HATAINGIA NDANI YAKO ASIYETAHIRIWA.

Shalom, jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima. Maandiko yanasema katika 

Isaya 52:1   Amka, amka, jivike nguvu zako, Ee Sayuni; Jivike mavazi yako mazuri, Ee YERUSALEMU, MJI MTAKATIFU; KWA MAANA TOKEA SASA HATAINGIA NDANI YAKO ASIYETAHIRIWA, WALA ALIYE NAJISI. 

Huo ni unabii alioutoa nabii Isaya juu ya mji wa Yerusalemu kuwa, tangu sasa hakitoingia ndani yake asiyetahiriwa. Sasa unaweza jiuliza, mbona baada ya kutoa unabii huo watu wasiotahiriwa walikua wakiuingia huo mji? Mfano Nebukadreza na watu wake, je! Huo unabii ulikuwa si wa kweli? Jibu ni la! Nabii Isaya alikuwa akiongelea Yerusalemu mpya, mji wa Mungu.

Waebrania 12:22  Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na MJI WA MUNGU aliye hai, YERUSALEMU WA  MBINGUNI, na majeshi ya malaika elfu nyingi, 

Na pia ni mji huo huo, aliooneshwa mtume Yohana akiwa kule kwenye kisiwa cha patmo

Ufunuo 21:2  Nami nikauona MJI ULE  MTAKATIFU, YERUSALEMU MPYA, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. 

Kumbe basi unabii huo wa Isaya ulikuwa ni kwaajili ya YERUSALEMU MPYA, lakini nabii hakuishia hapo tu, bali aliendelea mbele na kusema kuwa, ASIYETAHIRIWA hatoingia katika huo mji, sasa kutahiriwa kunapozungumziwa hapo sio kule kutahiriwa kimwili kama ambavyo Mungu alivyompa agano hilo Ibrahimu. Bali kutahiriwa kunapozungumziwa hapo ni kwa namna ya kiroho, yaani mioyo yetu na masikio yetu, na ndio maana Stephano aliwaambia Wayahudi ambao walitahiriwa kwa jinsi ya mwili kuwa, hawajatahiriwa

Matendo Ya Mitume 7:51   Enyi wenye shingo gumu, MSIOTAHIRIWA MIOYO WALA MASIKIO, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. 

Je! Na wewe umetahiriwa moyo wako na masikio yako. Kama bado fahamu kuwa, hutouingia huu mji mtakatifu wa Mungu.

Sasa unatahiriwaje? Kwanza ni kwa kumwamini Bwana Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa Maisha yako na kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi na kisha kupokea kipawa cha Roho mtakatifu. Govi la zunda ni kila aina ya dhambi iliyopo ndani yetu, hivyo mwanamke na mwanaume ambaye ana dhambi hizi ndani yake anapaswa aondolewe hilo govi (dhambi) kwa Roho mtakatifu kwani yeye atakufanya kuwa mtakatifu kama yeye alivyo.

Ndugu yangu, ukijiona kuwa wewe bado ni mlevi, mwasherati, mtukanaji, una chuki na vinyongo na watu na hutaki kusamehe, basi fahamu kuwa hujatahiriwa bado na hutouingia huu mji mtakatifu wa Mungu.

Wewe mchungaji unayezini na washirika wako Kanisani, na kutokemea dhambi Kanisani kwako basi fahamu kuwa bado hujatairiwa, wewe unayewaomba watu waliokufa, wewe unayeenda kwa waganga, na wewe uliye mchawi, fahamu kuwa hujatairiwa bado na hutouingia huo mji mtakatifu kwani maandiko yanasema katika 

Ufunuo 21:27  Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo. 

Hivyo Kama bado hujatairiwa usifanye shingo yako kuwa ngumu ndugu yangu, amuoa leo ndani ya moyo wako kuacha dhambi zako zote kwa kudhamiria kutokuzitenda na kumwamini Bwana Yesu na kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi kwenye kanisa lolote la kiroho lililopo karibu nawe.

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

NA HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO YONA.


BASI WAKIWAAMBIA, YUKO JANGWANI, MSITOKE; YUMO NYUMBANI, MSISADIKI. 

KAMA YOSHUA ANGALIWAPA RAHA, ASINGALIINENA SIKU NYINGINE BAADAE. 


ALIKUWA HAMJUI BWANA BADO, NA NENO LA BWANA LILIKUWA BADO HALIJAFUNULIWA KWAKE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *