Mana ni nini katika maandiko?

SWALI: Mana ni nini katika biblia? na inafunua kitu gani kwetu sisi wakristo wa sasa hivi?

JIBU: Mana kilikua ni chakula (mkate) ambacho Kilishushwa na Mungu kutoka Mbinguni na kuwalisha wana wa Israel wakiwa katika safari yao ya kutoka Misri kuelekea nchi ya ahadi. 

Kutoka 16:4   Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. 

Soma tena 

Yohana 6:31   Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. 

Soma tena

Kutoka 16:15   Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle. 

Sasa Bwana alifanya hivyo ili kufunua kitu fulani katika roho na kitu hiko sasa tunakuja kufahamu katika agano jipya. Tunasoma

Yohana 6:48  Mimi ndimi chakula cha uzima. 

49 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. 

50 Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. 

51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. 

Umeona hapo? Kumbe mana ilikuwa inamfunua au kumwakilisha Bwana wetu Yesu Kristo.  Wana wa Israel katika safari yao walikula chakula kilichoshuka kutoka Mbinguni lakini cha ajabu walikufa, sasa kuna chakula kingine ambacho kimeshuka kutoka Mbinguni, lakini  kwa sasa hivi mtu atakayekula chakula hiki hatokufa, yaani atakua na uzima wa milele ndani yake na chakula hiki si kingine zaidi ya mwili na damu ya Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo. 

Sasa kwa wakati huo Wengi iliwatatiza na hadi kufukia hatua ya kujiuliza kuwa atawezaje huyu kutupa mwili wake?

Yohana 6:52  Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? 

Lakini swali hili halikumfanya Bwana abadili alichokisema na badala yake akaweza na msisitizo na kusema 

Yohana 6:53   Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 

54   Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. 

Unaona hapo faida ya kuula mwili na kunywa damu yake? Ni kwamba tunakua na uzima wa milele ndani yetu na atatufufua siku ya mwisho. Sasa swali ni je! Huu mwili na damu ni kitu gani?  Ili tuelewe tusome

Luka 22:19  Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. 

20  Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] 

Kumbe sasa mwili wake ni mkate (ambao unafananishwa na mana) na damu ni kinywaji kile cha mzabibu na ametoa agizo kuwa, tufanye hivyo kwa ukumbusho wake, hivyo basi sisi kama wakristo ambao tunaelekea nchi yetu ya ahadi hatuna budi kushiriki meza ya Bwana kama wana wa Israel nao walivyoila mana wakati wanaelekea nchi yao ya ahadi 

Je! Mahali ulipo mnashiriki meza ya Bwana kwa ukumbusho wake? Au mchungaji wako anakwambia kuwa hiyo haina haja kwani ilikua ni ishara tu? Ndugu yangu usimsikilize huyo mchungaji toka hapo kwani hili ni agizo la Bwana mwenyewe wala usimsikilize huyo mwalimu wako kwasababu si kila mwalimu au mchungaji ataingia katika ufalme wa Bwana Yesu bali ni wale tu watakao fanya mapenzi yake yaani maagizo yake. 

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

Kivipi tunafarakana na imani kwa kutamani fedha?


Kulingana na ( 1 Petro 4:1) Ni silaha ya nia gani aliyokuwa nayo Kristo ambayo na sisi tunapaswa kujivika? 

Itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa Mbinguni.


Kulingana na Mathayo 5:29, Je! viungo vyetu vikitukosesha tuvikate?

One Reply to “Mana ni nini katika maandiko?
  1. mimi mahali nilipo nakulaka meza, ila tatizo ni kwamba huku kijijini kwetu akunaga DIVAI badala yake tunatumia JUS, je nisawa jambo hilo?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *