SWALI: Mgonjwa, au mtu mwenye mapepo, au mtu yeyote yule anapofunguliwa au anapofanyiwa maombezi, ni lazima aanguke chini?
JIBU: Jina la Bwana wetu Yesu Kristo litukuzwe milele. Kwanza kabisa inabidi tufahamu kuwa, mapepo huwa wanayo tabia hiyo ya kulipuka na kumwangusha mtu chini pale mtu anapoombewa au pepo linapomtoka mtu huyo baada ya kufunguliwa, mfano halisi ni kipinde kile ambacho Bwana alipokuwa akifundisha siku ya sabato katika sinagogi moja huko Galilaya katika mji wa Kapernaumu, kulikuwa na mtu mwenye pepo mchafu mule na Bwana alimkemea, na baada ya kukemewa, yule pepo mchafu akamtupa chini yule mtu na kumtoka. Labda tusome kidogo habari hiyo.
Luka 4:33 Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu,
34 akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu.
35 Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. NDIPO YULE PEPO AKAMWANGUSHA KATIKATI, akamtoka asimdhuru neno.
Unaona hapo? Hilo pepo lilimwangusha huyo mtu chini baada ya Bwana kulikemea, hivyo ni wazi kuwa, mapepo huwa yanatabia hiyo ya kuwatupa watu chini, na mapepo haya yalikuwa ya aina tofauti tofauti, mengine ya udhaifu, mengine ya ububu na uziwi, n.k Lakini mfano mwengine tunausoma katika katika [Marko 9:24-27] pale ambapo Bwana alipolikemea pepo la ububu na uziwi na baada ya hilo pepo kukemewa likamtupa yule kijana chini.
Sasa swali ni je! Hiyo ndiyo kanuni au amri kwamba, kila mtu mwenye shida ni lazima na yeye aanguke chini anapoombewa? Jibu ni la! Hiyo siyo kanuni wala amri kwamba ni lazima mtu aanguke chini pale anapoombewa ili kuthibitisha kuwa amefunguliwa kutoka katika shida yake, kwasabubu sio watu wote waliofunguliwa na Bwana walidondoka chini, sio mabubu wote waliofunguliwa na Bwana walianguka chini, na sio waliokuwa na udhaifu wote ambao Bwana aliwafungua walidondoka chini. Mafano halisi ni yule mwanamke ambaye alikuwa na pepo wa udhaifu kwa muda miaka kumi na nane na kumsababishia kupinda kabisa, sasa Bwana alipomfungua mwanamke huyo kutoka katika kifungo hicho cha pepo huyo wa udhaifu baada ya kumwekea mikono, maandiko hayasemi kuwa yule mama alianguka chini pale, badala yake yanasema kuwa, alinyoka saa ilele ile na akaanza kumtukuza Mungu.
Luka 13:11 Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na PEPO WA UDHAIFU muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.
12 Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.
13 Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.
Sasa watumishi baadhi kwa kushindwa kuelewa hichi kitu kuwa, si kanuni wala si sheria kwamba, lazima mtu aanguke chini anapoombwe, kumepelekea kuwapo na tabia kwa baadhi ya waombeaji ambayo si sawa kabisa katika makanisa, na tabia hiyo ni baadhi ya waombeaji kutumia jitihada zao au nguvu zao binafsi kutaka kuwaangusha watu pale wanapowaombea wakizani kwamba, wakimwangusha mtu kwa mbinu hiyo na watu wakiona, basi, watazidi kuaminika sana, ndugu yangu unayefanya hivyo, unatumia mbinu hizo za uongo ili kutafuta utukufu wa nani? Je! Unafanya hivyo ili utafute utukufu wa wanadamu? Basi fahamu kuwa, hivyo si sawa kabisa mbele za Mungu, acha Bwana atende mwenyewe kwa uweza wake. Wewe kazi yako kama mwombaji ni kuomba kwa Bwana na hizo ishara zitakufuata tu, na wala usitake kuzitengeneza.
Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.
Bwana akubariki, Shalom.
Maran atha!
MADA ZINGINEZO:
Bado Bwana Yesu anasema nawe kwa mifano?
Mailaika mikaeli ndiye Bwana Yesu?
Omri ni nani kwenye maandiko na sheria zake ni zipi? (Mika 6:16)