SWALI: Nina maswali yafuatayo ambayo naomba msaada wa ufafanuzi, swali la kwanza ni je ufalme wa MUNGU ni nini? Swali la pili ni kwamba, kwa nini ufalme wa MUNGU utakuwa ndani yetu, je ni Roho Mtakatifu ndiye anayezungumziwa hapa au? Na swali langu la tatu ni je, ufalme wa MUNGU ulikuja kipindi gani?
Shalom wapendwa wa Bwana!
JIBU: Tuanze na kipengele cha kwanza kinachouliza ufalme wa Mungu ni nini?
- UFALME WA MUNGU NI NINI?
Kabla ya kujifunza kuhusu ufalme wa Mungu tupate ufahamu kidogo kuhusu neno ufalme. Ufalme ni mamlaka inayotawala, Mfano unaposema ufalme wa Babeli maana yake Babeli anatawala, au unaposema ufalme wa Daudi maana Daudi anatawala, yuko juu ya yote, anahukumu.
Ufalme unaweza kuwa na nguvu au ukawa dhaifu. Ukiwa na nguvu maana yake umestirika na maadui, ulinzi wake ni imara, na ukiwa dhaifu maana yake ni rahisi kuangushwa.
Kila ufalme au utawala una utamaduni, desturi na katiba yake yaani jumla ya mambo yote yaliyo haki kuyafanya na jumla ya mambo yote yasiyo haki kuyafanya na hukumu juu ya mambo yote yasiyo haki. Mfano katika nchi ya Ujerumani si kosa mfungwa kutoroka gerezani kwa sababu wanatafsiri kuwa ni haki ya kila mwanadamu kutafta uhuru, ila tu mfungwa asivunje au kudhuru mtu wakati wa kutoroka kwake, hata akikamatwa anajaribu kutoroka bila uharibifu hashitakiwi, anaweza kushitakiwa kwa ule uharibifu alioufanya peke yake.
Lakini jambo hilo si haki kwa nchi kama Tanzania, Kutoroka au jaribio lolote la kutoroka lina adhabu endapo mtorokaji atakamatwa. Na mfungwa siku zote ni mtu yeyote aliyehukumiwa kwa kwenda kinyume na katiba ya nchi husika.
Hiyo ni mifano ya falme za dunia, zipo falme katika upande wa rohoni, nazo ni mbili tu. Falme hizi ni Ufalme wa Mungu na ufalme wa Shetani. Swali letu linalenga tujue ufalme wa Mungu ni upi au ni nini?
Ufalme wa Mungu ni utawala wa Mungu kwa wanadamu, Vivyo hivyo na ufalme wa shetani ni utawala wa Shetani kwa wanadamu. Falme hizi zote zinalenga kumtawala mwanadamu lakini kwa bahati nzuri au mbaya, Mungu na pia shetani hawapo kwa jinsi ya mwili lakini kwa njia ya imani tuna amini Mungu yupo na Shetani pia.
Waebrania 11
⁶ Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza(Mungu); kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
Lakini ikiwa Mungu au shetani hatuwaoni kwa macho yetu, wanatutawala kwa namna gani?
Biblia ni Neno la Mungu aliye juu limeandikwa kutujulisha yatupasayo kuyatenda na yale yasiyotupasa kuyatenda. Yale yatupasayo kuyatenda tukiyatenda tumekuwa katika ufalme wake maana tunamtii au tunatii ufalme wake. Lakini kama hatuyatendi basi moja kwa moja tunakuwa tunayatenda yasiyotupasa; Na hivyo tunausaliti ufalme wa Mungu. Sehemu ya pili tutajifunza kwa nini nasema tunausaliti ufalme wa Mungu.
Wakati tunamkasirisha Mungu, yupo mwingine aitwaye kwa jina la mungu yaani Shetani, ambaye yeye ufalme wake unajengwa juu ya matendo yote yasiyo haki, Na matendo hayo Mungu aliyaita Dhambi. Hivyo kwa mwanadamu kutenda dhambi moja kwa moja anakuwa milki ya shetani awe anajua au hajui. Sasa, Kwa kuwa Mungu ndiye Muumba wa vyote wala hapana mwingine ila Yeye; Hivyo, Mwanadamu hana chaguo zaidi ya kuutii ufalme wake, ikiwa kwamba hatii, ataangamia kwa hasira yake yeye aliyemuumba.
Bwana Mungu anasema;
Kumbukumbu la Torati 30
¹⁵ Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;
¹⁶ kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, KUENENDA KATIKA NJIA ZAKE, NA KUSHIKA MAAGIZO YAKE, NA AMRI ZAKE, NA HUKUMU ZAKE, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.
¹⁷ Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia;
¹⁸ nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki.
Tumepewa kuchagua, tuna uhuru wa kuamua tuwe ufalme upi, lakini aliyetoa njia zote ni Mungu, upande wowote utakaochagua lazima utakutana na mkono wa Mungu tu. Iwe mkono wa Baraka au laana uzima au mauti. Shetani hana amri juu ya mwanadamu wala hukumu bali yeye pia atahukumiwa na Mungu
Ufunuo wa Yohana 12
⁹ Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye IBILISI NA SHETANI, AUDANGANYAYE ULIMWENGU WOTE; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
Ufunuo wa Yohana 20
¹⁰ Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, AKATUPWA KATIKA ZIWA LA MOTO NA KIBERITI, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.
Kazi ya shetani ni kuudanganya ulimwengu utende yasiyowapasa kuyatenda. Akijua ni hukumu ya namna gani ipo kwa watu hao. Kazi zake huzitenda akishindana na kazi za Mungu pengine anaamini kuna lengo akilifikia atamiliki.
Hapo juu Biblia inaposema tumepewa njia mbili; MEMA NA UZIMA, MAUTI NA MABAYA. Inazungumzia falme mbili zinazotawala, Moja inataka wanadamu watende mabaya ili wapate mauti(kutengwa na Mungu milele), kwa kuwa ndiyo mshahara wa mabaya na mfalme wake huo ni Shetani. Nyingine ni inataka tutende mema tupate uzima, ikiwa na maana uzima haumo ndani yetu(hasa baada ya kifo cha kutengwa na dunia hii) na mfalme huo ni Mungu.
Uchaguzi huo ni sawa kusema, lazima utende mema na kama sivyo uwe tayari kuinywa ghadhabu ya Mungu na kuangamia milele. Kwa ufupi hamna chaguo hapo, kwa sababu hakuna apendaye na kufurahia adhabu na mauti.
Ni wazi kuwa, kila mtu anatamani awe katika ufalme wa Mungu yaani anatamani atende mema ili apate uzima lakini Shetani ndiye azuiae tusimtii Mungu. Na kimsingi hatuna sababu ya kumtwika mzigo shetani maana siye yeye anayezini, kusema uongo, kuiba, kula rushwa, kutamani, kutukana, n.k, bali ni sisi. Hivyo kwa kuwa tumeshatenda dhambi, tumempa shetani nguvu ya kututawala na kutumiliki na kila alitakalo kulifanya analifanya maana tumemkiri kwa matendo yetu awe mfalme wetu.
Hivyo mashitaka aliyonayo shetani akitushitaki mbele za Mungu yana nguvu kwa sababu tumefanya dhambi. Dhambi zetu zinatuelemea kuzipiga mbio za kufikia uzima katika kutenda mema. Tangu Adamu hatuna tumaini katika ulimwengu huu wala ujao, shetani hata akawa mfalme wa dunia yote maana wanadamu wote wayatendayo na ibada zao zimetoka kwa shetani (2kor 4:4)
Ashukuriwe Mungu aliye juu, ambaye licha ya kwamba ulimwengu mzima tulimkataa, tukachagua njia ya mabaya na mauti; bado alituhurumia na kuamua kutuokoa na udanganyifu wa shetani. Yesu Kristo, aliyetumwa na Mungu alikuja awe msaada kwetu, kwa kutusamehe hizo dhambi tulizotenda, akatuondolea mzigo mzito na kutuongezea nguvu kwa Roho wake ili tupige mbio kwa wepesi kuufukia ufalme wa Mungu( Kutenda Mema).
Ufalme wa Mungu upo katika uweza wa kutenda mema, na uweza huo tunaupata kwa njia imani, kumwamini Yesu Kristo atupaye uweza kushinda dhambi. Ufalme wa Mungu ni utakatifu, Maisha pasipo dhambi, Utimilifu!
Tito 2
¹³ tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;
¹⁴ ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, WALE WALIO NA JUHUDI KATIKA MATENDO MEMA.
Hii ni sehemu ya kwanza, Sehemu ya pili itafafanua ufalme ulitoka wapi kisha tutajifunza kama upo ndani yetu au la. Na kama upo, tutajifunza kwa namna gani ufalme wa Mungu upo ndani yetu.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Mawasiliano +255755 251 999 au +255652274252
MADA NYINGINEZO
NENDENI MKAJIFUNZE MAANA YAKE MANENO HAYA ‘NATAKA REHEMA WALA SI SADAKA’
MWANAMKE ATAOKOLEWA KWA UZAZI WAKE, JE! NI UZAZI UPI HUO UNAOZUNGUMZIWA?
MAKANISA NA MAFUNDISHO YA UONGO YANAYOPOTOSHA WATU WENGI NYAKATI HIZI ZA MWISHO (sehemu ya 01)
Barikwa Sana kwa mafundisho mazuri ya neno la Mungu