SITAWAADHIBU BINTI ZENU WAZINIPO, WALA BIBI ARUSI ZENU WAFANYAPO UASHERATI

  Biblia kwa kina, Maswali ya Biblia, Uncategorized

SITAWAADHIBU BINTI ZENU WAZINIPO, WALA BIBI ARUSI ZENU WANYAPO UASHERATI

Swali; Nini maana ya mstari huu “Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wao wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia.” Hosea 4:14

JIBU; Kitabu cha Hosea kimeandikwa karne ya 8 K.K, na karne hiyo hiyo Israel upande wa kazikazini iliyokuwa na makabila 10 ilichukuliwa utumwani na taifa la Ashuru. Hosea alikuwa nabii kabla hilo taifa kuchukuliwa utumwani. Kulikuwa na makosa mengi yaliyopelekea Bwana kuipeleka Isaraeli utumwani. Kwa mda wako soma kitabu chote cha Hosea utayaona, lakini sababu kubwa ya makosa hayo ilikuwa ni ufahamu mdogo kuhusu Mungu.

Hosea 4:6Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;…

Hii iliwapelekea kufanya makosa mengi, kwa kufuata desturi za miungu migeni ya mataifa hasa ya Ashuru. Ukisoma Hosea sura ya pili utaona jinsi Mungu ambaye anajilinganisha kuwa ni mume wa Israeli lakini amesalitiwa na mkewe israeli, yaani kwa kufuata desturi ya miungu mingine na huo ndio uzinzi/uasherati alioufanya. Akamkataa Mungu asiwe mme wake na kuchagua kujifunza chini ya wale miungu na kuwatumikia. BWANA akamwacha na kufukuza katika nchi yake aende kwa hao waume zake.

Hosea 2:5 Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu.

7 Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa.

8 Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye aliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali.

Unaona hapo? Hivyo kitendo cha kumpeleka Ashuru ni kwa sababu aliitumikia miungu ya Ashuru. Sawa na sisi tunapotenda matendo ya anasa za dunia, kusengenya, kusema uongo, kula rushwa, husuda, wivu, chuki, ugomvi, hasira, kuchonganisha, kuiba, uzinzi, kutukana, uasherati, kuvaa vimini, suruali kwa wanawake, kunyoa mitindo ya ki-ulimwengu, kuchora tatoo, tunasujudia sanamu za kuchonga, tunaabudu na kuombea wafu, tunaenda kwa waganga, tunafanya ushirikina n.k. Kisha, tunasema tumeokolewa na Yesu wakati hayo tunayoyafanya hayatoki kwake bali kwa shetani, kiroho tunazini na kufanya uasherati na shetani. Mwisho wetu ukiishia katika hali hiyo moja kwa moja tunakwenda kwa mme wetu tuliyemchagua ambaye ni shetani.

Sasa, turudi kwenye swali letu, Kwa nini Mungu alisema hatawaadhibu Binti na Bibi harusi kwa uzinzi walioufanya?

Moja wapo kati ya matendo ya kizinzi waliyofanya wana wa Israeli ni wanaume kuingia katika nyumba za miungu na kufanya ibada, lakini sio hilo tu bali walifanya uzinzi wa kimwili kabisa na wanawake waliohudumu katika nyumba hizo ambao waliitwa Makahaba wa Hekaluni (SACRED PROSTITUTES). Hawa walikuwa makahaba tofauti na mahakaba wa kawaida wanaojiuza kwa pesa, japo hata hawa pia walipokea pesa lakini ilikuwa kwa niaba ya lile hekalu.

Hizo pesa waliziacha hekaluni na kuchukua ujira kiasi kutoka katika pesa hizo, Walikuwepo wanaume pia waliofanya kazi hiyo hekaluni. Miungu hii ilijulikana kama miungu ya uzazi(Fertility gods). Walikuwepo wanawake ambao wao walikuja si kwa ajili ya mapato au utumishi katika hekalu bali kwa ajili ya kupata Uzazi. Hivyo walilala na wanaume wa hekaluni ili wapate kibali kwa ile miungu.

Wanaume na wanawake wa Israeli nao walipopata tatizo hilo walienda katika hii miungu. Binti za Israeli na Bibi harusi za hawa wanaume wa Isareli wengine ni wakwe, nao walifanya uzinzi na uasherati huo, pia na huu wa kimwili kabisa unaoendelea leo. Sasa Mungu akasema hatawaadhibu hawa binti wala bibi harusi kwa uzinzi wanaoufanya juu ya waume zao kwa kuwa hata waume zao nao hufanya hayo na kuabudu miungu hiyo.

Hos 4:14 SITAWAADHIBU BINTI ZENU WAZINIPO, WALA BIBI ARUSI ZENU WAFANYAPO UASHERATI; MAANA WAO WENYEWE HUENDA KANDO PAMOJA NA WANAWAKE WAZINZI, HUTOA DHABIHU PAMOJA NA MAKAHABA; NA WATU HAWA WASIOFAHAMU WATAANGAMIA.

Halelluya; Bwana anamaliza kwa kusema, hawa wote, binti, bibi arusi na wanaume wataangamia kwa kukosa ufahamu, na kinachowaangamiza si Mungu bali dhambi zao ambazo zinampa haki shetani kuangamiza maisha yao. Kama tu alivyosema katika Hosea 4:6 kuwa, watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. Na maarifa hayo ni maarifa ya kumjua Mungu, wangekuwa wanamjua Mungu vizuri wasingedanganyika kirahisi na hiyo miungu.

Hata sasa wapo watu wengi waliomwamini Yesu Kristo wanadanganyika na shetani kwa kukosa maarifa, utakupa mtu anafanya ushikirikina kwenye biashara au nyumba yake halafu anadanganywa na shetani kuwa Mungu anasaidiwa, mwingine anaabudu sanamu kwa uongo wa shetani kuwa anafanya hivyo kuwaheshimu watakatifu waliotangulia. Mwingine anafanya hivyo ili kutii dhehebu lake tu, mwingine kutii nabii wake, wengine wengi wananendea ibada za manabii na makristo wa uongo kukanyaga mafuta, maji yaliyotungiwa jina la kuwa ya UPAKO, wengine hata kupeleka udongo, nywele, kucha, na mpaka kulala na hawa manabii kimwili kabisa ili watatuliwe matatizo yao, hawana tofauti na hawa binti na bibi arusi za Israeli waliokosa ujauzito wakalala kikahaba katika mahekalu ya miungu.

Unaweza ukajiuliza kwa nini Mungu alisema Sitaawadhibu binti na bibi arusi na si wanaume? maana wote walifanya hayo hayo lakini wanaume waliofanya hivi ni wachache sana, idadi kubwa ilikuwa ni wanawake, ndio maana Mungu akawazungumzia wao. Na kama wanaume wote nao wangekuwa wasafi mbele za Mungu, Bwana angewararua wanawake peke yao.
Paulo aliliona hilo na kumwonya sana Timotheo juu ya watu kama katika kanisa.

2Timotheo 3:6 Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na KUCHUKUA MATEKA WANAWAKE WAJINGA WENYE MIZIGO YA DHAMBI, WALIOCHUKULIWA NA TAMAA ZA NAMNA NYINGI;

7 WAKIJIFUNZA SIKU ZOTE, ILA WASIWEZE KABISA KUUFIKIA UJUZI(MAARIFA) WA KWELI.

Mara nyingi watu hawa ukiwauliza Neno la Mungu utakuta wamekalili vimistari vya kusimamia kwenye uongo wao lakini Biblia hawaijui, kama vile shetani alivyosimamia vimistari kumjaribu Bwana Yesu. Kundi kubwa la watu hawa ni wanawake, Kwa kufanya hivyo wengi wanaangamizwa na shetani kwa ufahamu mdogo wa Neno la Mungu walio nao. Tubu leo, kabla Bwana hajakusumia kwenye ziwa la moto ambako ndiko liliko fungu la shetani na wote wamfuatao katika matendo yao, wala mtu yeyote asisingizie tunakombolewa kwa Neema. Neema inafanya kazi kukuleta kwa Kristo, ukiwa mtii na bidii katika Neno lake utaokolewa; lakini ukifika kwa Kristo ukakataa maarifa utaangamia pasipo shaka, Ubarikiwe.

Maran atha!

Unaweza kuwasiliana nasi kwa namba +255755251999 au +255625574252


Mada nyinginezo:

UMEMWAMINI YESU KRISTO KWA NAMNA GANI?


MWANAMKE ATAOKOLEWA KWA UZAZI WAKE, JE!  NI UZAZI UPI HUO UNAOZUNGUMZIWA?

LEAVE A COMMENT