila neno ambalo Bwana Yesu alilitumia “NATAKA REHEMA WALA SI SADAKA” (Pia unaweza kusoma Mathayo 12:1-7)

Bwana Yesu alimaanisha nataka kuwahurumia wenye dhambi na kuwasaidia kutoka katika dhambi na makuhani iliwapasa watende hivyo hivyo kama anavyotenda Yesu na si kusubiri ng’ombe, mbuzi, kondoo ama njiwa zao kwa ajili ya sadaka. Na jambo hilo alitangulia kuwaambia mda mrefu huko nyuma, ndio maana akawaambia nendeni mkajifunze maana yake nini maneno haya. Tunalisoma katika,

[Hosea 6:6]

6 Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

[Mika 6:6-8]

6 Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja?

7 Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu?

8 Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda REHEMA, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

Sasa hapo ilinenwa lakini wakati wa kutimia hilo neno ndio ule mafarisayo wanashindwa kumwelewa Bwana Yesu. Yeye ndiye aliyekuja kuondoa agizo la kwanza la sadaka na kuweka la pili kama Zaburi ilivyotangulia kusema,

[Zaburi 40:6-7]

6 Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.

7 Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)

Yesu Kristo ndiye aliyeandikiwa kuyatenda mapenzi ya Bwana ambayo wana wa Israeli hawakujua kuyatenda, Na kusimamisha agano la pili. Mtume Paulo alifafanua vizuri hili,

[Waebrania 10:8-9]

8 Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati),

9 ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili.

Sasa agano la pili tulilonalo linatutaka kutenda Rehema na Fadhili, Lakini wengi huzani ni hiari kutenda fadhili na rehema. Kama tu jinsi ambavyo Mungu hakutoa amri kwa wana wa Israeli kutoa sadaka lakini ukiangalia kwa makini ilikuwa lazima wafanye hivyo maana hawakuwa wakamilifu. Na kama mtu asingetoa sadaka angekatiliwa mbali kwa ile dhambi aliyoitenda.

Hivyo na sisi kutenda fadhili na rehema ni lazima wala si hiari, utaona jambo hilo Bwana alilitaka mikononi mwa wana wa Israeli waliposhindwa kuwafadhili watumishi wake, makuhani, katika nyumba ya Bwana.

[Malaki 3:8-10]

8 Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.

9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.

10 LETENI ZAKA KAMILI GHALANI, ILI KIWEMO CHAKULA KATIKA NYUMBA YA YANGU, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.

Hizo ni fadhili kwa watumishi wa Mungu katika mali alizokupa Bwana, wakiona njaa na wewe umezuia mkono wako kuwafadhili ukizani sio lazima, Bwana atanyosha mkono wake juu yako, Pia onyesha fadhili kwa wengine kama yatima, wajane, walemavu, masikini na wagonjwa. Pia wapo masikini katika roho yaani watu walio katika dhambi, kama hufanyi juhudi yoyote wafikie toba, Mungu atalitaka mkononi mwako na mkono wake utakuwa juu yako(Ezekieli 3:18-19)

Ubarikiwe, na Bwana akupe macho ya kuona.
Maran atha!
+255755 251 999 au +255652274252


MADA NYINGINEZO

SITAWAADHIBU BINTI ZENU WAZINIPO, WALA BIBI ARUSI ZENU WAFANYAPO UASHERATI


MWANAMKE ATAOKOLEWA KWA UZAZI WAKE, JE!  NI UZAZI UPI HUO UNAOZUNGUMZIWA?


MAKANISA NA MAFUNDISHO YA UONGO YANAYOPOTOSHA WATU WENGI NYAKATI HIZI ZA MWISHO (sehemu ya 01)


MAKANISA NA MAFUNDISHO YA UONGO YANAYOPOTOSHA WATU WENGI NYAKATI HIZI ZA MWISHO (sehemu ya 02)


JE! KUNA TOFAUTI GANI KATI YA MTU WA MUNGU NA MTOTO WA MUNGU?

LEAVE A COMMENT