UMESHAIFAHAMU NA KUIPOKEA BARAKA YA IBRAHIMU KATIKA MAISHA YAKO .

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo litukuzwe milele na milele, nakukaribisha katika kujifunza neno la Mungu na leo tutajifunza juu ya baraka ya Ibrahimu aliyoahidiwa na Mungu na kama tumeipokea katika siku hizi za mwisho ama la! Na ahadi yenyewe tunaisoma katika…

Mwanzo 22:18 NA KATIKA UZAO WAKO MATAIFA YOTE YA DUNIA WATAJIBARIKIA; kwa sababu umetii sauti yangu. 

Mungu baada ya kumjaribu Ibrahimu na Ibrahimu kushinda, Mungu alimbariki Ibrahimu kwa baraka mbali mbali, lakini kuna baraka moja ambayo aliambiwa na Mungu kuwa, kupitia uzao wake, MAKABILA YOTE YA DUNIA YATABARIKIWA. Lakini kimsingi ahadi ya baraka hiyo, Mungu alishamwahidi Ibrahimu tangu wakati ule aliomwambia aende katika nchi atakayomwonesha..

Mwanzo 12:3  nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; NA KATIKA WEWE JAMAA ZOTE ZA DUNIA WATABARIKIWA. 

Anaposema katika uzao wa Ibrahimu jamaa zote za dunia zitabarikiwa, anamaanisha kuwa, makabila yote duniani yatabarikiwa kupitia uzao wa Ibrahimu, yaani wachanga, wapare, wachina, n.k. Sasa Kwa kawaida, hakuna mtu anayechukia baraka, kila mtu hupenda baraka, hata mimi pia, watu tunapenda tubarikiwe na tuwe na marafiki bora, familia bora, afya njema, maisha mazuri, n.k hivyo basi hata baraka hiyo ambayo inawahusu watu wote ulimwenguni hakuna mtu ambaye asiyeitaka.

Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba, baraka hii Mungu aliiachilia muda mrefu sana duniani kwa watu wa makabila yote ulimwenguni, ila cha kushangaza ni kuwa, watu bado hawajaifahamu wala kuipokea baraka hii (labda huenda ibilisi kawafumba watu macho wasiweze kuitambua kama ilivyo tabia yake ya kutokutaka watu kupokea baraka kutoka kwa Mungu)  Ila baraka yenyewe ni ipi hasa? Kwasabubu kama ni katika uzao wa Ibrahimu, basi tulitegemea ingekuwa kwa Isaka, Yakobo, Rubeni, n.k lakini haikuwa hivyo, sasa ni ipi baraka hiyo?  Tusome..

Wagalatia 3:14 ili kwamba BARAKA YA IBRAHIMU IWAFIKILIE MATAIFA KATIKA YESU KRISTO , tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani. 

Soma tena

Matendo Ya Mitume 3:25 Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Ibrahimu, Katika uzao wako kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa.

 26 Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake. 

Umeona? Kumbe baraka ambayo Mungu aliyoiahidi kwa watu wa makabila yote duniani ni Yesu Kristo, kwa wangoni, wasambaa, wafaransa, wamisri, n.k na ndio maana leo hii kila kona ya dunia utasikia habari zake Bwana Yesu.

Swali ni je! Umeshaipokea baraka hii kutoka kwa Mungu kwenye maisha yako? Kama bado unangojea nini? Kumbuka, watu huwa hawalazimishwi kupokea baraka isipokuwa wanazitafuta kwa nguvu, mfano; Yakobo alivyoshindana na malaika ili abarikiwe. Hivyo na wewe leo hii, usikiapo baraka hii, basi, ni muda wa kuifurahia kama unavyofurahia baraka zingine katika maisha yako, ni muda wa kufanya maamuzi ya mapema ya kuipokea baraka hii.

Utaipokeaje sasa baraka hii Kutoka kwa Mungu? Jibu ni rahisi sana, unachotakiwa kufanya ni kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kuziacha kabisa, kama ulikuwa ni muongo unacha, unaamua kuacha ulevi, chuki, husuda, majivuno, anasa, kiburi, dharau, uzinzi na uasherati, rushwa, disco, kusengenya watu, matusi, kutazama picha za ngono, kunyoa viduku, kuvaa vimini na suruali kwa wanawake, kucha bandia make up, n.k kisha kumwamini Bwana Yesu ambaye ndiye baraka kwa ulimwengu wote, kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu sawasawa na matendo 10:48 

Kumbuka tunaishi katika siku za mwisho na Bwana yupo mlangoni kurudi muda wowote na saa yoyote, hivyo, jiweke tayari kwa kuipokea baraka hii na kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.

+255652274252/ +255789001312

Bwana akubariki, Shalom.


MADA ZINGINEZO:

Nini maana ya “Msitweze unabii”?(1Wathesalonike 5:20)


Je! Yohana mbatizaji alibatizwa na nani?


KWA SABABU NALIWAOGOPA WALE WATU, NIKATII SAUTI YAO. 

4 thoughts on - UMESHAIFAHAMU NA KUIPOKEA BARAKA YA IBRAHIMU KATIKA MAISHA YAKO .

LEAVE A COMMENT