Mjumbe wa agano la kwanza alikuwa ni nani?


SWALI: Shalom, Bwana Yesu apewe sifa. Maandiko yanasema kuwa, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu ni mjumbe wa agano jipya, Kwa mfano tukisoma kitabu cha Waebrania 12:24 tunalithibitisha hilo.

Waebrania 12:24 na YESU MJUMBE WA AGANO JIPYA, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili. 

Sasa, kama Kristo ni Mjumbe wa agano jipya, je! Mjumbe wa agano la zamani (la kwanza) alikuwa ni nani?


JIBU: Mjumbe wa agano la kwanza, au agano la zamani, yaani maagizo ya Mungu (torati) alikuwa ni nabii Musa.

Wagalatia 3:19 TORATI ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika KWA MKONO WA MJUMBE. 

Soma tena

Yohana 1:17  KWA KUWA TORATI ILITOLEWA KWA MKONO WA MUSA; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. 

Na agano hilo lilifanyika kati ya Mungu na uzao wa Ibrahimu (Waisraeli) pale ambapo Mungu alipowatoa Misri utumwani na kuelekea nchi ya ahadi. Kwa mkono wa nabii Musa, Waisraeli walipokea maagizo yote (torati) kutoka kwa Mungu kwa utumishi wa malaika ya nini cha kufanya tangu ile siku wanatoka Misri hadi watakapoingia katika nchi ya ahadi, na Musa ndiye aliyekuwa kiunganishi kati ya Mungu na wana wa Israeli, na wakati wote walipokuwa na jambo, basi, walipitia kwa Musa ili kumuuliza Bwana.


Lakini ni nini tunachopaswa tukijue hapo? 


Tunachopaswa kujua hapo ni kuwa, mtu yeyote yule anayetubu na kumwamini Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yake, na kubatizwa kwa jina lake,  huyo anafanyika kuwa mzao wa Ibrahimu (sawasawa na Wagalatia 3:7) na kuingia katika agano la kwenda katika nchi ya ahadi (mbinguni) chini ya Mjumbe wa agano jipya Yesu Kristo, na anakuwa hana budi kuyashika maagizo yote ya Yesu Kristo, Mjumbe wa agano jipya, ili aweze kuingia katika ile nchi ya ahadi. 

Kama vile Yoshua na Karebu walivyoweza kuingia nchi ya ahadi kwa kuyashika maagizo ya Mungu yaliyoletwa na Musa mjumbe, ndivyo na kila mtu aliye mwanini Kristo anavyotakiwa kuyashika maagizo ya Mungu yaliyoletwa na Mjumbe wa agano jipya Yesu Kristo.

Yohana 14:6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. 

Na pia kama vile Musa alivyokuwa kiungo kati ya wana wa Israeli na Mungu kule jangwani, ndivyo na Huyu Mjumbe wa agano jipya Yesu Kristo alivyokuwa kiungo na mpatanishi kati ya Mungu na wadamu wote ulimwenguni, Yeye huwaombea na kwa Kupitia Yeye tunamwomba Mungu wetu wa Mbinguni, 

Yohana 14:13 Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. 

Lakini inasikitisha kuona kuna baadhi ya watu leo hii wanawaomba watu waliokufa (maana Kristo mjumbe wa agano jipya yu hai milele na milele) na mfano wa mtu aliyekufa na wanaomwomba ni Maria, utawasikia wakimwomba “Maria mama wa mungu, UTUOMBEE SISI WAKOSEFU sasa na saa ya kufa kwetu amina” ndugu yangu, nani kakwambia kuwa, Maria anaombea watu kwa Mungu sasa na saa ya kufa kwao? Usiwe mjinga, anayewaombea watu kwa Mungu Yesu Kristo peke yake.

Na tena, kama vile mjumbe wa agano la zamani Musa, alivyochukua damu ya wanyama kama ISHARA YA AGANO.

Waebrania 9:19 Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, 

20 akisema, HII NI DAMU YA AGANO mliloamriwa na Mungu. 

Ndivyo ambavyo mjumbe Huyu wa agano jipya Yesu Kristo, alivyomwaga damu yake (si ya wanyama tena) kama ISHARA YA AGANO pale msalabani kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu na kutuamuru tufanye kama alivyosema kwa ajili ya ukumbusho wake tunaposhiriki meza ya Bwana.

1 Wakorinto 11:25 Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni AGANO JIPYA KATIKA DAMU YANGU; FANYENI HIVI KILA MNYWAPO, kwa ukumbusho wangu. 

Lakini inasikitisha kuona baadhi ya watu kutokufanya maagizo haya na mengine mengi kama vile, kutawadhana na miguu, ubatizo wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, Wanawake kufunika vichwa Wakati wa ibada, kujitenga na udunia, kuwa na upendo, kutokuwa na moyo wa kusamehe, vinyongo, fitina, pombe, anasa, fashion, miziki ya kidunia, uongo, rushwa, uzinzi, matusi, uchawi, kwenda kwa waganga, umbea, usengenyaji n.k na tunadai kuwa, tupo katika safari ya kwenda katika nchi ya ahadi, hapo tunajidanganya tu na kamwe hatuwezi fika huko kama tusipotaka kubadilika. 

Hivyo tumwombe Bwana atupe nguvu ya kujikana nafsi zetu na kijitwika misalaba yetu na kumfuata Mjumbe wa agano jipya kila siku katika maisha yetu.

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

 +255652274252/ +255789001312



Mada zinginezo:

LAKINI KWA NENO LAKO NITAZISHUSHA NYAVU.


UMESHAIFAHAMU NA KUIPOKEA BARAKA YA IBRAHIMU KATIKA MAISHA YAKO .



KWANINI MNANIITA BWANA, BWANA, WALAKINI HAMYATENDI NISEMAYO?


Kwanini Nabii Eliya alitumwa sarepta kwa mjane katika mji wa sidoni?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *