Kwanini Bwana Yesu alijeruhiwa ubavuni pale msalabani?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized


SWALI: Naomba kuuliza, ni kwanini Bwana Yesu ALIJERUHIWA UBAVUNI pale masalabani? Kwanini asingejeruhiwa shingoni kwa ule mkuki pale msalabani? au kwanini asingejeruhiwa tumboni, au kwenye goti, au kifuani?…Kwanini iwe ubavuni?

Yohana 19:34 lakini askari mmojawapo ALIMCHOMA UBAVU kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. 

JIBU: Ni kweli kabisa kuwa, ipo sababu ya Kwanini Bwana Yesu alijeruhiwa ubavuni pale msalabani, na si katika tumbo au mgongo, kwa sababu tunaona hata baada ya kufufuka kwake Bwana Yesu, mtume Tomaso alililejea jeraha hilo hilo la ubavuni kama ishara ya kuamini, na Bwana alipowatokea tena kwa mara nyingine wakati mtume Tomaso akiwepo, alimwambia alete mkono wake pale, hii ikimaanisha kuwa, jeraha hilo lilikuwa lina siri nyuma yake na kulikuwepo na sababu ya kwanini Bwana kujeruhiwa ubavuni.

Yohana 20:27  Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ULETE NA MKONO WAKO UUTIE UBAVUNI MWANGU, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. 

Sasa ili tuelewe sababu ya Yesu Kristo kujeruhiwa ubavuni, hatuna budi kwanza kumchunguza Adamu, mtu wa kwanza kuumbwa, ambaye mtume Paulo alitupa siri kwamba, huyo Adamu mtu wa kwanza kuumbwa alikuwa ni mfano ya Yeye ajeye yaani Yesu Kristo (Adamu wa pili), kisha ndipo tutakapotambua sababu ya Kristo kujeruhiwa ubavuni.

Warumi 5:14 walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo NA KOSA LA ADAMU, ALIYE MFANO WAKE YEYE ATAKAYEKUJA.

Umeona hapo?..sasa tukirudi nyuma kidogo katika maandiko matakatifu, tunaona kwamba, Adamu mtu wa kwanza kuumbwa ALIJERUHIWA UBAVUNI NA MUNGU pale alipoletewa usingizi mzito (Mwanzo 2:21), na lengo la kujeruhiwa kule kwa Adamu wa kwanza ubavuni, kulikuwa ni kumletea Adamu wa kwanza mke.

Lakini pia kama tulivyoona kuwa, Adamu wa kwanza alikuwa ni mfano wa Adamu wa pili ajaye ambaye ni Kristo, hivyo basi, Kristo naye kama Adamu wa pili, ilimpasa kujeruhiwa ubavuni mwake pale msalabani kama Adamu wa kwanza kwa kusudi hilo hilo la kujipatia mke ambaye ni kanisa, mke aliyesafishwa kwa maji na damu, mke aliyevikwa kwa kitani nzuri na safi ambayo ni matendo ya haki ya watakatifu.

Ufunuo 19:7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya MWANA-KONDOO IMEKUJA, NA MKEWE AMEJIWEKA TAYARI. 

Hiyo ndiyo sababu ya Kristo kujeruhiwa ubavuni kama Adamu wa kwanza, ikufunua uhusiano wa Bwana arusi (Kristo) na mke wake (kanisa)

Waefeso 5:31 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.

 32 SIRI HIYO NI KUBWA; ILA MIMI NANENA HABARI YA KRISTO NA KANISA. 

Je! Na wewe ni miongoni mwa mke wa Kristo (Kanisa)? Kama bado unangoja nini? Chukua uamuzi leo wa kutubu dhambi zako na kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, nawe utaoshwa dhambi zako zote kwa damu na maji, na kupokesa kipawa cha Roho Mtakatifu Aliye muhuri wake Mungu.

Tafadhari, washirikishe na wengine ujumbe huu;

Bwana akubariki, Shalom.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

MWANAMKE ATAOKOLEWA KWA UZAZI WAKE, JE!  NI UZAZI UPI HUO UNAOZUNGUMZIWA?


Kwanini biblia inalitambua kanisa kama mwanamke?


Je! Ni dhambi kwa mwanamke wa Kikristo kuvaa suruali?Biblia iliandikwa na nani?


Kwanini Adamu na Hawa, Mungu aliwaita kwa jina moja ADAMU ?

LEAVE A COMMENT