Kufunua Marinda ni nini katika biblia? (Yeremia 13:26) 

SWALI: Bwana alimaanisha nini aliposema, nitayafunua marinda yako? na neno marinda ni nini katika biblia kama tunavyosoma katika Yeremia 13:26?

Yeremia 13:26  Kwa ajili ya hayo, mimi nami NITAYAFUNUA MARINDA yako mbele ya uso wako, na aibu yako itaonekana. 

JIBU: Marinda ni vazi linalovaliwa na wanawake ambalo hufungwa kuanzia kiunoni na kuning’inia hadi miguuni kwa lugha ya sasa hivi ni sketi (tazama picha). Neno hilo pia tunaweza lisoma katika 

Yeremia 13:22  Nawe ukisema moyoni mwako, Mbona mambo haya yamenipata mimi? Ni kwa sababu ya wingi wa uovu wako, marinda yako yamefunuliwa, na visigino vya miguu yako vimeumia. 

Ukisoma maandiko utagundua kuwa, Bwana alilifananisha taifa la Israel na mwanamke, na sio taifa hilo tu bali hata mataifa mengine tofauti na Israel nayo aliyafananisha na wanawake kwa kuwaita wapenzi wake.

Warumi 9:25  Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu. 

Hivyo basi, Mungu aliliona taifa lake takatifu kama mwanamke, lakini kutokana na uovu uliokuwa ukiendelea katika taifa hilo, watu kuabudu mabaali na kuyafukizia uvumba, watu kupitiasha watoto wao kwenye moto, dhuluma kwa wasiojiweza kuongezeka, Mungu aliwaona kama wanaficha huo uovu ndani ya marinda(sketi) zao.

Maombolezo 1:9  Uchafu wake ulikuwa KATIKA MARINDA yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, Bwana, teso langu; Maana huyo adui amejitukuza. 

Sasa ulipofika wakati wa Mungu kuwaaibisha mbele ya adui zao na kuwatia aibu kwa kuwafanya wapigwe na kupelekwa utumwani, ndipo Mungu akatumia huo mfano ili wapate picha jinsi gani hiyo aibu yao itakapowapata kwa kuwafunua sketi zao (marinda)  na kuwa uchi mbele za watu, fikiria ni aibu kubwa kiasi gani? Na Mungu anasema ni mbele za watu, unaweza vuta picha kuwa ni kitendo cha aibu kiasi gani? Lakini msemo huu Mungu aliutumia pia hata kwa mji wa Ninawi kutokana na uovu wao kuwa mwingi, hivyo akadhamilia kuuadhibu mji huo kwa ghadhabu ambayo ilipelekea kuwa kama aibu kwao, kuwa kama mwanamke aliyefunuliwa sketi yake harafu utupu wake kuonekana na watu wote.

Nahumu 3:5  Tazama, mimi ni juu yako, asema Bwana wa majeshi; nami NITAFUNUA MARINDA yako mbele ya uso wako; nami nitawaonyesha mataifa uchi wako, na falme aibu yako.

6  Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau.

7  Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji? 

Hata na sisi pia, Mungu anatutazama kama alivyowatazama na hawa, ulevi wetu tunaoufanya kwa siri siri na huku tunasema kuwa tumeokoka ipo siku Mungu atafunua marinda yetu na itakuwa aibu kwetu, uzinzi wetu tunaoufanya kwa siri siri na huku tunasema kuwa ni wakristo ipo siku Mungu ataufunua hadharani kama tusipotubu na kuwa aibu kwa watu wote.

Wewe baba, huyo mke wa mtu unayezini naye kwa siri siri ukidhani kuwa hakuna anayejua, basi fahamu kuwa, ipo siku Mungu atafunua huo uovu wako kama usipotubu. Mchungaji unayefanya uasherati na waumini wako kwa siri siri jua ipo siku Mungu atafunua hiyo aibu yako usipotubu. Mvulana/msichana unayefanya masturbration kwa siri na kutazama picha za ngono ukidhani kuwa hakuna anayekuona, fahamu kuwa ipo siku Mungu atafunua huo uchafu wako tena mbele za watu na kuwa aibu kwako, hivyo tubu leo ndugu yangu.

Haijalishi umefanya hivyo mara ngapi, lakini ukitubu leo  na kukusudia ndani ya moyo wako kwa kudhamiria kuacha hivyo vitu basi utapata rehema kwani Bwana alikufa kwaajili ya hayo.

Mithali 28:13  Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. 

Na kama bado hujampa Bwana maisha yako basi huu ndio wakati sahihi unaposikia ujumbe huu wa Mungu, kwani mlango wa neema bado upo wazi, haijalishi ni mdhambi kiasi gani njoo kwa Bwana Yesu upate ondoleo la dhambi zako kwa kumwamini na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu (matendo 19:5) na kuishi maisha ya usafi na utakatifu.

Bwana akubariki.


Mada zinginezo:

Je biblia inaruhusu kubatizwa kwa ajili ya wafu?(1Wakorintho 15:29)


Ni lini Bwana alivitakasa vyakula vyote kulingana na 1 Timotheo 4:3?


Mede ni nini kama tunavyosoma katika Wafilipi 3:14?


Je! neno “Mego” linamaana gani katika biblia?


Je! Busu kanisani kwa watu wanaofunga ndoa ni sawa? 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *