Nini maana ya shekina, Je Utukufu wa shekina una maana gani?

Uncategorized No Comments

JIBU…

Shekina au shekhinah /schechinah, Ni neno la kiyahudi linalomaanisha, “kutua” au “kuweka makao” au “makazi” ya uwepo wa Mungu duniani… Basi utukufu wa shekina maana yake ni kujifunua kwa uwepo wa Mungu kwa dhahiri duniani, na kujifunua kwake kunaweza kuchukua mfumo wa vitu mbalimbali vya asili kama vile moto, wingu,moshi,mwanga, kijiti kinachoteketea n.k.,..

Shekina huwezi kulikuta kwenye biblia, lakini maudhui yake ipo ndani ya biblia.. Ni neno lililoanzishwa, na waalimu wa kiyahudi , (Marabi) , na yalionekana kwenye fasihi zao na maandishi yao ya kale, kipindi cha pale katikati kutoka agano la kale kuelekea agano jipya..

Mara ya kwanza utukufu wa Shekina kuonekana ilikuwa ni siku ile wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, kuelekea Jangwani walipokuwa pale Sukothi, siku hiyo ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kuuona uwepo wa Mungu dhahiri katika wingu na nguzo ya moto,

Kutoka 13:20 “Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa.

21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;

22 ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu”.

  • Ulikuja kuonekana tena ndani ya hema ya kukutania, kule jangwani;  Soma (Walawi 16:2, 1Wafalme 8:10-11)
  • Ulikuja kuonekana tena Hekaluni, kipindi kile ambacho Sulemani analiweka wakfu hekalu la Bwana (1Wafalme 8:10-11)
  • Ulionekana tena siku ile Mungu alipomthibitishia Ibrahimu agano lake alipokuwa amelala, na moto ukashuja juu ya madhabahu,aliyokuwa ameitengeneza, Mwanzo 15:17
  • Ulionekana pia kwa Ayubu wakati ule Mungu alipomtokea katika upepo wa kisulisuli na kuzungumza naye dhahiri (Ayubu 38-42)
  • Katika agano jipya tunaona ulionekana kwa Paulo siku ile alipokuwa anatoka Yerusalemu na kuelekea Dameski ili kuliharibu kanisa la Mungu, ndipo utukufu wa Mungu ukamtokea katika mwanga mkali na Kristo kuongea naye.. Matendo 9:3
  • Na utaonekana pia katika ile Yerusalemu mpya ambayo  tunayoingojea huko mbeleni (Ufunuo 21:23-..

Na Kadhalika..

JE! NA SISI TUNAWEZA KUKUTANA NA UTUKUFU WA SHEKINA?

Pamoja na kwamba Mungu alijifunua dhahiri katika vitu vingi vya asili, kwa watu wachache, lakini kuna wakati ambao aliuweka mahususi kwa ajili ya kujifunua kwa watu wote, katika viwango vya juu kabisa vya utukufu wake ambao havijawahi kutokea hapa duniani.. Utukufu ambao ni zaidi ya wingu, au nguzo ya moto, au moshi, au tufani..na huo sio mwingine zaidi ya mwili wa Mwanadamu, ulioitwa YESU KRISTO. Biblia inatuambia kabisa kuwa Yesu alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyechukua umbo la kibinadamu na kuishi na sisi (1Timotheo 3:16)Na yeye ndiye utukufu pekee wa Mungu ambao alishawahi kufunua hapa duniani tangu dunia iumbwe..Yohana 1:14

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”.Soma tena..Wakolosai 2:9 “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili”.Hivyo kwa kifupi tunaweza kusema utukufu wa shekina tulionao sasa ni YESU KRISTO. Na kila mmoja wetu ameweza kumwona Mungu zaidi hata ya wale waliotokewa katika nguzo ya moto, ikiwa tu atakubali kuingia katika neema yake..Swali ni Je! Utukufu huo umefunuliwa ndani yako?

Je Umempokea Yesu katika maisha yako?. Kumbuka hakuna njia yoyote utakayoweza kumfikia Mungu, au hata kumjua Mungu isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo. Jiulize, ulimwengu umekuahidia nini tangu umeanza kuutumikia? Ukweli ni kwamba haujakupa ahadi yoyote, ya kuendelea kuishi, Lakini Kristo anakuahidia uzima wa milele baada ya kufa, kwanini usichague uzima, na mengine mengi?

Kama upo tayari leo hii kuyakabidhi maisha yako kwa Yesu, ili utukufu huu halisi wa Shekina uweze kuja juu yako, basi huo ni uamuzi wa busara sana kwako. Ikiwa jibu ni ndio, wasiliana nasi kwa namba hii 25593036618,255789001312

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba zetu hapo juu..

NURU YA UPENDO” Kwa kubofya hapa>> WhatsApp: https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *