Makuhani wa Mungu ni watu gani katika biblia?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

Makuhani wa Mungu katika biblia ni watu waliotiwa mafuta na kuteuliwa na Mungu kwa kazi zote za ibada mbele za Mungu kwa ajili ya watu wake, mfano; upatanisho wa dhambi, kufukiza uvumba n.k na watu hawa ndio waliokuwa na NAFASI AU UWEZO wa kumsogelea Mungu kwa ukaribu zaidi. Lakini pia hata miungu mingine mfano baali, ilikuwa na makuhani wao ambao walifanya kazi za kishetani kama ilivyo tu sasa hivi (soma 2 wafalme 11:18) 


Katika taifa la Israeil, makuhani hawa wa Mungu walikuwa wengi na kulikuwa na zamu kwa kila kuhani kwenda mbele za Bwana kulingana na utaratibu wa kikuhani, Mfano; kuhani Zakaria baba yake Yohana mbatizaji ambaye wakati wa zamu yake ya kwenda mbele za Bwana, alitokewa na malaika na kuambiwa habari kuzaliwa nabii Yohana mbatizaji.


Luka 1:8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika TARATIBU YA ZAMU YAKE mbele za Mungu, 

9 kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. 

10 Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. 

11 Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. 


Ijapokuwa makuhani hawa wa Mungu walikuwa wengi, lakini pia alikuwepo kuhani mkuu miongoni mwao, ambaye huyo kila mwaka peke yake, na tena ni mara moja, huingia katika hema ya pili kwa ajili ya upatanisho wa dhambi za taifa zima la Israel. Mfano wa kuhani mkuu ni Haruni, Kayafa, n.k

Sasa kazi za ukuhani wa Mungu zilikuja kuzihirika kwa uwazi kabisa baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri (ijapokuwa kabla, Mungu alishakuwa na kuhani, mfano; Melkizedeki na watu waliofanya kazi kama hiyo inayofanana na ya kikuhani mfano; Ayubu 42:8) ambapo Mungu alilichagua kabira la Lawi kwa ajili ya utumishi katika nyumba yake, na kutoka katika kabila hilo alimchagua HARUNI NA UZAO WAKE WAKIUME TU! Katika kazi ya ukuhani, hivyo makuhani wote katika Israeli walikuwa ni wa uzao wa Haruni tu.

Kutoka 40:13 Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani. 

14 Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao; 

15 nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote. 

Lakini katika agano jipya, ukuhani huu wa Mungu unabadilika kwa sababu Mungu alimwambia Bwana Yesu (ambaye hakutoka katika kabila la Lawai) kuwa, ndiye atakayekuwa Kuhani Mkuu na wa milele kwa mfano wa Melkizedeki.

Waebrania 7:11 Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine ainuke, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni? 

12 Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. 

13 Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hiyo aliyeihudumia madhabahu.

 14 Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lo lote juu yake katika mambo ya ukuhani. 


Kufunua jinsi ambavyo watu wa mataifa, waliomwamini Bwana Yesu na kubatizwa kwa jina lake (sawasawa na matendo 10:48) na wao pia watakavyostahili kushiriki kufanywa kuwa wafalme na MAKUHANI mbele za Mungu kwa njia ya Yesu Kristo katika ufalme ujao, kwa sababu, Kama uzao wa haruni kuhani mkuu, walivyofanywa kuwa makuhani mbele za Mungu, ndivyo itakavyokuwa kwa wale wote walivyofanywa wana kwa Roho wa Kristo, Kuhani Mkuu, watakavyofanywa makuhani mbele za Mungu


Ufunuo 5:9 Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, UKAMNUNULIA MUNGU KWA DAMU YAKO WATU WA KILA KABILA NA LUGHA NA JAMAA NA TAIFA,

10 UKAWAFANYA KUWA WAFALME NA MAKUHANI kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi. 


Na ukuhani wetu mbele za Mungu katika ufalme ujao hautokuwa wa kufukiza uvumba tena, Bali ni NAFASI AU UWEZO wa kumkaribia Mungu kwa ukaribu zaidi kama ilivyokuwa kwa makuhani wa hapa duniani. Hivyo hatuna budi kuyafanya mapenzi ya Mungu na kazi yake kwa bidii kila mmoja kwa kadiri ya neema aliyopewa ili tuwe na nafasi nzuri mbele za Mungu ufalme ujao.

Bwana akubariki. Shalom 


MADA ZINGINEZO:

Pazia la Hekalu ni nini katika biblia?


Mana ni nini katika maandiko?


BWANA ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA “HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO HEKALU?”


WEWE HU MBALI NA UFALME WA MUNGU.

LEAVE A COMMENT