JE! MAPAMBO YA VITO NI DHAMBI?

Vito ni vitu vya nakshi nakshi ambavyo huvaliwa katika mwili kwa lengo la kujipamba, jina hili hutumiwa kwa vitu vyote vyote ambavyo hutumika katika kumpamba mtu, kwa lugha ya kiingereza ni “Jewelry” na mfano wa vitu kama hivi ni hereni, mikufu, bangiri n.k

Sasa swali ni je, kwa mwanamke wa kikristo ni dhambi kuvaa vitu hivi?

Jibu ni ndio, ni dhambi mbele za Mungu kwa mwanamke wa kikristo kuvaa vitu hivyo. Ukisoma maandiko katika agano la kale utagundua kuwa, wana wa Israel (uzao wa Ibrahimu), hawakua wakivaa vitu hivi katika utamaduni wao, hili tunaweza lithibitisha katika kitabu

Waamuzi 8:24 Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.)

Unaona hapo? Biblia inasema walikuwa na pete za masikio za dhahabu KWASABABU WALIKUA NI WAISHMAELI. Kumbe kwa wana wa Israel ilikua si kawaida yao kuvaa hivyo vitu isipokuwa watu wa mataifa kama hao waishaeli, lakini pia hata kipindi kile Ibrahimu alipomtuma mtumwa wake akamtafutie mwanae Isaka mke (mwanzo 24), utagundua kuwa, yule mtumwa na yeye alikua ni mtu wa mataifa na hakumjua kwa undani sana Mungu wa bwana wake Ibrahimu, na ndio maana alimpatia Rebeka pete ya sikio nusu shekheli na vikuku (mwanzo 24:22 ), kwa sababu ulikuwa ni utamaduni wao watu wa mataifa, hivyo, alivibeba vitu hivyo na kwenda kumpa Rebeka kwani ilikua ni kitu cha kawaida kwao watu wa hapo kaanani lakini kwa wana wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo haikuwa hivyo kama tulivyoona katika WAAMUZI 8:24

Sasa na wewe pia mwanamke uliyeokoka na kumwamini Bwana Yesu fahamu kuwa wewe pia ni wa uzao wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa imani kama ilivyoandika katika

Wagalatia 3:7 Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.

Mwanamke uliyeokoka, wewe ni wa uzao wa Ibrahimu kwa hiyo imani ya Bwana Yesu, na wale wasio mwamini Bwana ni watu wa mataifa. Kama ambavyo wana wa Israel hawakuenenda kama mataifa katika vitu hivyo na ndivyo na wewe dada/mama inavyokupasa kutokuenenda kama mataifa kama ilivyoandikwa katika

Waefeso 4:17 Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao;

Dada/mama hayo mahereni si yako wewe, waachie mataifa wasiomjua Bwana, hiyo mikufu waachie wadada wa mataifa wasio mjua Bwana, hayo mabangili si yako waachie mataifa wasio mjua Bwana, hizo wigi si zako iachie dunia.

Jambo hilo hilo biblia limethibitisha tena kwa uwazi kabisa katika

1 Petro 3:3 Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na KUJITIA DHAHABU, na kuvalia mavazi;

1 Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, WALA KWA DHAHABU NA LULU, wala kwa nguo za thamani;

Wanawake wanaoambiwa hayo ni wale wanao utii uchaji wa Mungu yaani wale walio mwamini Bwana na kuoshwa kwa damu yake. Kinyume cha wanawake wasio utii uchaji wa Mungu na imani ya Bwana wetu Yesu kristo ndio hao wanao jipamba kwa hivyo vitu, ukisoma katika

Ufunuo 17:4 Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, AMEPAMBWA KWA DHAHABU, NA KITO CHA THAMANI, NA LULU, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.

Sasa jiulize kwanini mwanamke huyo kahaba amepambwa kwa hivyo vitu? Jibu ni kwamba hautii uchaji wa Mungu.

Hivyo ni dhambi kwa wewe Mwanamke uliyeokoka kuvaa vitu hivyo, baki katika hali yako ya asili Bwana aliyokuumba.

BWANA akubariki.

Shalom


Mada zinginezo:

Kwanini biblia inalitambua kanisa kama mwanamke?


KWANINI MNANIITA BWANA, BWANA, WALAKINI HAMYATENDI NISEMAYO?


Kwanini wale askari hawakumvunja miguu Bwana Yesu?(Yohana 19:36)


Kulingana na Mathayo 5:29, Je! viungo vyetu vikitukosesha tuvikate?

2 thoughts on - JE! MAPAMBO YA VITO NI DHAMBI?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *