Shalom, jina la Bwana wetu na Mungu wetu lipewe sifa milele na milele. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi wetu Yesu Kristo.
Maji ni moja ya vitu ambavyo ni muhimu sana kwaajili ya uhai wa mwanadamu, na ndio maana hata wana wa Israeli walipotembea siku tatu katika jangwa la shuri bila kuona maji walilalamika kwani walijua wazi kabisa kuwa, pasipo maji wasingeweza kuishi
Kutoka 15:22 Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani WASIONE MAJI.
23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.
24 NDIPO WATU WAKAMNUNG’UNIKIA MUSA, WAKISEMA, TUNYWE NINI?
Ijapokuwa walikuwa na hofu ya kufa kwa kukosa maji lakini walikufa wote jangwani ingawa waliyapata hayo maji waliyodhania kuwa ni uhai kwao (isipokuwa Yoshua na Karebu). Hii haimaanishi kuwa wao hawakuwa sahihi kudhania kuwa maji ni uhai kwaajili ya nafsi zao, walikuwa sahihi sana kudhani hivyo, kama vile tu ilivyo leo hii kwa wanasayansi wanavyodhani hivyo na kuwasisitiza watu umuhimu wa maji. Isipokuwa tunashindwa kuelewa ni maji yapi hayo ambayo yanaleta uhai kwa nafsi zetu, ni maji yapi hayo ambayo tukinywa hatuwezi pata kiu tena na ni nani huyo aliye na hayo maji.
Yeremia 17:13 Ee Bwana, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, KWA SABABU WAMEMWACHA BWANA, KISIMA CHA MAJI YALIYO HAI.
Kumbe Mungu mwenyewe, ndiye kisima cha hayo maji yaletayo uhai, ndiye anayetoa hayo maji ya uzima na ndiye chemchemi ya maji ya uzima, umeona? Na ndio maana maandiko yanasema.
Ufunuo 21:5 NA YEYE AKETIYE JUU YA KILE KITI CHA ENZI AKASEMA, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.
6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. MIMI NITAMPA YEYE MWENYE KIU, YA CHEMCHEMI YA MAJI YA UZIMA, BURE.
7 Yeye ashindaye atayarithi haya, NAMI NITAKUWA MUNGU WAKE, naye atakuwa mwanangu.
Ndugu yangu, maji hayo ya uzima yanatolewa hadi sasa, na tena ni bure kwa kumwamini Bwana Yesu na kudhamilia kuacha dhambi zako zote na kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi kwani Bwana Yesu yupo tayari kutoa maji haya bure kwa kila mwenye kiu.
Yohana 4:13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;
14 WALAKINI YE YOTE ATAKAYEKUNYWA MAJI YALE NITAKAYOMPA MIMI HATOONA KIU MILELE; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
Mpendwa ambaye bado huna maji haya ndani yako fahamu kuwa utakufa, kwani pasipo maji hakuna uhai, hivyo usimwache leo hii huyu Mungu aliye chemchemi ya maji ya Uzima kwani ukinywa maji yake kwa kutubu dhambi zako na kubatizwa katika ubatizo sahihi basi, uhai utakua ndani yako na utaishi milele kama alivyotuahidi.
Yohana 11:25 Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;
Hivyo kama unavyopambana ili upate maji ya kunywa pale unapo hisi kiu, basi vivyo hivyo, pambana kwa nguvu ili uyapate haya maji ya uzima, haijalishi kuwa utapoteza marafiki, utatengwa na ndugu, utaonekana mtu aliyepitwa na wakati, wewe usiangalie hayo bali akili yako na mawazo yako yawe kwa huyu aliye chemchemi ya maji ya uzima.
Ubarikiwe na Bwana.
Mada zingizeno:
KWANINI MNANIITA BWANA, BWANA, WALAKINI HAMYATENDI NISEMAYO?
Kwanini wale askari hawakumvunja miguu Bwana Yesu?(Yohana 19:36)