ITAMBUE NA KUIFANYA HUDUMA YA YOHANA MBATIZAJI  KATIKA UKRISTO WAKO.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele na milele, nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya Mungu wetu aliye hai. Leo tutatazama ni kwa namna gani wakristo tunavyotakiwa kuifanya huduma ya Yohana mbatizaji katika  ukristo wetu.

Maandiko yanasema kuwa, huduma ya Yohana mbatizaji ilikuwa ni kumwandalia Bwana watu kwaajiri ya ujio wake, ambapo  kwa wakati ule watu wa Bwana walikuwa ni taifa la Israel.

Luka 1:16  Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. 

Tena, kwa roho ya Eliya alikuja ili kuwaandaa watu wa Bwana (Waisraeli) kwaajiri ya ujio wa Mungu wao, alikuja ili kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.

Luka 1:17  Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, NA KUMWEKEA BWANA TAYARI WATU WALIOTENGENEZWA. 

Na Kweli, Yohana alimwandalia Bwana watu wake kwa kuwatoa watu katika njia zao mbaya zisizo sahihi mbele za Mungu na kuwarejeza katika njia ya Bwana Mungu wao, na kisha Bwana akaja sasa katika hali ya mwanadamu. Na Yohana kwa kuifanya tu kazi hiyo, alishuhudiwa na Bwana kuwa ni mkuu kuliko wazao wote wa wanawake waliotangulia.

Matayo 11:11 Amin, nawaambieni, Hajaondokea MTU KATIKA WAZAO WA WANAWAKE ALIYE MKUU KULIKO YOHANA MBATIZAJI; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. 

Lakini baada ya Bwana kupaa kwenda Mbinguni, alitoa ahadi ya kurudi tena ili kuwachukua watu wake (Yohana 14:3) na safari hii watu wake si taifa la Israel pekee, bali hadi watu ambao si wana wa Yakobo. Na hii ilikuwa ni siri iliyofichwa tangu zamani kama mtume Paulo alivyoandika.

Waefeso 3:4  Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. 

5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; 

6 ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; 

Unaweza soma tena kwa muda wako katika kitabu cha Warumi 9:22-25

Umeona? Watu wa Bwana sasa hivi si Waisraeli pekee, bali hadi watu wasiokuwa  wa taifa la Israel.  Hivyo basi katika ujio huu wa sasa wa Bwana, watu wake wanapaswa kuandaliwa kwaajiri ya ujio huo. Kama Yohana Mbatizaji alivyowaanda watu wa Bwana kwa kuwaambia watubu dhambi zao, ndivyo ilivyo hata sasa, wakristo wanapaswa kuifanya huduma hii ya Yohana Mbatizaji kwa kuhubiri injili ya kweli isiyogoshwa, ili watu watubu dhambi zao kwaajiri ya ujio wa Bwana wa kulinyakua kanisa lake.

Watu wa Bwana wengi sasa hivi bado wapo katika giza, wengine bado wanaabudu sanamu na kuwaomba wafu, wengine bado wapo katika uzinzi na uasherati, wengine bado wapo katika ulevi na uvutaji wa sigara, wengine bado wanachuki na kuto kusamehe ndani ya mioyo yao, wengine bado wapo katika ukahaba, wengine bado wapo katika uchawi na uganga, wengine bado wapo katika utumwa wa rushwa, wengine bado wapo chini utumwa wa mafundisho ya mashetani ya kujiepusha na vyakula fulani na kuwazuia watu wasioe (1 Timotheo 4:1-3)  wengine bado wapo chini utumwa wa mafundisho ya Yezebeli ya kujipamba nyuso zao kwa make-up, wanja, kucha bandia, nywele bandia, kope bandia na mawigi, wengine bado wapo china ya mafundisho ya Wanikolai n.k  hawa wote wanahitaji kurejezwa katika njia ya Bwana, hawa wote wanapaswa kuwa tayari kwaajiri ya ujio wa Bwana wao. Sasa  kazi hii ya kuwatoa watu hawa katika giza hili si ya mtu mwingine yeyote isipokuwa ya Wakristo ambao wamekwisha kutakaswa kwa damu ya Yesu Kristo na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo na kujazwa Roho Mtakatifu.

Mfano wa Mkristo mmoja ambaye aliifanya hii huduma ya Yohana Mbatizaji ya kumwandalia Bwana watu wake ni mtume Paulo. Mtume Paulo aliwatoa watu wa Bwana katika giza na kuwaleta katika Nuru kama alivyoagizwa na Bwana mwenyewe (Matendo 26:18)

2 Wakorinto 11:2  Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. 

Vivyo hivyo na sisi Wakristo tuliojaariwa kuifafamu kweli ya Mungu kwa NEEMA ya Bwana wetu Yesu Kristo, hatuna budi kuifanya huduma hii ya Yohana Mbatizaji ya kuwarejeza watu kwa Bwana huku tukijitahidi sana na sisi kwa upande wetu na Bwana atatuweka juu kama ilivyokuwa kwa Yohana Mbatizaji.

Matayo 11:11 Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; WALAKINI ALIYE MDOGO KATIKA UFALME WA MBINGUNI NI MKUU KULIKO YEYE. 

Tafadhari shea na Wakristo wengine habari hii njema.

Bwana akubariki, Shalom.  

Maran atha!


MADA ZINGINEZO

KANISA LA KWELI NI LIPI DUNIANI?


Biblia imeruhusu ubatizo wa vichanga? (kulingana na matendo 16:33)


Je! Nikiwa naona maono si ndo basi Roho mtakatifu ninaye hivyo sina haja ya ubatizo?

LEAVE A COMMENT