Kuna jambo ambalo tunapaswa kulifahamu katika habari ya Danieli na yale maandishi yaliyoandikwa kwa vidole vya mwanadamu (kiganja cha mkono alichokiona mfalme Belshaza kikiandika katika ukuta), kwa sababu habari hiyo haikuandikwa tu kama hadithi fulani ya kujifurahisha ambayo haina funzo wala maudhui yoyote yale, bali kipo kitu cha kufahamu na kujifunza katika habari hiyo, kwani biblia inasema, kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho
2 Timotheo 3:16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;
17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
Hebu tusome mstari unaohusu habari hiyo kwa ufupi kisha tuone nini tuanachopaswa kukifahamu.
Danieli 5:5 Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika.
Ukisoma mstari huo utagundua kuwa, kiganja hicho cha mkono hakikuwa kiganja cha kawaida, bali cha muujiza ujiza, na kiliandika maneno ambayo yalikuwa na UJUMBE FULANI KUTOKA KWA MUNGU ALIYE HAI, Muumba wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana, lakini kitu cha kushangaza ni kuwa, katika ujumbe huo wa maandiko yaliyoandikwa pale kwa kiganja hicho cha mkono, hakukuwa na mtu yeyote yule aliyeweza kuyasoma maandiko yale na kuelewa tafsiri yake isipokuwa Danieli, si watu wenye hekima wa Babeli, si wachawi, si waganga, wala wanajimu, wote walishindwa kuyasoma maandiko yale na kutoa tafsiri yake kama tunavyosoma habari hiyo
Danieli 5:8 Basi wakaingia WENYE HEKIMA WOTE WA MFALME; lakini hawakuweza kuyasoma YALE MAANDIKO, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake.
Soma tena
Danieli 5:15 Basi sasa, WATU WENYE HEKIMA na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate KULISOMA ANDIKO HILI, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili.
Lakini Swali ni kuwa, kwanini Danieli ndiye aliyeweza kusoma na kutoa tafsiri ya maandiko yale?…Hapo ndipo funzo lilipo. Jibu ni kwamba, Danieli alikuwa na roho ya miungu watakatifu ndani yake, yaani Roho Mtakatifu (Daniel 5:11), ambaye alimpa nuru na ufahamu wa kuelewa mafumbo ya maandiko yale yenye ujumbe kutoka kwa Mungu, hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Danieli kuweza kusoma na kutoa tafsiri ya maandiko yale.
Danieli 5:14 Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako.
(Maneno hayo na tafsiri yake unaweza yasoma binafsi katika sura yote ya tano ya kitabu cha Danieli)
HII INATUFUNDISHA NINI?
Hii inatufundisha kuwa, hata sasa ujumbe wa Mungu, yaani Neno lake (ambaye ni Yesu Kristo), umeandikwa katika mafumbo (Luka 24:27), lakini safari hii si katika ukuta wa chokaa tena bali katika gombo la chuo (biblia takatifu)
Zaburi 40:7 Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo NIMEANDIKWA,)
8 Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
Ni ujumbe uliobeba sheria za Mungu kuhusu hatma za nafsi zetu sisi wanadamu, hivyo, ili tuweze kusoma na kupata tafsiri sahihi ya ujumbe uliopo kwenye maandiko hayo ni lazima tuwe na Roho Mtakatifu ndani yetu kama ilivyokuwa kwa Danieli, hekima zetu za vyuo vikuu, PHD, falsafa, theologia, sayansi n.k, haviwezi kutujulisha tafsiri sahihi ya ujumbe uliopo kwenye maandiko hayo ya Mungu kama ilivyokuwa kwa wale wenye hekima wa Babeli na wanajimu, badala yake tukivitegemea hivyo tutapata tafsiri zisizo sahihi na kupotea kabisa kwa sababu hekima hizo zitatutafsiria kuwa, kuwaomba watu walio kufa sio dhambi, zitatutafsiria kuvaa nusu uchi na suruali kwa wanawake sio dhambi, kuweka mawigi, kucha bandia, hereni sio dhambi, vitatutafsiria ubatizo wa kunyunyuziwa maji hauna shida, ubatizo wa watoto wachanga hauna shida, wanawake kufunika vichwa wakati wa Ibada ni uzamani, vitatutafsiria wanawake kuwa maaskofu na wachungaji haina shida haki sawa, na tafsiri nyingine nyingi Kama hizo endapo tu! tusipokubali Roho Mtakatifu atuongoze kupata tafsiri sahihi kama ilivyokuwa kwa Danieli.
Wapo watu wanaompinga Roho wa Mungu na kuziamini hekima zao wenyewe, na mapokeo ya madhehebu yao, (ndugu hapo tegemea kupata tafsiri ya maandiko ya wenye hekima na wanajimu wa Babeli wala sio tafsiri ya Danieli), wapo wengine wakielezwa habari ya Roho Mtakatifu na mafunuo yake, watakwambia usitudanganye, Kristo mwenyewe alifundisha kwa mifano, hivyo usitueleze habari za mafunuo ya Roho Mtakatifu hapa.
Mpendwa, unatakiwa kufahamu kuwa, pasipo Roho wa Mungu huwezi elewa mafumbo ya ujumbe wa Mungu yaliyopo katika biblia takatifu, na wala huwezi pata tafsiri sahihi kwa sababu Roho wa Mungu ndiye anayetueleza sisi wanadamu siri zote za Mungu
1 Wakorinto 2:10 Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.
11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.
Na habari njema ni kuwa, Roho Mtakatifu anapatikana bure kwa kila mwenye uhitaji, na tena ni ahadi ya Mungu Mwenyewe kwa yoyote yule atakayeamua kutubu dhambi zake kwa kumwamini Kristo kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38)
Ufunuo 22:17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! NAYE MWENYE KIU NA AJE; NA YEYE ATAKAYE, NA AYATWAE MAJI YA UZIMA BURE.
Shea na wengine ujumbe huu;
Bwana akubariki, Shalom.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
Nini maana ya mstari huu “unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya wanadamu” (2 Petro 2:21)
Ni maneno yapi ya unabii yaliyotangulia juu ya Timotheo? (Kulingana na 1 Timotheo 1:18)
UMEMWAMINI YESU KRISTO KWA NAMNA GANI?
BWANA ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA “HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO HEKALU?”