KWA SABABU NALIWAOGOPA WALE WATU, NIKATII SAUTI YAO. 

Shalom, jina la Bwana litukuzwe. Karibu tena katika kuyatafakari maneno ya uzima ya Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo.

Kwenye maandiko kuna mfalme mmoja wa taifa la Israel aliyeitwa Sauli, ambaye pia alikuwa ni mfalme wa kwanza wa taifa hilo. Mfalme huyu kuna siku Mungu alimpa AGIZO  kupitia nabii Samweli la kwenda kuwaamgamiza Waamaleki wote katika nchi yao, wanaume na wanawake, watoto wachanga wanyonyao, mifugo yote kama ng’ombe, kondoo, punda, na ngamia bila kuacha chochote.

1 Samueli 15:3  Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda. 

Kwa urefu unaweza soma habari hiyo katika (1 Samweli 15:1-7). 

Na ni kweli Sauli alienda kuupiga ule mji wa Waamaleki, lakini alishindwa kutenda kama Bwana ALIVYOMWAGIZA kufanya, kwani Bwana alimwambia aangamize kila kitu, wanaume, wanawake, watoto wachanga wote, kondoo, ngamia n.k lakini yeye alimwacha mfalme wa Waamaleki  na baadhi ya wanyama wakiwa hai, kinyume kabisa na maagizo aliyopewa na Bwana. Sasa si kwamba mfalme Sauli hakuwa na nia ya kufanya kama Bwana alivyommbia la! Nia alikuwa nayo sana ya kutenda agizo la Bwana, lakini kwanini sasa Sauli hakufanya kama Bwana alivyoagiza? Jibu ni kwamba, wakati Sauli alipotaka kufanya agizo la Mungu, kumbuka pale walikuwepo watu wengine ambao walishiriki pamoja na Sauli katika kuwaangamiza Waamaleki, hawa watu hawakuwa tayari kuyafanya mapenzi ya Mungu, walitaka kufanya walichoona wao kuwa sahihi, kwamba, hatupaswi kuangamiza mifugo yote hii. Sasa kwa kuwa watu wote hao walikuwa na wazo hilo la kuondoka na mfalme wa Waamaleki na baadhi ya mifugo, Sauli aliwaogopa wale watu na kushindwa kufanya AGIZO LA Mungu na kutii sauti ya wale watu.

1 Samueli 15:24  Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana NIMEIHARIFU AMRI YA BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu NALIWAOGOPA  WALE WATU, NIKAITII SAUTI YAO. 

Umeona? Sauli kwa kuwaogopa wale watu  kwamba watampiga au wata mfanya chochote   alishindwa kutekeleza AGIZO la Mungu kwa kuwaogopa watu wale. Sasa hichi kitu kinatufundisha nini sisi watu wa sasa hivi? Maandiko yanasema kuwa, mambo hayo yaliandikwa ili kutuonya na sisi watu tunaoishi kwenye agano jipya kupitia mjumbe wa agano hilo jipya yaani Yesu Kristo (Waebrania 9:15) 

Sasa Wakristo wengi leo hii ni kama Sauli, wanashindwa kuyashika MAAGIZO YA MUNGU kwa kuwaogopa watu, ama ndugu, wazazi n.k Wakristo wanashindwa kuacha kuabudu sanamu kwasababu wanawaogopa wazazi wao, wakristo wanashindwa kuacha kwenda kwa waganga wa kienyeji kwa sababu wanawaogopa wazazi wao, wanashindwa kushika maagizo ya Mungu kwa kuwahofia ndugu zao. Mkristo anashindwa kutekeleza agizo la ubatizo sahihi baada ya kuhubiriwa na kuamini kabisa kwasababu anahofia mume wake au mama yake au dada yake. Ndugu yangu, ni heri ukatii maagizo ya Mungu, kuliko mwanadamu, ni heri ukatii agizo la Mungu la kuvaa mavazi ya heshima kuliko kumwogopa huyo bosi wako, ni heri ukashika agizo la Mungu la kuacha kuwaomba hao wafu kuliko kumwogopa baba yako, kwani tusipofanya hivyo yatatupata kama yaliyompata mfalme Sauli.

 Kumtii Mungu ni bora kuliko kumtii mwanadamu, hata wakati ule mitume Petro na Yohana walipokatazwa na baraza kutokuhubiri wala kufundisha kwa jina la YESU, waliwauliza watu wa baraza kwamba, hukumuni ninyi wenyewe kama ni vyema kumtii Mungu au mwanadamu.

Matendo Ya Mitume 4:18  Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.

 19 Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; 

Ndivyo hivyo na sisi pia, tunapaswa kutii maagizo ya Bwana wetu Yesu Kristo kuliko wanadamu. Mungu atujaalie neema ili tuwe na ujasiri wa kumtii yeye na kumkiri yeye katika njia zetu. 

Tafadhari, washirikishe na wengine habari hizi njema.

Bwana akubariki Shalom.


MADA ZINGINEZO

HATAINGIA NDANI YAKO ASIYETAHIRIWA.


Ni lini Bwana alivitakasa vyakula vyote kulingana na 1 Timotheo 4:3?


Biblia imeruhusu ubatizo wa vichanga (kulingana na matendo 16:33?)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *