UFALME WA MUNGU NI NINI, ULITOKA WAPI NA ULIANZA LINI? (Sehemu ya 02)

Shalom!

SWALI: Nina maswali yafuatayo ambayo naomba msaada wa ufafanuzi, swali la kwanza ni je ufalme wa MUNGU ni nini? Swali la pili ni kwamba, kwa nini ufalme wa MUNGU utakuwa ndani yetu, je ni Roho Mtakatifu ndiye anayezungumziwa hapa au? Na swali langu la tatu ni je, ufalme wa MUNGU ulikuja kipindi gani?

Karibu katika sehemu ya pili, leo tutaangalia kipengele cha Ufalme wa Mungu ulikuja kipindi gani.

  1. UFALME WA MUNGU ULIKUJA KIPINDI GANI NA NI KWA JINSI GANI UPO NDANI YETU?
    Ufalme wa Mungu ulianza wakati Mungu alipomuumba Adamu, alimpa mipaka ya ufalme wake unapoishia

Mwanzo 2
¹⁶ Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
¹⁷ walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.

Hapo inaonyesha dhahili uzima upo katika neno la Mungu(Ufalme wa Mungu), na nje ya Neno lake kuna mauti. Kama Hawa angetii angekuwa anaishi hata leo. Lakini alipoingia nje ya Neno la Mungu, akafa.

Shetani alimwekea ujuzi mwingine ili atamani kufanya jambo alilokatazwa kufanya, na uzazi wake wote wanakufa. Kumbuka kosa alilolifanya na adhabu ya kifo ilikuwa kwa Adamu au Hawa peke yake, yaani atayekula lile tunda. Lakini na sisi kizazi chake kwa nini tunakufa?

Warumi 5
¹² Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; NA HIVYO MAUTI IKAWAFIKIA WATU WOTE KWA SABABU WOTE WAMEFANYA DHAMBI;

Sote tumefanya dhambi, hivyo sote tumetoka katika ufalme wa Mungu, tupo ufalme wa shetani ambaye tayari yuna mauti ndani yake na sisi tunarithi ile mauti. Na njia pekee ya kuurudia ufalme wa Mungu ni kuondoa dhambi tulizozifanya na kisha tusitende tena.

Njia ya kuondoa dhambi tulizozifanya ni kwa njia ya Damu; tangu Adamu, damu ya wanyama ilitumika, yaani uhai wa mnyama badala ya uhai wetu. Ndio agano pia ambalo Mungu aliingia na wana wa Israeli wakati wa Musa.

Ufalme wa Mungu ukaja tena wakati wa Musa, kuwarejesha watoto wa Ibrahimu kutenda mema. Kipindi hiki ilikuwa ni kwa taifa moja tu ambalo ni Israeli. Mungu aliweka sheria nyingi sana kuliko mara ya kwanza, ili kuwazaa tena katika ufalme wake kutoka katika ule wa giza. Kwa kuwa wakati huu mavumbuzi ya dhambi yalikuwa mengi, vivyo hivyo na sheria nazo zilipaswa kuwa nyingi.

Mungu akafanya agano nao, maneno ya agano Musa akayaandika yawe ukumbusho siku zote; ndiyo torati. Lakini Israeli hawakudumu katika ahadi hiyo, wakadanganyika, wakageuka na kumrudia shetani tena, wakamtenda Bwana kwa hiana. Mungu alimfunulia nabii Ezekieli mambo ya hiana waliomtendea wana wa Israeli.

Ezekieli 17
² Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali;
³ useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi;
⁴ akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi.
⁵ Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto.
⁶ Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko.
⁷ Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha.
⁸ Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri.
⁹ Basi nena wewe, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Huo utafanikiwa? Yeye hataing’oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ili ukauke? Kwamba majani mabichi yake yote yachipukayo yakauke, hata ikiwa hana nguvu nyingi, wala watu wengi wa kuung’oa na mizizi yake?
¹⁰ Naam, tazama, ingawa umepandwa, je! Utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo wa mashariki utakapoupiga? Naam, utakauka katika matuta hapo ulipopandwa.

Mungu alinena mithali akijifananisha na huyo tai wa kwanza, aliwaleta wana wa Israeli(mzabibu) kutoka ufalme wa shetani, akawapa kila kitu(kuwapanda kando ya maji mengi). Lakini tai mwingine(Shetani) alikuwa ametulia mahali, Isaraeli alipomwona akamgeukia ili ale na kunywa kutoka kwake. Mungu akawauliza, mtafanikiwa? Hivyo ndivyo walivyomsaliti Mungu/Ufalme wa Mungu.

Ni dhahiri hawakufanikiwa, Ndipo Mungu akawaonea huruma maana nao ni mwili. Bwana Mungu, akaahidi katika siku zijazo kuwapa Roho wake ili atufundishe kuzishika sheria, hukumu na amri zake kwa usahihi.

Ezekieli 36
²⁶ Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.
²⁷ NAMI NITATIA ROHO YANGU NDANI YENU, NA KUWAENDESHA KATIKA SHERIA ZANGU, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.

Habari hizi zilitimia kwa kuja kwa mkombozi, Yesu Kristo ambaye Roho wa Mungu alikuwa juu yake(Isaya 42:1) kabla ya kuja juu yetu yaani ndani yetu. Roho wa Mungu ndiye Roho mtakatifu, na kuwako kwa Roho mtakatifu ndani yetu kunatupa nguvu ya kuuteka ufalme wa Mungu. Ndio maana utaona mafarisayo waliokuwa wanausubilia ufalme wa Mungu wakitaraji kupata raha juu ya maadui zao(Maana walizania utakuwa kama huu tulionao wa kidunia)

Luka 17
²⁰ Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza;
²¹ wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, UFALME WA MUNGU UMO NDANI YENU.

Hilo ni jibu la swali letu, Ufalme wa Mungu upo ndani yetu. Lakini uweza kujiuliza, umo ndani yao namna gani wakati Yeye(Kristo) mwenyewe alikuwa akiwahubiri wamwamini wasipotee bali wawe na uzima wa milele? Jibu ni rahisi tu, hawawezi kuufikia/kuuteka bila Yeye. Torati ilikuwa imegoshiwa kwa mapokeo lukuki, mafundisho yaliyotolewa ni maagizo ya wanadamu, yaliyo ya muhimu yakafanywa manyonge na mapokeo yakatukuzwa na maarifa ya kweli yakakosekana.

Yeremia 8
⁸ Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, KALAMU YENYE UONGO YA WAANDISHI IMEIFANYA KUWA UONGO.

Hivyo hakuna aliyeijua kweli, adili, imani, rehema, tangu kuhani aliye mwalimu wa torati hata taifa lote. Watu wakakosa kuijua kweli kwa kuwa Kuhani aliyakataa maarifa (Hosea 4:6)

Kuwepo kwa Roho mtakatifu tunaweza leo kuyaelewa haya na kuyaishi, Pasipo Roho mtakatifu bado mtu atakuwa kama hao mafarisayo tu. Warumi 8:9 inasema Asiyekuwa na Roho wa kristo, huyo si wake, maana yake hata kama amemwamini Yesu hawezi kuingia ufalme wa Mungu, hawezi kufikilia ukamilifu wote.

Hivyo ufalme wa Mungu umekuwepo ndani yetu wakati wote, tukijua kutenda mema lakini hatutendi wala hatuna nguvu za kutenda mema. Hivyo Roho mtakatifu kwa kuwa ndiye anatupa uwezo huo wa kufanyika watoto wa Mungu, ni sahihi kusema ndiye Ufalme wa Mungu ndani yetu.

MADA NYINGINEZO

UFALME WA MUNGU NI NINI, ULITOKA WAPI NA ULIANZA LINI?(sehemu ya 01)

WEWE HU MBALI NA UFALME WA MUNGU.

MAKANISA NA MAFUNDISHO YA UONGO YANAYOPOTOSHA WATU WENGI NYAKATI HIZI ZA MWISHO (sehemu ya 04)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *